


Serikali yala hasara ya Sh. bilioni 69
Fidia ya bima nayo yachakachuliwa
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametoboa siri iliyosababisha atengue uteuzi wa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi, kuwa ni pamoja na kuingia kwa siri mkataba wa ukodishaji wa ndege bila kuijulisha wizara.
Alisema mkataba huo umeisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 69 ambazo zimetokana na matengenezo ya ndege hiyo pamoja na riba.
Akizungumza na wafanyakazi wa ATCL jana jijini Dar es Salaam, Waziri Mwakyembe alisema tangu atengue uteuzi wa Chizi, kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu ambao wanahoji kuwa kaonewa bila kufanya utafiti wa kina kujua ni sababu zipi ambazo zimeilazimu serikali kuchukua maamuzi hayo.
Dk. Mwakyembe alizitaja sababu kuwa ni pamoja na menejimenti ya ATCL kuingia mkataba wa kukodisha ndege bila wizara kujulishwa, pia Chizii alikuwa ameshastaafu kazi tangu mwaka 2002 na kulipwa mafao yake, lakini taratibu za kumrejesha kazini hazikuzingatiwa.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya mendeleo ya ATCL, badala ya kutumika kwa lengo lililokusudiwa uongozi wa shirika hilo uliamua kuzitumia kwa kununua magari ya kifahari.
Aliongeza kuwa sababu nyingine zilizopelekea achukue maamuzi hayo ni kutokana na zaidi ya Dola za Marekani milioni 7 (Sh. bilioni 11.1) ambazo zilitolewa na kampuni moja ya bima kwa ajili ya ndege ya ATCL iliyopata ajali mkoani Kigoma kuanza kuchakachuliwa na menejimenti.
“Nilikuwa nasoma leo (jana) kwenye gazeti moja na pia baadhi ya redio ikawa inazungumzia uamuzi niliouchukua,” alisema na kuongeza: “Tatizo moja sisi Watanzania tunapenda kulalamika tu bila kufanya utafiti, lakini hizi ni propaganda za kipuuzi, hazitanirudisha nyuma wala watendaji wenzangu wizarani.”
Alisema amefurahishwa kwamba wanaolalamikia suala hilo wamelifikisha kwa wabunge ambao ni watu makini ambao hawajadili suala la mtu, bali mambo ya msingi.
Dk. Mwakyembe alisema baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuingia katika Wizara ya Uchukuzi, alipata taarifa kupitia kwenye vyombo vya habari kwamba Tanzania imenunua ndege mpya ya Boeng 737.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo alimwita Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Omari Chambo, ili ampe maelezo kuhusu ndege hiyo, lakini katika hali ya kushangaza alimweleza kuwa hana taarifa zozote kuhusu ndege hiyo, jambo ambalo alisema lilimshitua sana.
Alisema hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali hakuwa na taarifa za ndege hiyo na kwamba hata mkataba wizara imeupata kutoka kwa mtu mwingine nje ya menejimenti ya ATCL.
Alisema mkataba huo wa kukodisha ndege ya Air Bus utaingiza serikali kwenye matatizo makubwa kwa kuwa amebaini ni wa kipuuzi sana na pengine kuliko hata ule wa kampuni ya kufufua umeme wa dharura wa kampuni ya Richmond.
“Nimepata uzoefu mwingine, tumekwenda kukodisha ndege ya Air Bus, ni mkataba wa kipuuzi na haijapata kutokea katika historia, ni wa kipuuzi kupita hata wa Richmond,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema pamoja na kwamba ATCL waliingia katika mkataba huo bila wizara kujua, lakini serikali ilijikuta ikianza kulipa baada ya miezi sita ndege hiyo ikiwa bado nje ya nchi.
“Tanzania inalipa pesa ya kukodisha hiyo ndege maana hii nchi kila mwendawazimu anakuja kuchuma huku, sisi tunalipa kwa pesa ya wakulima na wafanyakazi halafu tunasema wizara isituingilie,” alisema.
Alisema katika hali ya kushangaza ndege imechukuliwa huku wataalamu wa hapa nchini wakijua katika muda mfupi ujao ndege hiyo itakua juu ya magogo kwa matengenezo na ndiyo maana imeruka miezi kadhaa gharama zimeongezeka na Watanzania watalipa kwa sababu ni kichwa cha mwenda wazimu.
Dk. Mwakyembe alisema serikali inadaiwa Sh. bilioni 69 wakati aliyeikodishia ndege amekwisha kufungua kesi mahakamani akitaka kulipwa fedha hizo.
Alisema kutokana na utata wa mkataba wa ndege hiyo, aliwaita wawekezaji na kuwahoji kama je, wakati wanaingia mkataba huo walielezwa kwamba ATCL ni mtu binafsi au ni shirika la umma ambapo walijibu kuwa ni la umma.
Dk. Mwakyembe alisema aliwabana wawekezaji hao kuwa kwanini pamoja na uzoefu wao huo wa uendeshaji wa kampuni ya ndege wameshindwa hata kuijulisha serikali wakati wanaingia mkataba na ATCL ambapo walikiri kuwa wamekosea.
“Tunapata mkataba kutoka kwa watu wa pili ambao ni wawekezaji, lakini siyo ATCL ambayo ilitupa hao wawekezaji, nikaiita menejeimenti ya ATCL lakini hawakufika,” alisema.
Alisema hivi sasa uchunguzi juu ya mkataba huo umeanza kufanyika na kwamba baada ya kuupitia amebaini kuwa serikali itakuwa inalazimika kulipa bima makampuni shiriki yapatayo matano.
NDEGE ILIYOPATA AJALI KIGOMA
“Kilichoniudhi sana tumepata pesa ya bima kutokana na ajali ndege ilitotokea Kigoma zaidi Dola milioni saba, kampuni ya bima ikasema inatuletea hizo pesa kwa awamu ya kwanza dola milioni tatu, tukawaambia ATCL kwamba hizo ziwekwe kwenye akaunti yenu zipelekwe moja kwa moja kwa mtengenezaji wa ndege ili tuwe na ndege mbili,” alisema.
Dk. Mwakyembe alisema licha ya kukubaliana na menejimenti ya ATCL fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti yao, lakini siku mbili baadaye menejimenti ilisema imekuwa vigumu hivyo akawaambia kama haiwezekani waziweke fedha hizo kwenye akaunti ya wizara.
Alisema hata hivyo, licha ya kutoa agizo hilo alipata taarifa kutoka kwa kampuni ya bima kuwa watendaji wa ATCL wameamua kuweka fedha hizo kwenye akaunti yao na fedha zimekamatwa kwa amri ya mahakama.
“Waliokasirishwa na uamuzi niliouchukua ondokeni, simameni..mko wapi,” alisema.
Dk. Mwakyember alisema serikali imechoka kuibeba ATCL, sasa wakati umefika kwa shirika hilo kujizatiti kusimama kwa miguu yake.
“Wizara ndiyo inayolipa mishahara, wizara ndiyo inayotoa pesa za opereation (uendeshaji), we can't go like that (hatuwezi kwenda hivi) ifike muda tuone dalili za ATCL inasimama kwa miguu yake yenyewe. Kama mashirika madogo wameweza kwa nini ATCL ishindwe?” alihoji.
Mbali na Chizi, wengine waliosimamishwa ni Amini Mziray (Mwanasheria); Justus Bashara (Kaimu Mkurugenzi wa Fedha) na Josephat Kagirwa (Kaimu Mkurugenzi wa Biashara).
Alisema kupitia ukiukwaji huo, itaundwa kamati ya wajumbe watatu wenye uelewa wa mambo ya fedha na sheria ili kuchunguza matumizi ya fedha iliyopokelewa kuanzia mwanzoni mwa Mei, mwaka huu.
CHIZI AZUNGUMZA
Saa chache baadaye juzi, Chizi alinukuliwa na Televisheni ya ITV akisema aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo Agosti, mwaka jana, hivyo amepokea na anakubaliana na uamuzi uliochukuliwa dhidi yake.
Kabla ya uteuzi wake, ATCL ilishindwa kuendesha shughuli zake, hivyo akateuliwa kurudisha hadhi ya shirika hilo na kwamba alijitahidi kufanya kazi hiyo kwa uwezo wake.
“Kama uteuzi umetenguliwa nashukuru kwa hilo,” alisema Chizi na kuongeza kabla ya uteuzi wake kutenguliwa alikuwa tayari kishaingia mkataba wa kununua ndege ya pili ya shirika.
“Nawashukuru Watanzania kwa ushirikiano, hususan vyombo vya habari na wote waliokuwa wakifurahia huduma za shirika. Nitachangia kwa njia nyingine ambazo nchi itaona zinasaidia,” alisema Chizi.