



Michezo ya Olimpiki 2012 iliyokuwa ikifanyika katika jiji la London nchini Uingereza ilimalizika jana na kama ilivyotarajiwa, Tanzania haikuambulia medali yoyote baada ya wanamichezo wake saba kufanya vibaya katika michezo yote waliyoshiriki.
Wawakilishi wa Tanzania katika michezo ya riadha, kuogelea na ngumi hawakufika popote. Bondia Selemani Kidunda alitolewa mapema katika hatua ya mchujo, kama ilivyokuwa kwa Zakia Mrisho aliyekuwa akishiriki mbio za mita 5,000 kwa wanawake. Waogeleaji wawili, akiwemo Magdalena Moshi, pia hawakufurukuta.
Matokeo mabaya yalijitokeza tena jana wakati wanariadha watatu wa Tanzania, ambao ni Mohamed Msenduki, Faustine Mussa na Samson Ramadhani walipokosekana hata katika orodha ya 10-bora ya wale walioshiriki mbio ndefu za marathon. Badala yake, wanariadha kutoka kwa majirani zetu Uganda (waliotwaa dhahabu) na Kenya waliotwaa medali zote mbili za fedha na shaba waling'ara zaidi.
Kwa ufupi, pigo la jana katika mbio za marathon lilimaanisha kuendelea kwa hadithi ileile mbaya, inayosikitisha na pengine kuwaumiza mamilioni ya Watanzania. Nayo ni habari ile ile ya wanamichezo wetu kurejea mikono mitupu, huku wapinzani wakiwakebehi kwa kuwaita wanamichezo wetu wamaobahatika kupeperusha bendera ya taifa nje ya nchi kuwa ni "watalii". Inauma sana!
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mara ya mwisho, walau Tanzania iliambulia medali mbili tatu kwenye michezo ya Olimpiki wakati wa serikali ya awamu ya kwanza, chini ya utawala wa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Inakumbukwa kwamba wakati huo, wanariadha kama Filbert Bayi na Suleiman Nyambui waliitangaza sana Tanzania nje ya mipaka yake kutokana na umahiri wao katika mchezo wa riadha.
Tangu wakati huo wa miaka ya 1980, Tanzania imekuwa ikifanya vibaya zaidi katika Olimpiki na michezo mingine ya kimataifa. Ushahidi wa mfululizo wa kuvurunda kwetu ni juu ya ukweli kwamba, tangu enzi hizo, hakuna medali yoyote iliyowahi kutwaliwa.
Pengine hili si jambo la kawaida. Tunapaswa kujiuliza kwamba, je, kulikoni? Tunakosea wapi?
Kwanini nchi zinazofanana na sisi kijiografia na hata kiuchumi kama za majirani zetu Kenya na Uganda zinatupita katika michezo hii? Kwa kujiuliza maswali ya aina hii, na kama kweli tukiamua kupata majibu yake kwa usahihi, ni wazi kwamba Tanzania haitaendelea kupeleka "wasindikizaji" katika mashindano makubwa kama ya Olimpiki yanayofanyika kila baada ya miaka minne.
Kwa mfano, kama kweli tunataka kuambulia medali kama ilivyokuwa enzi za akina Bayi na Nyambui, Serikali na wadau wote wa michezo nchini wanapaswa kufuata njia zilezile zinazotumiwa na wenzetu katika kuandaa wanamichezo wao.
Lazima tutambue kuwa hakuna njia ya mkato kuelekea mafanikio. Nchi kama China ambayo ina watu takriban bilioni 1.5 na pia kuwa na uchumi mzuri, bado ililazimika kuandaa wanamichezo wake kwa miaka zaidi ya minne ili kupata medali zaidi ya 80 wanazojivunia nazo sasa baada ya kumalizika jana kwa michuano ya mwaka huu ya Olimpiki.
Kenya na Uganda wamejitengenezea mifumo mizuri pia ya kubaini chipukizi wenye vipaji vya mchezo wa riadha, kuwaweka katika shule maalum za mchezo huo na kuwaandaa vya kutosha kwa miaka mitatu na zaidi ili kupata mafanikio waliyo nayo sasa.
Sisi pia hatujachelewa. Ni wakati mwafaka sasa wa kutafuta wanamichezo wetu chipukizi kutoka katika michezo mbalimbali tunayoimudu na kuwaandaa kisayansi kabla ya michezo ijayo ya Olimpiki 2016.
Serikali iwekeze zaidi katika kukuza michezo katika shule zake mbalimbali nchini. Kwa kufanya hivyo, haitachukua muda mrefu kuwapata vijana wenye vipaji vya michezo mbalimbali kama riadha kupitia mashindano ya shule za msingi (UMITASHUMTA) na sekondari (UMISSETA). Baada ya hapo, kwa kushirikiana na sekta binafsi, vijana hao wapewe maandalizi kabambe kama wanavyofanya China, Kenya na Uganda.
Tunadhani kwamba ni kwa kupitia utaratibu huo na mwingine wowote unaofanana na huo tu, ndipo siku moja nasi tutaondokana na aibu ya kufanya vibaya katika kila mashindano ya kimataifa.
Shime. Tuanze maandalizi sasa ili nasi tupiganie kutwaa medali wakati wa michezo ya Olimpiki 2016 badala ya kuendeleza desturi hii mbaya ya kuwa wasindikizaji.