Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Miezi mitatu haitoshi kupunguza migogoro ya ardhi kwa majaji 14

24th June 2012
Print
Comments

Kwanza kabisa, ningependa kutumia nafasi hii kupongeza jitihada nzuri zinazofanywa na serikali kupunguza migogoro ya ardhi iliyokithiri katika kila kona nchini.

Ni ukweli usiopingika kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada kupunguza migogoro hiyo kwa kuchukua hatua mbalimbali.

Hatua mojawapo iliyokwishachukuliwa na inayoendelea kuchukuliwa na serikali, ni pamoja na kuimarisha ulinzi katika maeneo ambayo yamekuwa maarufu kwa kukumbwa na migogoro ya mara kwa mara.

Kutokana na jitihada hizo, hivi sasa maeneo hayo, kama yale ya wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro na la hivi karibuni la Ikwiriri wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, kwa kiasi kikubwa yametawaliwa na migogoro ya ardhi.

Kabla ya hapo, maeneo mengi yaliyohusishwa na migogoro ya ardhi, ilikuwa ni kawaida kuingia siku pasipo kusikia yakikumbwa na vurugu.

Vurugu hizo zimekuwa zikisababisha uvunjifu wa amani na watu kujeruhiwa, mali zenye thamani ya mamilioni ya Shilingi kuharibiwa na wakati mwingine kusababisha vifo.

Migogoro hiyo mara nyingi imekuwa ikihusisha wakulima na wafugaji kwa upande mmoja na wananchi na wawekezaji kwa upande mwingine.

Pia imekuwa ikihusisha mtu mmoja mmoja dhidi ya mwingine. Migogoro hiyo ni mingi sana kulinganisha na mingine niliyoitaja hapo juu.

Ni mara chache sana migogoro ya mtu mmoja mmoja kusikika ikiripotiwa na vyombo vya habari.

Zaidi inapokuwa inamhusisha au kuwahusisha watu mashuhuri au maarufu katika jamii.

Baadhi ya maofisa ardhi ni miongoni mwa watu katika jamii, ambao nao pia wamekuwa wakichangia migogoro hiyo kwa kuuza maeneo zaidi ya mara moja na hivyo kusababisha jamii kugombana hata kuchukiana.

Jambo kubwa linalochangia maofisa hao kusababisha migogoro ya ardhi zipo nyingi, kubwa zaidi ni tamaa ya fedha, huku wakijua wanachokifanya ni kinyume cha maadili ya kazi zao.

Hatua nyingine iliyochukuliwa na serikali kupunguza migogoro ya ardhi, ni ile ya Rais Jakaya Kikwete ambapo hivi karibuni aliwateuwa majaji 10 wapya, walioapishwa na Jaji Mkuu, Othman Chande Jumanne wiki hii.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, katika miezi yao mitatu ya mwanzo, majaji hao watapelekwa kusaidia kupunguza kesi katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, ambako kwa sasa kuna majaji wanne tu, huku kesi za ardhi zikifikia 2,200.

Hatua nyingine iliyochukuliwa kupunguza migogoro ya ardhi, ni ule mpango uliotangazwa na Jaji Mkuu Chande hivi karibuni.

Kwamba, Mahakama itaongeza matawi ya Mahakama Kuu. Matawi hayo pamoja na mambo mengine, yatashughulikia migogoro ya ardhi.

Pamoja na jitihada zote hizo zilizo njema, bado nina wasiwasi kuhusiana na majaji hao 10 wapya kama wanaweza kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi nchini kwa kipindi walichopangiwa kushughulikia tatizo hilo kubwa na zito.

Kwa hakika idadi ya majaji walioteuliwa na muda waliopewa kushughulikia kesi zinazohusu migogoro ya ardhi, havitoshi kupunguza migogoro ya ardhi iliyokithiri nchini.

Kwa mfano, Dar es Salaam peke yake tu ni eneo kubwa. Migogoro ya ardhi imejaa kila mahali.

Je, hali ikoje katika mikoa mingine? Ikiwa hali ni hiyo, je, majaji 14 watafanikiwa kiasi gani kupunguza migogoro hiyo? Hilo ni swali linalohitaji kukaliwa kitako na kujadiliwa.

Wasiwasi wangu unatokana na ukweli kwamba, Mahakama kwa muda mrefu sasa kuwa na utaratibu wa kimasihala, ambao umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa kuchelewesha maandalizi ya kesi.

Mara nyingi imeshuhudiwa kesi zikishindikana kusikilizwa kwa wakati si kwa sababu upelelezi wa kesi husika haujakamilika. La! Hasha! Upelelezi unaweza kuwa umekamilika.

Lakini siku, ambayo kesi imepangwa kusikilizwa, jalada la kesi husika linatafutwa na makarani wa mahakama kwenye kabati lilikohifadhiwa, hadi muda wa kusikiliza kesi unaisha, halipatikani.

Matokeo yake muda wa kesi unasogezwa mbele kwa maana kwamba, kesi inapangiwa tarehe nyingine ya kusikilizwa au kwa lugha ya mitaani "Inapigwa kalenda"!Kwa hali hiyo peke yake tu, je, miezi mitatu inaweza kupunguza kwa kiasi gani migogoro ya ardhi iliyokithiri nchini?

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu Chande, ni kwamba, Mahakama bado iko katika mchakato utakaowezesha kuwafikia wananchi kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Teknohama), ambapo watapata taarifa za kesi zao kupitia simu na mitandao ya kompyuta.

Licha ya Jaji Mkuu Chande kueleza kuwa teknolojia hiyo kwamba, tayari imeanza kutumika katika Mahakama Kuu ya Biashara katika usikilizaji wa kesi zake, haijulikani lini itaanza katika mahakama nyingine, ikiwamo Divisheni ya Ardhi.

Kwa hali hiyo, nionavyo mimi, migogoro ya ardhi kwa njia ya mahakama inaweza kupungua iwapo idadi ya majaji itaongezwa kushughulikia kesi hizo.

Hiyo ni kutokana na ukweli ni kwamba, Watanzania wenye sifa ya kuwa majaji wapo wengi sana ndani na nje ya nchi. Na suala la migogoro ya ardhi kama tulivyoona hapo juu ni bado kubwa na zito nchini.

Pili, majaji waliopo wapewe muda mrefu wa kutosha. Na ikiwezekana walipwe muda wa ziada ili waweze kusikiliza kesi hizo.

Kama tatizo ni fedha za kuwalipa, nchi inavyo vyanzo vingi vya mapato, ikiwa ni pamoja na kusheheni rasilimali nyingi, ambazo zinaweza kutumiwa kupata fedha za kulipa mishahara na posho za majaji.

Kwa upande mwingine, migogoro ya ardhi inaweza kupungua kwa serikali kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi na maendeleo ya kiuchumi.

Matumizi bora ya ardhi, ni pamoja na kuainisha maeneo ya mifugo na kilimo. Kwa kufanya hivyo, mfugaji na mkulima, kila mmoja atajua, kwanza mpango huo upo. Pili, watajua wapi pa kuweka mifugo na kuendesha shughuli za kilimo.

Maendeleo ya kiuchumi, ni kuweka mipango itakayomfanya mfugaji auze mifugo yake ili aweze kutumia mapato kufungua biashara, kama ya duka nakadhalika.

Kadhalika, mkulima vivyo hivyo, ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia ya kilimo cha kisasa kupunguza ukubwa wa ardhi, ambayo itamuwezesha kuzalisha zaidi kwenye eneo dogo la ardhi ili kuwezesha mfugaji naye apate eneo la kulisha mifugo yake.

Mpango huo kwa mkulima utamuwezesha kupunguza matumizi makubwa ya ardhi na hivyo, kupunguza migogoro yake. Na la mwisho ni hili. Maofisa ardhi wabadilike na kufanya kazi kwa kufuata sheria za nchi.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment