Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Millya ni tunu ama gamba lililojisitiri Chadema?

18th April 2012
Print
Comments

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Arusha, James Ole Millya, amejiengua kutoka chama hicho na kujiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hatua ya Millya kuihama CCM akiwa pia na nyadhifa tofauti ndani ya chama hicho, imeibua hisia tofauti miongoni mwa wanachama na wasiokuwa wanachama wa Chadema.

Hoja ya msingi inayoishi sasa ni je, hatua ya Millya imetokana na dhamira ya dhati yenye kujikita katika haki za kiraia hususani katika mchakato wa kidemokrasia, kwamba kila mtu ana haki ya kujiunga ama kujiondoa katika chama chochote cha siasa?

Hoja hiyo inaishi kutokana na ukweli kwamba, wapo wanasiasa wengi waliowahi kujiondoa CCM na kujiunga upinzani ikiwemo Chadema, lakini kwa Millya kuna maana tofauti.

Kwanza Millya amedaiwa kuwa mshirika wa karibu sana na kikundi cha watu wachache wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya CCM na ambao wanatakiwa kutekeleza kile kinachojulikana kama ‘kujivua gamba.’

Katibu wa halmashauri Kuu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye, anasema “…kajivua gamba, tunampongeza kwa kuitikia wito wa kujivua gamba. Kila la kheri aendako…”

Kauli ya Nape inadhihirisha wazi kwamba Millya alikuwa mmoja wa washukiwa wa ufisadi ndani ya CCM waliotakiwa kujivua gamba ili chama hicho kibaki safi, kirejeshe mvuto wake na kukubalika zaidi kwa umma.

Lakini Nape haishii kumtaja Millya kama mmoja wa washukiwa waliotakiwa kujivua gamba tu, lakini anasema, “itakumbukwa Millya alikuwa afukuzwe kwenye chama kutokana na aliyokuwa akiyafanya, akapewa karipio ili apate muda wa kurekebisha tabia yake. Kaondoka akiwa chini ya karipio.”

Kauli ya Nape inaweza kutafsiriwa kama kuwepo dalili za njia iliyoandaliwa kwa ajili ya kumtimua Millya kutoka kwenye chama hicho, kilichofanyika (pengine) ni mwanasiasa huyo kijana kuikoa nafsi yake kwa kukimbilia Chadema, abaki katika siasa za ndani ya nchi.

Hivyo changamoto inayoikabili Chadema hivi sasa, ni kwa namna gani Millya atakubalika si kwa viongozi na wanachama peke yao, bali kwa mtazamo wa umma dhidi ya chama hicho kinachojipambanua kwa vita dhidi ya ufisadi?

Kwa maana ufisadi hauishi hewani, ufisadi haukamatiki, ufisadi hauonekani, ufisadi haupo katika umbile kama la kiumbe hai. Bali ufisadi unatokana na matendo ya watu wasiokuwa na nia njema ambao miongoni mwa waliopo nchini, wanaaminika kuwa na ushirika na Millya!

Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Maingu Samson Mwigamba, anafananisha kujiunga kwa Millya katika Chadema na mtu aliyekuwa jambazi ama muuaji, kisha akabadili mtindo wa maisha yake.

Akaingia (mathalani) kanisani na kujiita mkristo mpya, moja kwa moja anakuwa ametakaswa dhambi zake.
Kauli hiyo aliyoitoa kupitia mchango wake kwenye mtandao wa kijamii wa Wanabidii, inatoa tafsiri ya uhalisia wa taswira hasi ya Millya kwa jamii. Ujambazi na uuaji si mfano mwema kwa mwanasiasa, hasa pale anapojiunga na chama makini akiwa na ‘joho la uuaji na ujambazi.’

Lakini kwa namna iwayo yote, Mwigamba ameshamkaribisha Millya katika Chadema, je, chama hicho kinakichunguza vipi na kujiwekea mazingira yasiyoruhu kugeuzwa kuwa ‘nyumba ya utaso’, kwamba watuhumiwa wa ufisadi na washirika wao wanaweza kuhifadhiwa humo?

Kwa maana kama nilivyoanisha awali, ufisadi hauonekani isipokuwa kama unafanywa na mtu ama watu.
Vita dhidi ya ufisadi kwa kadri ambavyo Chadema inashiriki, nafasi ya mtu mmoja mmoja anayetuhumiwa ama kuwa mshirika wa washirika wa vitendo hivyo viovu iko wapi?

Si nia yangu kumpingana na haki ya msingi wa Millya na dhamira binafsi ya kuhamia chama hicho ambacho mimi si mwanachama wake kama nisivyokuwa katika chama kingine chochote cha siasa.

Kusudio ni kuainisha kauli tofauti za pande mbili, CCM alipotoka Millya na Chadema anapojiunga mwanasiasa huyo.
Wakati Chadema ikiwatambua wahusika wa vitendo vya ufisadi na kushinikiza kuchukuliwa kwa ‘uamuzi mgumu’ dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi na washirika wao, tatizo la msingi lilikuwa chama (CCM) ama wahusika?

Kwa maana kama tatizo ni watuhumiwa wa ufisadi na washirika wao ndani ya CCM, lakini wanapoondoka ‘wanaokolewa’ kwa ‘kutakaswa’ huku wakionekana kuwa mashujaa, kuna maana gani?

Siwezi kumkaribisha Millya kwa maana sina mamlaka hayo, siwezi kumuwekea pingamizi kwa maana ametekeleza haki yake ya msingi, lakini mlinganisho wa ‘imani’ ya Chadema na ile ya CCM, chama hicho kimempata mpambanaji na tunu ya kisiasa?

Chadema imepata ‘kifaa’ kilichokuwa moja ya mihimili mikuu ya kisiasa kwenye kile kinachoaminika kuwa ngome ya kisiasa ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya ufisadi uliohusisha Tanesco na kampuni ya Richmond, Edward Ngoyai Lowassa?

Arusha inapotajwa kuwa ngome ya kisiasa ya Lowassa,  inakuwa ngome ya CCM kwa ujumla, hivyo uhalisia katika tukio hilo uko wapi?

Chadema imempata Millya akiwa tunu ya kisiasa ama kama wanavyosema viongozi wa CCM, chama hicho kikuu cha upinzani kimeambulia ‘gamba’ lililojisiitiri ili kupata uhai wa kisiasa?

Tusubiri!

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe; [email protected]

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles