



Juzi abiria 17 waliokuwa wanasafiri kwa basi la Sabena wakitoka mkoani Tabora kwenda Mbeya walikufa papo hapo baada ya basi hilo linalodaiwa kupakia abiria kupita kiasi kupata ajali. Pia wengine 78 walijeruhiwa kwa viwango tofauti vya majeraha.
Kumekuwa na simulizi mbalimbali juu hasa ya chanzo cha ajali hiyo iliyotokea mchana wa Jumanne wiki hii eneo la Kitunda wilayani Sikonge, wapo wanaosema ni mwendo kasi kupita kiasi, lakini wengine wanasema ni kujaza abiria kupita kiasi, ilhali wengine wakisema ni uzembe wa gari jingine lililokuwa limeegeshwa barabarani bila tahadhari zozote; sababu zote hizi haziondoi ukweli mmoja unaosimama, kwamba maisha ya watu 17 yamekatizwa ghalfa na wengine huenda wakapata vilema vya maisha kwa waliojeruhiwa.
Tunaungana na wasomaji wetu wote kuwapa pole ndugu na jamaa waliopoteza ngugu katika ajali hii, tunawaombea kwa mola ila wapate moyowa subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi; pia tunawapa pole majeruhi na kuwaombea neema ya muumba ili waponde haraka na kurejea katika kazi za ujenzi wa taifa.
Hakika katika safu hii ya tahariri imekuwa kama ada kuadika juu ya majanga haya. Imekuwa kama kawaida, siyo kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa kwa sababu wimbi la ajali katika nchi hii ni kubwa sana. Ajali hizi zimekuwa nyingi kiasi cha watu kuzizoea, ni kawaida kabisa kuona hata pale watu chini ya 10 wanapokufa kwenye ajali vyombo vya habari kuziona kama za kawaida kabisa, kisa, wamezoeza idadi kubwa ya vifo, makumi kwa mamia. Ni kawaida.
Kwa hakika hakuna kifo kidogo kwa maana ya madhara kwa jamii, kila anayekufa ni kiumbe hali, ni nguvu kazi ya taifa, pengine ni tegemeo pekee la familia. Kila anayeondoka katika maisha haya anaacha pengo ambalo kuzimbwa kwake ni vigumu kwa maana ya mchango wake kwa wale waliomtegemea au waliokuwa na mipango mipana kwake.
Tukirejea kwenye ajali ya Sabena kuna maswali mengi sana ya kujiuliza, muda ambao ajali hii imetoea ni mapema sana, ni mchana, ina maana kokote walikokuwa wamepita kuanzia Tabora mjini hadi wanapata ajali takribani km 200 kutoka Tabora mjini kwa hakika walikuwa mengi yakiwa na askari wa usalama barabarani.
Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo akiwamo mwanajeshi mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ameshuhudia kwamba askari wa usalama barabarani walielezwa kuwa basi hilo lilikuwa limekiuka sheria nyingi za usalama barabarani, kwamba lilikuwa limepakia abiria wengi kupita uwezo wake siyo jambo lenye ubishi kwani hata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora ameshuhudia hilo, lakini pia lilikuwa likendeshwa kwa mwendo kasi kupita kiasi.
Pamoja na askari kuelezwa matatizo yote ya basi hilo, liliachwa na kuendelea na safari. Matokeo yake maisha ya watu 17 yamepukutishwa hivi hivi tu. Ni siri iliyowazi kwamba kufumba macho kwa askari wetu kwa kutokuchukua hatua katika matukio kama haya ya jali ya Tabora siyo jambo la bahati mbaya, siyo kughafilika, wala siyo udhaifu wa kibinadamu, ni maamuzi ya makusudi kwa malengo maalum.
Tulipata kusema katika safu hii kwamba kama wadau wakuu watatu wa usalama barabarani wakiamua kuwa makini katika usimamizi wa sheria za usalama barabarani, kwa hakika idadi ya ajali za barabarani zitapungua kwa zaidi ya asilimia 70.
Tulipata kuwataja wadau hawa kwamba namba moja ni askari wa usalama barabarani, namba mbili ni madereva na wamiliki wa vyombo vya moto, na kundi la tatu ni abiria. Kila kundi miongoni mwa haya ana nafasi yake, lakini ni bahati mbaya mwenye nguvu, mamlaka na uwezo wa kulazimisha mambo yatokee ni askari wa usalama barabarani. Hata pale abiria wanapopiga kelele kama ilivyokuwa kwa ajali hii ya Tabora kama askari hawasikii kwa sababu wamewezeshwa kutokusikia, inakuwa ni kazi bure.
Tunachukua fursa hii kuomba hatua zichukuliwe kama taifa kwa kusema ajali hizi sasa basi, inawezekana kama kila mdau miongoni mwetu atatimiza wajibu wake. Hakika ajali hizi siyo amri ya Mungu, tunaweza kuzizuia kabisa kama tukiamua.