



Sakata la Waislamu kugomea kushiriki sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika nchini kuanzia Agosti 26, mwaka huu, limechukua sura mpya baada ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), kutoa kauli inayotofautiana na baadhi ya viongozi wa dini hiyo wanaopinga zoezi hilo.
Badala yake, Bakwata limewataka Waislamu kushiriki kama kawaida kwani sensa ni jambo la kisheria na la kimaendeleo katika nchi na halihusishi dini wala ukabila.
Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Issa bin Simba, alitoa tamko hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya Bakwata jijini Dar es Salaam baada ya viongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu kutangaza kuandamana Agosti 26 kama serikali itakuwa haijaweka kipengele cha dini katika dodoso la sensa.
“Nachukua fursa hii kuwapa taarifa Wasilamu wote nchini na wananchi kwa ujumla kuhusu sensa inayotaka kufanyika nchini kwetu washiriki kwa ukamilifu kwani katika nchi yetu sensa zimefanyika nyingi miaka ya nyuma na hazikuhusishwa na dini wala ukabila, ni jambo la kisheria lililozoeleka na kukubalika,” alisema.
Hata hivyo, alisema kilichowakera Waislamu si sensa bali ni kutokana na hivi karibuni kuibuka kwa baadhi ya watu na kutoa takwimu kwamba Waislamu wapo kadhaa na Wakristo kadhaa wakati hawana dhamana ya kufanya hivyo kisheria.
Mufti Simba alisema takwimu hizo zimeleta mkanganyiko na hivyo kuna haja kwa serikali kutunga sheria itakayoainisha atakayekuwa na dhamana ya kutoa taarifa ya sensa badala ya hivi sasa ambapo watu wanajitokeza na kutoa takwimu zisizokuwa za kweli.
Alisema viongozi wa Waislamu washiriki sensa hiyo na wasisite kuihoji serikali iwafafanulie kama takwimu za sensa zilizotolewa kwenye mitandao ya kijamii inazitambua au la.
Hivi karibuni Katibu Taasisi za Jumuiya za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, alisema atahakikisha Waislamu hawashiriki zoezi la sensa ya watu na makazi iwapo Serikali haitarudisha kipengele cha dini katika maswali wanayoulizwa wananchi.