



Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyoanza Agosti 20 inaelekea ukingoni na timu nyingi zimebakiza mechi tatu tu kabla ya kukamilisha ratiba ya msimu huu.
Klabu zitakazomaliza katika nafasi mbili za juu katika msimamo wa ligi hiyo zitapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika na pia ya Kombe la Shirikisho barani.
Nyingine mbili zitakazomaliza mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo zitateremka daraja na hadi sasa, tayari kuna baadhi ya timu ziko katika vita kali ya kupigania kubaki ligi kuu. Simba, Azam na Yanga ndizo timu tatu pekee kati ya 14 zinazoshiriki ligi hiyo ambazo hadi sasa zina nafasi ya kutwaa ubingwa.
Hata hivyo, wakati ligi hiyo ikielekea ukingoni, kumeendelea kuibuka hofu ya kutokea vitendo viovu vya upangaji matokeo kwa maslahi ya baadhi ya timu.
Kwakuwa ni timu mbili tatu tu ndizo zinazoelekea kupigania ubingwa, sisi tunadhani kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa kuongeza umakini zaidi sasa ili kudhibiti dalili zozote za kuwepo kwa huruma ya timu zisizokuwa na cha kupoteza dhidi ya timu zinazosaka ubingwa au kukabiliwa na tishio la kuteremka daraja.
Kwamba, katika mechi ambazo timu zinasaka ubingwa na zile zinazopigania kubaki ligi kuu zitacheza dhidi ya timu nyingine zilizopoteza matumaini ya ubingwa na pia zisizokuwa na hofu ya kuteremka daraja na kucheza ili kukamilisha ratiba tu, wahusika wanaweza kupanga kirahisi mbinu fulani za nje ya uwanja ili kubebana.
Ushahidi huwa mgumu kupatikana, lakini TFF kupitia kamati yake ya ligi wanalo jukumu la kuhakikisha kuwa vitendo vya aina hiyo havitokei.
Tunaamini kwamba TFF ina wataalam wanaofahamu kwa kina athari zinazoweza kutokea pindi timu moja ikibebwa na kutwaa ubingwa kwa njia hiyo; ama nyingine ikabaki ligi kuu kwa kupitia mlango wa nyuma.
Kwa kukumbushia, mbali na kukiuka kanuni za ligi, miongoni mwa athari zinazoweza kutokea pindi timu zikiachiana ni kupatikana kwa bingwa wa ligi asiye na hadhi ya kweli ya kuliwakilisha taifa katika michuano ya kimataifa.
Nyingine ni hatari mbaya zaidi ya ligi hiyo kupoteza heshima yake machoni mwa wadau na hatimaye kuwakimbiza wadhamini badala ya kuwavuta wengine wengi zaidi.
Sisi tunaamini kwamba TFF haiko tayari kuona ligi yake ikikumbwa na madhila ya namna hii.
Kwa sababu hiyo, tunaamini kuwa kamwe TFF haitaruhusu pia kuona ubabaishaji wa aina yoyote ukipata nafasi. Hilo likiwezekana, washindi wa kweli watapatikana katika ligi hiyo yenye hadhi ya juu kuliko zote kwa ngazi ya klabu nchini.
Ligi hiyo pia itaendelea kuwa na wawakilishi wanaostahili katika michuano ya Afrika na wadhamini watakuwa hawajutii uamuzi wao wa kuwekeza katika maendeleo ya mchezo huo nchini.
Tunadhani kwamba miongoni mwa mbinu muafaka za kuhakikisha kuwa hakuna ubabaishaji utakaofanyika wakati wa kuelekea kileleni mwa ligi kuu ni kuhakikisha kwamba mechi zote zinachezwa kwa wakati na kamwe hakuna 'viporo'. Kila mechi ichezwe katika siku na wakati uliopangwa.
Kamati ya Ligi ya TFF ihakikishe vilevile kuwa maafisa wa kusimamia mechi hizo wanaandaa ripoti sahihi zitakazosaidia uchunguzi makini pindi malalamiko ya kubebana yakijitokeza. Kama ikithibitika, wahusika wote wachukuliwe hatua kali kwa manufaa ya mchezo wa soka na pia kuwa fundisho kwa wengine.
Viongozi wa klabu zilizo katika mbio za kuwania ubingwa na wanachama wao wanapaswa pia kupinga bila woga aina yoyote ya ujanja wa kupata ushindi utokanao na ‘fitna’ za nje ya uwanja.
Watambue kuwa wakiacha kushinda kwa njia ya kawaida ya kuvuja jasho uwanjani, watakuwa wameshiriki katika kitendo kibaya cha kuangamiza maendeleo ya soka nchini.
Tunasisitiza kuwa TFF, klabu na wadau wengine wa ligi kuu wanapaswa kuongeza umakini ili kuzuia jaribio lolote la kubebana. Kwa kufanya hivyo, taifa litapata bingwa sahihi wa kuliwakilisha vyema taifa katika michuano ya kimataifa.