



Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajia kuwasilisha hoja binafsi katika Bunge lijalo la bajeti kupendekeza kuanzishwa kwa baraza maalum ya kushughulikia makosa ya rushwa na uhalifu wa uchumi.
Mwigulu alisema kumekuwepo wimbi kubwa la kushuka kwa maadili ya uongozi, hali ambayo inachangia kwa namna moja au nyingine wananchi kupinga vitendo vya rushwa na hujuma nyingine zinazohusiana na mali za umma.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, kutokana na ukubwa wa wimbi hilo na wananchi wengi kuchukia rushwa, ameona ni vyema likaanzishwa baraza maalumu litakaloshughulikia kesi zote ambazo zitahusu vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi.
Mwigulu ambaye pia ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, alisema kuwa ameona kuna haja ya kuwasilisha hoja hiyo kwa kuwa mazingira ya kusikiliza kesi za rushwa yaliyopo kwa sasa yanakwamisha ufanisi katika kushughulikia kesi hizo.
Alivitaja baadhi ya vitu vinavyokwamisha ufanisi wa usikilizwaji wa kesi za rushwa kuwa ni pamoja na msongamano wa kesi mahakamani.
Mbunge huyo alisema kuwa kuchelewa kuamua kesi za rushwa pia huchangia kumjengea mtuhumiwa mazingira ya kutoa rushwa nyingine kwa anayesikiliza kesi yake.
Mwigulu alisisitiza kwamba kuchelewa huko kunachangia pia kuchelewa kutolewa adhabu ambazo ni fundisho watu wenye tabia ya kutoa na kupokea rushwa, hivyo kuongezeka kwa vitendo hivyo.
“Ili kufanikisha suala hilo, ni vyema yakafanyika marekebisho ya sheria ya upelelezi iliyopo hivi sasa na kutumia ushahidi wa mazingira kwa kuwa kutolea ushahidi wa rushwa ni mgumu sambamba na ongezeko la adhabu ya makosa ya aina hiyo kwa watuhumiwa watakapobainika kupatikana na hatia,” alisema.