Monday Feb 8, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Yanga walia hujuma, kujadili kipigo leo

8th May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga

Kamati ya utendaji ya Yanga inatarajia kukutana leo jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali huku kubwa likiwa ni kipigo cha aibu cha goli 5-0 ilichokipata juzi kutoka kwa watani zao wa jadi Simba katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga alisema jana kuwa wamelazimika kuitisha kikao hicho ili kutathmini ripoti ya kiufundi kutoka katika kamati yao ya ufundi ambayo ilikutana jana jioni chini ya mwenyekiti wake, Mohammed Bhinda.

Hata hivyo, viongozi wa Yanga tangu juzi baada ya kipigo walikuwa hawapatikani kuzungumzia mustakabali wa klabu yao na timu nzima hasa kufuatia msimu wa ligi kumalizika huku habari kutoka ndani zikidai kuwa wachezaji watahojiwa kuhusiana na tuhuma za kufanya hujuma katika mechi hiyo.

Wachezaji wa timu hiyo kwa nyakati tofauti waliliambia gazeti hili kuwa kuwa matokeo ya mchezo wao wa juzi yanatokana na matunda 'yasiyofaa' ambayo yaliandaliwa na viongozi wa klabu yao.

Kiungo, Haruna Niyonzima, alisema kuwa Yanga imekuwa kwenye hali ngumu katika mechi zote za mzunguko wa pili lakini wachezaji walikuwa wakijituma na kucheza ili kutimiza wajibu wao.

Niyonzima alisema kuwa timu yao ilikuwa ikifanya maandalizi ya mechi mbalimbali kwa kubahatisha jambo ambalo lilikuwa linawaumiza na kukwaza programu ya kocha wao mkuu.

Alisema kuwa endapo hali hiyo itaendelea katika klabu hiyo hata ubingwa wa Kombe la Kagame wanaoushikilia wataupoteza na wala hakuna mchezaji anayestahili kuangushiwa lawama.

"Najua mpira una matokeo ya aina tatu, kinachoniuma mimi ni kufungwa magoli 5-0, tumedhalilika sana na sijui nitapita njia gani nikifika Kigali (Rwanda)," alisema nyota huyo ambaye anatarajia kwenda kujiunga na timu yake ya taifa ya Rwanda inayojiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Tunisia itakayofanyika Mei 18 mwaka huu.

Nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa, alisema kuwa anasikitika sana kupoteza mchezo huo na haamini kilichotokea katika mchezo huo kwa timu yake kupoteza nafasi nyingi.

Nsajigwa alisema kuwa kumalizika kwa msimu huo ndio maandalizi ya msimu ujao ambapo ameutaka uongozi uhakikishe unafanya tathmini kujua kiini cha matokeo mabaya kwa msimu huu uliomalizika.

Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic, ambaye juzi alikaa jukwaani akidai malimbikizo ya mshahara wake, alisema kwamba timu yake ilicheza vizuri kipindi cha kwanza lakini mabeki wa Simba na kipa Juma Kaseja walikuwa makini na kuwafanya washindwe kutingisha nyavu za timu hiyo.

Papic alisema kuwa kipindi cha pili Yanga ilizidiwa na hapo ndipo safu ya ushambuliaji wa Simba ilipofanya kila inachotaka na kusababisha "maangamizi" hayo.

"Penati zote walizopata ni halali, Simba walikuwa wazuri zaidi kipindi cha pili na waliwafanya Yanga wapotee uwanjani," alisema kocha huyo ambaye hajui hatma yake ndani ya timu hiyo.

Hata hivyo, habari kutoka kwenye uongozi wa klabu hiyo unadai kwamba wachezaji wake wameihujumu timu yao na tayari wameshaanza uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo. Wachezaji watakaobainika watachukuliwa hatua kali ikiwemo kutimuliwa  kwenye kikosi hicho.

Wakati huo huo, mechi baina ya Simba na Yanga iliyochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam imeingiza Sh. milioni 260.9, imeelezwa.

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema jana kuwa kiasi hicho cha fedha kimetokana na mashabiki 41,733 walioingia uwanjani kwa kukata tiketi kushuhudia mechi iliyokuwa kati mechi saba za funga dimba ya ligi hiyo.

Wambura alisema kuwa mashabiki wengi walioshuhudia mchezo huo walikata tiketi za viti vya rangi ya bluu na kijani ambazo zilikuwa zinauzwa Sh. 5,000 na walikuwa ni 36,980 huku zile za VIP A zilizokuwa zinauzwa kwa Sh. 40,000 zilinunuliwa 203.

Baada ya makato mbalimbali ikiwemo asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni Sh. milioni 39.7 kila klabu iliambulia Sh. milioni 62.6 wakati TFF ambao ndio wasimamizi wa mechi hiyo walipata Sh. milioni 19.9.

Idadi kubwa ya mashabiki waliohudhuria mchezo huo walikuwa ni wa Simba ambao tayari walikuwa wana raha kutokana na timu yao tayari kutwaa ubingwa wa ligi.

Simba ilitwaa ubingwa huo kutokana na kuwa na pointi 59 ambazo zisingeweza kufikiwa na timu nyingine baada ya Azam iliyomaliza ikiwa ya pili kwenye msimamo ilikuwa na pointi 53 kabla ya mechi yake ya mwisho.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment