Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Hongera Pinda, sasa tunataka utekelezaji

27th June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwasilisha bungeni mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu juzi, alitangaza maamuzi magumu ya kuchukuliwa na serikali katika kukabiliana na  tatizo sugu la matumizi ya magari ya kifahari maarufu kama mashangingi kuanzia mwaka wa fedha wa 2012/13.

Pinda alisema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kupunguza matumizi yasiyo na tija, akiyaelezea kuwa ni ya gharama kubwa sana, hivyo kuanzia mwaka 2012/2013, hatua zaidi zitachukuliwa kwa kuweka ukomo wa ukubwa wa injini wa magari ambayo yanaweza kununuliwa na serikali kuu na taasisi zake pamoja na mamlaka za serikali za mitaa.

Pinda alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa chini ya utaratibu huo, magari yatakayonunuliwa yatakuwa ni yale yasiyozidi ukubwa wa injini wa CC 3,000 kwa viongozi na watendaji wakuu na yasiyozidi CC 2,000 kwa watumishi wengine ambao wana stahili ya kutumia magari ya serikali.

Katika kuhakikisha kuwa hatua hizo zinazaa matunda tarajiwa, Pinda aliliambia Bunge kuwa ili kupunguza matumizi ya magari kwa viongozi na watendaji wakuu kwa safari za mikoani, serikali itaanzisha vituo vya kanda vya magari ya serikali au kila ofisi itatenga magari machache yatakayotumika mikoani kwa shughuli za kikazi, aliahidi kuwa mwongozo wa utekelezaji wake utatolewa.

Kwa hatua hizo serikali inategemea kuwa utaratibu huo utapunguza matumizi ya fedha za umma kwa kiwango kikubwa, nia ikiwa ni kwanza kuitikia wito na vilio vya miaka na miaka kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ya taifa hili kuwa miongoni mwa maeneo ambayo matumizi yangeliweza kubanwa na wananchi wakanufaika na kodi zao, ni eneo la magari ya kifahari ambayo yamekuwa ni fasheni kwa watendaji wa umma kwa miaka mingi sasa.

Sisi tunafarijika kwamba pamoja na hatua hizi kuchukua muda mrefu kufikiwa na pengine kugharimu fedha nyingi za walipakodi ambazo zingeliweza kuelekezwa kwingine na kuleta matokeo chanya katika kupambana dhidi ya umasikini wa watu wetu, hatimaye serikali imetambua na inachukua hatua mwafaka katika kukabiliana na matumizi ambayo hayana tija kwa maendeleo ya taifa hili.

Tunapongeza tamko la serikali na kusudio hili la kuachana na ulevi wa magari ya kifahari, tunapongeza kwa kuwa siyo jambo la siri tena kwamba watumishi wa umma katika miaka ya hivi karibuni wamejivua utumishi na kujivalisha ukubwa na ubwana, kujitazama wao tu katika mambo mengi, ndiyo maana ukiitazama kwa darubini kali serikali kila mwaka haiachi kununua vitu kama samani na magari huku shida za wananchi zikiachwa kana kwamba hazionekana na haziihusu serikali.

Tunatambua kuwa Tanzania siyo nchi ya kwanza kuchukua hatua kama hizi za kubana matumizi katika mambo ambayo hayana tija; majirani zetu wawili yaani nchi za Rwanda na Kenya zilipata kuchukua hatua kama hizo, kwa maana hiyo inawezekana.

Kwa wenzetu hatua zao zilikuwa kali zaidi, wapo waliotangaza siku ya mwisho kwa serikali kutumia magari ya aina hiyo na waliokuwa wanayatumia wote walitakiwa kuyasalimisha, yalipigwa mnada na watumishi wa umma wakiwamo mawaziri walipewa magari madogo ambayo serikali ilisema wazi ilikuwa na uwezo wa kuyahudumia.

Hata hivyo, watumishi ambao waliojiona kwamba kwa hadhi zao hawawezi kutumia magari madogo, walitakiwa kujigharimia wenyewe kwa magari ambayo waliona yanakidhi mahitaji yao, lakini ilisisitizwa kamwe serikali isingelibeba mzigo wa kuyaendesha.

Kwetu hatua zilizotangazwa na Pinda ni kuachana na uagizaji wa magari hayo zaidi, kwa maneno mengine yalioyoko nchini na chini ya matumizi ya watumishi wa umma yataendelea kutumika, lakini hayatanunuliwa mengine muda wake wa matumizi ukifikia ukomo. Kitakachoendelea ni utaratibu huu mpya.

Tunafikiri hatua hizi siyo hapa, ni mwanzo mzuri kama kweli kutakuwa na utekelezaji wa dhati wa kuachana na magari haya ambayo hakika yamekuwa ni moto unoateketeza kodi za wananchi na kuifanya serikali mwaka baada ya mwaka kulia kuwa haina fedha za kugharimia miradi ya maendeleo kutokana na matumizi ya kawaida kuumuka kila mwaka wa fedha.

Ni matarajio yetu kwamba Pinda safari hii naye hatageuka tena kuwa malalamikaji kwa wale watumishi wa umma ambao hawatatekeleza kwa vitendo halisi maamuzi haya, ili sasa nasi turejeshe heshima na utiifu katika ofisi za umma kama ambavyo ilipata kuwa huko nyuma hasa wakati wa serikali ya awamu ya kwanza.




 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment