Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wanaowania tuzo Mwanamichezo Bora kutajwa leo

8th June 2012
Print
Comments
Mwanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2009 wa netiboli Mwanaid Hassan mwenye jezi nyeusi

Majina ya wanaowania tuzo ya Mwanamichezo Bora ya Mwaka inayoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) yatatajwa leo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Kamati ya Tuzo hizo, Amir Mhando, majina hayo yatawekwa hadharani leo katika kikao na wanahabari kitakachofanyika saa 5 asubuhi katika mgahawa wa City Sports Lounge jirani na Mnara wa Askari, Posta jijini Dar es Salaam.

"Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Wanamichezo Bora wa Tanzania Mwaka 2011, Masoud Sanan atazungumza na waandishi wa habari na kutangaza majina ya wanamichezo waliopitishwa kuwania tuzo hiyo itakayofanyika Juni 14 mwaka huu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Mshindi wa tuzo kuu katika tamasha la tuzo hizo ataondoka na zawadi ya dola za Marekani 8,000 (ambazo ni sawa na zaidi ya Sh. milioni 12), cheti na kombe.
Tuzo hizo ambazo zimedhaminiwa na bia ya Serengeti zitatoa pia zawadi ya Sh. milioni moja kwa kila mshindi wa michezo mbalimbali.

Mhando aliitaja michezo ambayo wanamichezo bora wake watazawadiwa kuwa ni riadha, wavu, netiboli, kuogelea, tenisi, judo, kikapu, soka, ngumi za kulipwa, ngumi za ridhaa, gofu (ridhaa), gofu (wa kulipwa), baiskeli na kriketi.

Michezo mingine ni mpira wa mikono, olimpiki maalum, Mchezaji Bora wa Nje anayecheza Tanzania, Mchezaji Bora wa Tanzania anayecheza Nje, Mchezaji Bora Chipukizi, Karate, Mwanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2011 na Tuzo ya Heshima.

Mwanamichezo Bora wa Tanzania 2006 alikuwa Samson Ramadhan aliyezawadiwa Sh. 500,000, wakati mwaka uliofuata mshindi Martine Sulle alizawadiwa Sh.500,000, huku mwaka 2008 mshindi Mary Naali alizawadiwa Sh.750,000. Wote hao ni wanariadha.

Mshindi wa mwaka 2009 alikuwa mchezaji wa netiboli Mwanaid Hassan aliyezawadiwa Sh. Milioni moja na mwaka 2010 pia alikuwa Mwanaid aliyezawadiwa gari aina ya Toyota Cresta GX 100 .

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment