Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mhadhiri awashangaa viongozi kukosa mbinu za kukuza uchumi

30th July 2012
Print
Comments

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) jijini Mwanza, Dk. Odass Bilame, ameeleza kushangazwa kwake na ugumu wa viongozi wa Tanzania kushindwa kujifunza mbinu walizotumia viongozi wa nchi zilizoendelea kwa ajili ya kukuza uchumi wa taifa letu.

Dk. Bilame ambaye kitaaluma ni mchumi alionyesha mshangao huo wakati alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu mafundisho, faida na changamoto katika utekelezaji wa bajeti ya taifa kwa kurejezea taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Alikuwa akiwasilisha mada hiyo kwenye mafunzo ya mwezi mmoja ya uandishi wa habari za biashara na uchumi yanayofanyika katika chuo cha SAUT na kuwashirikisha jumla ya wandishi wa habari 30 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Alisema inashangaza kuona kwamba viongozi karibu wote wa Tanzania wanapata fursa ya kutembelea nchi mbalimbali zilizoendelea, lakini wanashindwa kujifunza mbinu zilizotumiwa na viongozi wa nchi hizo kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wao.

“Binafsi naamini kwamba viongozi wetu wanatembelea na wanao ufahamu kuhusu siasa, maisha na mifumo mbalimbali ya kiuchumi katika nchi zilizoendelea, lakini sielewei ni kwa nini wanashindwa kutumia ufahamu huo kwa ajili ya kuendeleza taifa letu,” alisema.

Akizungumzia mikakati ya kukuza uchumi na kuondoa umaskini hapa nchini, Dk. Bilame alisema serikali inapaswa kuondokana na mazoea ya kuongeza ushuru na kodi katika vitu vidogo vidogo kama sigara, soda, bia, mvinyo na vyakula.

Badala yake ameshauri kwamba serikali inapaswa kutumia sekta kubwa kama vile madini, bandari na utalii kuongeza wigo wa kukusanya mapato ili kukuza uchumi na hivyo kuboresha maisha ya watanzania.

Kwa mujibu wa Dk. Bilame, sekta ya uwekezaji pia ina mchango mkubwa katika kuongeza mapato na kukuza uchumi iwapo itasimamiwa vizuri na kwa uadilifu mkubwa.

Ili kuondokana na hali ya sasa ambapo watendaji serikalini wanasaini mikataba isiyo na tija kwa watanzania wote, alishauri mikataba yote ya uwekezaji inayohusisha makampuni ya nje ipelekwe kwanza bungeni na kujadiliwa na wabunge kabla ya kuidhinishwa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment