Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mawaziri wapya wajaa hofu

8th May 2012
Print
Comments
Rais Jakaya Kikwete akimwapisha Shamsi Vuai Nahodha kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuliapisha Baraza la Mawaziri alilotangaza Ijumaa iliyopita. Kabla ya hapo Nahodha alikua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema uteuzi uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete kwake, ameupokea kama changamoto kubwa kutokana na historia kuonyesha kwamba mawaziri wengi waliopita katika wizara hiyo hawakutoka salama.

Balozi Kagasheki ambaye amehamishiwa katika wizara hiyo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi alikokuwa Naibu Waziri, alisema hayo katika mahojiano na waandishi wa habari katika viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam jana, katika hafla ya kuapishwa Mawaziri na Naibu Mawaziri.

“Mimi uteuzi wa Mheshimiwa Rais nimeupokea kama ni changamoto kubwa sana. Changamoto kwa maana ya kusema kwamba ukitizama historia ya wizara hii, mawaziri wengi ambao wamepita katika wizara hii hawakutoka salama. Sasa najiuliza kuna nini pale? Lazima kutakuwa kuna kitu,” alisema Balozi Kagasheki.

Tangu Rais Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, wizara hiyo imekwisha kuongozwa na mawaziri wanne, Anthony Diallo, Profesa Jumanne Maghembe, Shamsa Mwangunga na Ezekiel Maige, wakati makatibu wakuu ni Saleh Pamba, Blandina Nyoni na Balozi Dk. Ladslaus Komba na sasa Maimuna Tarishi.

Balozi Kagasheki alisema Watanzania pia wamekuwa wakisema kwamba katika wizara hiyo kumekuwa na vitendo vya ulaji wa kutisha na usiokuwa na aibu wa fedha za umma.

“Maana yake wizara hii nitasema Watanzania wote wanasema hii wizara watu mle wanakula vibaya, maana yake hata kunawa hawanawi, na wanakula kwa mikono yote miwili. Kwa hiyo, wanategemea kuona kwamba mambo yote yanawekwa katika order (sawa),” alisema Balozi Kagasheki.

Hata hivyo, alisema miongoni mwa mambo makubwa ambayo kwa kushirikiana na naibu wake pamoja na watendaji wengine wa wizara watakayoyasimamia na kutekeleza ni kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali zao.

Alisema watafanikisha hilo pamoja na mengine kwa kuwa anapo pa kuanzia licha ya kwenda katika wizara hiyo huku akikabiliwa na changamoto.

Balozi Kagasheki alisema tayari ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Kamati ndogo ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, imekwishaeleza kiini na matatizo katika wizara hiyo na imetoa mapendekezo ya mambo ya kufanya.

“Kwa hiyo, pa kuanzia tunapo, siyo kwamba tunaingia gizani. Tunapo pa kuanzia. Kwa hiyo, tunavyoenda tuanze kufanya kazi,” alisema Balozi Kagasheki.

Aliongeza: Watanzania mimi niseme kwamba unajua ni vigumu kusema kwamba nini watu watarajie. Lakini watutazame na najua watatutazama utendaji wetu wa kazi na vipi tunavyotetea zile rasilimali zinavyoweza kukafaidisha taifa, kwa sababu hii ni sekta moja ambayo ikiandaliwa na ikasimamiwa vizuri inaweza ikaendesha uchumi wa nchi hii.”

Alisema jambo lingine analokusudia kulirekebisha ni tabia iliyoota mizizi ya kupuuzwa bila kufanyiwa kazi maelezo ya ripoti za uchunguzi.

Kuhusu maeneo anayokusudia kuyashughulikia, alisema ni pamoja na malalamiko kuhusu vitalu vilivyogawiwa, wizi wa nyara za serikali, biashara haramu na utoroshaji wa wanyama hai nje ya nchi.

“Watu wanapiga matembo kule. Unasikia kwamba, kontena ya meno ya tembo imekamatwa Kongo, imekamatwa wapi. Yanakwenda mambo haya? Unakuta wanyama ndiyo hao kama unavyosikia, inakwenda. Kwa hiyo, vitu vipo na vitu ambavyo vinatia uchungu kwa Watanzania, lakini pia ni vitu ambavyo vinaweza vikasaidia katika kuongoza uchumi wa nchi yetu,” alisema Balozi Kagasheki.

PROFESA SOSPETER MUHONGO

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema Rais Kikwete hakukosea kumteua kwa kuwa anafaa sana kwa sababu ana uzoefu wa miaka mingi.

Alisema alimaliza digrii ya kwanza mwaka 1979 na kwamba, mpaka leo amebaki katika fani ya Jiolojia kitaifa na kimataifa, hivyo kazi anaimudu.

Kabla ya uteuzi wake, tayari wizara hiyo ilikwishaongozwa na mawaziri watatu tangu Rais Kikwete aingie madarakani mwaka 2005; akiwamo Dk. Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi na William Ngeleja. Wote waliondoka kwa kashfa.

Profesa Muhongo alisema mambo yaliyopo wizarani kwake hayana tofauti na sehemu nyingine zote duniani na kwamba, ili watu waendelee na uchumi wa nchi ukue, umeme ni kitu cha muhimu sana.

Alisema kwa kiwango cha uchumi wa nchi hivi sasa, Tanzania ilipaswa kuwa na umeme usiopungua megawati 1,500 na kwamba, iwapo nchi ingetaka kuwa na matunda mazuri ya Dira yake ya Maendeleo, inabidi iwe na umeme wa megawati zaidi ya 3,000.

Hivyo, alisema yeye pamoja na wenzake watakachokifanya na kusisitiza katika utendaji wao wa kazi, ni kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia umeme kwa vile kwa sasa wako chini ya asilimia 14 kati watu milioni 44.

Alisema kiwango hicho cha watumiaji wa umeme nchini ni cha chini, kwani ilipaswa tangu baada ya uhuru mwaka 1961 hadi sasa angalau Watanzania walio na umeme majumbani na sehemu zao za kazi wafikie angalau asilimia 75.

“Kwa hiyo, hilo nitaliwekea mkazo sana. Watu wanaotumia umeme waongezeke, namna ya kuupata huo umeme, gharama ziwe za chini, halafu na umeme wenyewe uwe wa kutegemewa na kukadiriwa. Siyo leo unakuja kesho hauji.”

Kuhusu Watanzania wategemee kwa muda gani kupata mambo hayo, alisema yeye siku zote huwa hatoi majibu ya kisiasa, kwani watu wote wanaotengeneza mipango ya umeme wanayo ya muda mfupi na mrefu.

Hata hivyo, alisema mipango ya muda mfupi kwa sasa kutokana na hali ilivyo, inabidi wazalishe umeme kwa haraka sana usiopungua megawati 500 na kwamba, ili kufikia kiwango hicho, lazima wawe na mchanganyiko wa umeme.

Alisema mchanganyiko wa umeme ambao anakwenda kushauriana na wenzake wizarani, ni wa kutumia vyanzo vikuu vitatu; cha kwanza kikiwa ni matumizi ya makaa ya mawe, cha pili gesi, na cha tatu ni umeme wa maji unaotumika kwa sasa.

“Lakini dunia ya leo hii, duniani kote hata makampuni makubwa ya kimataifa yanayoshughulikia nishati kama BP Shell wameingia kwenye nishati mbadala. Na hapo lazima Watanzania na sisi twende. Na hizo nishati mbadala, kwanza ni wa jua, pili wa upepo, tatu wa majimoto. Hiyo ndiyo ambayo ni ya uhakika kabisa,” alisema Profesa Muhongo.

“Kwa hiyo tukichanganya vyote hivyo tunaweza tukapata umeme wa uhakika zaidi kuliko ule wa kutegemea mvua na maji. Hayo ni mambo ya zamani, ya kutegemea maji, yamepitwa na wakati kabisa.”

Kuhusu wachimbaji wadogo wa madini Tanzania, alisema toka miaka ya 1990 amekuwa akifanya kazi na watu hao, hivyo si mgeni, kwani amewahi pia kuishauri serikali kwa njia nyingi sana kuhusu watu hao.

Kutokana na hilo, alisema matatizo ya wachimbaji wadogo yanajulikana, msaada wa kwanza wanaouhitaji ni utaalamu wa madini, vitendea kazi, fedha (mtaji) na masoko ya kuuza mazao ya uchimbaji.

“Kwa hiyo, hivi vyote tunaenda kuvitekeleza kwa vitendo,” alisema Profesa Muhongo.

Kuhusu madini kwenda nje ya nchi huku Watanzania wakiachwa wakiambulia mashimo matupu, alisema anadhani Watanzania sasa watafaidika na madini kwa sababu watakuwa na njia nyingi za kufaidika.

Alisema kwa mfano, wachimbaji wakubwa, inabidi serikali ianze kuangalia mikataba yao na sera za nchi ili kuona Tanzania inafaidika kiasi gani na hasa madini hayo yasaidie wachimbaji wadogo na watu wanaoishi sehemu yanakopatikana.

WAZIRI DK. MWAKYEMBE

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema uteuzi wake anauchukulia kuwa ni jambo la kawaida katika mgawanyo wa kazi kwa watumishi wa umma ambapo alisema wakati wowote mabadiliko lazima yatokee, hivyo mhusika hana budi kuwajibika.

Kabla ya uteuzi wake, wizara hiyo ilikuwa ikiongozwa na Omar Nundu ambaye ameachwa katika baraza jipya la mawaziri la sasa.

Alisema licha ya wizara aliyoteuliwa kuiongoza kuwa na matatizo mengi, lakini kwa sasa yeye si muarobaini wa kuponya matatizo hayo kwa kufumba na kufumbua.

“Wizara ya Uchukuzi kwa kweli ina matatizo mengi sana. Na mimi siwezi leo nikawa muarobaini wa hayo matatizo sasa hivi. Niacheni nipate muda na naibu wangu tuangalie ukubwa wa hayo matatizo na kwa muda si mrefu mtasikia tumechukua hatua,” alisema Dk. Mwakyembe.

Aliongeza: “Watanzania tunawahakikishia kwamba tumekuja watu ambao tutahakikisha kwamba ile wizara inakuwa wizara. Na kama haiwi wizara hakuna haja ya sisi kuteuliwa kukaa pale. Mtanisikia nikitangaza nikisema najitoa.”

Alisema anasema hivyo, kwa vile anaamini kuwa yeye na naibu wake, Dk. Charles Tizeba, wameteuliwa kwenda kuihangaikia wizara hiyo na kwamba, kama wizara hiyo ina changamoto nyingi, basi kazi yao ni kuzishughulikia.

Dk. Mwakyembe, alisema ana uhakika watafanya hivyo iwapo tu watapewa muda wa kujua ukubwa wa tatizo, kiini chake, kuelewa wafanye nini na kupanga mikakati ya kujikwamua, bila kukimbikizwa kama wao ni muarobaini.

Alisema watakuwa na sera ya uwazi wizarani kwao kwa wananchi kupitia vyombo vya habari katika kila hatua watakayopiga ya utekelezaji wa majukumu yao.

Dk. Mwakyembe alisema hakuna kisichokuwa muhimu miongoni mwa sekta zinazopaswa kushughulikiwa na wizara hiyo. “Vyote ni vipaumbele, reli ni kipaumbele, bandari ni kipaumbele. Unajua hapa hakuna ambacho ni muhimu zaidi kuliko kingine,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema leo hii asilimia zaidi ya 90 ya mizigo ya Tanzania inasafirishwa kwa kutumia malori, jambo ambalo alisema limekuwa likiharibu barabara kila siku.

“Hilo katika uchumi wowote ambao ni health (wenye afya) haliwezekani. Lazima reli ndio ichukue mzigo mkubwa,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema pia asilimia 80 ya wasafiri nchini ni wale wanaotumia barabara na kusema hicho ni kipaumbele kingine ambacho kinapaswa kushughulikiwa.

Dk. Mwakyembe, alisema pia kwa upande wa bandari, kuna nchi ambazo bidhaa zote za nje lazima zipitie hapo na kwamba, Tanzania ni nchi ambayo Mungu ameipa bahati kwa kuzungukwa na nchi zisizokuwa na maziwa na kuhoji kwanini bandari yake isiwe pia kitegauchumi cha maana?

Alisema pia leo Tanzania inaelezwa ina shirika ambalo halina ndege na kusema kitu hicho ni changamoto na si cha kufurahia.

Mawaziri walioapishwa jana, ni Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa-JKT), Dk. Hussein Mwinyi (Afya na Ustawi wa Jamii), Profesa Jumanne Maghembe (Maji), Hawa Ghasia (Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi), Mathias Chikawe (Katiba na Sheria), George Mkuchika (Ofisi ya Rais-Utawala Bora) na Celina Kombani (Ofisi ya Rais-Utumishi).

Wengine ni Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Mhandisi Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika), Balozi Kagasheki, Dk. Mwakyembe, Fenella Mukangara (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Dk. Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Dk. William Mgimwa (Fedha) na Profesa Muhongo.

Naibu Mawaziri walioapishwa ni Adam Malima (Kilimo, Chakula na Ushirika), Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii), Gregory Theu (Viwanda na Biashara), Pereira Ame Silima (Mambo ya Ndani ya Nchi), Charles Kitwanga (Ofisi ya Makamu wa Rais), Jerryson Lwenge (Ujenzi), Seif Suleiman Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk. Binilith Mahenge (Maji), George Simbachawene (Nishati), Stephen Masele (Madini), January Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Charles Tizeba (Uchukuzi), Amos Makalla (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Angella Kairuki (Katiba na Sheria), Janet Mbene (Fedha) na Saada Mkuya Salum (Fedha).

CHADEMA: WALIOTIMULIWA WAFIKISHE KORTINI

Wabunge watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, wametishia kuwashawishi tena wabunge wa vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni, kutokubali kupitisha bajeti ya serikali katika mkutano ujao wa Bunge, ikiwa mawaziri walioachwa katika baraza jipya, hawataburuzwa mahakamani.

Wabunge hao, David Silinde (Mbozi Magharibi), Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr. Sugu (Mbeya Mjini), walisema hayo wakati wakihutubia maelfu ya wakazi wa wilaya mpya ya Wanging’ombe na Wilaya ya Njombe katika operesheni maalumu ya Twanga kote kote iliyofanyika katika viwanja vya Polisi Makambako.

 “Kama walifikiri kubadili mawaziri ni suluhisho pasipo kuwaburuza mahakamani mawaziri wanane, tunaowatuhumu kwa ufisadi, tunawataarifu kwamba tutashawishi wabunge wa vyama vyenye uwakilishi bungeni kuzigomea baadhi ya bajeti za serikali katika Bunge lijalo,” alisema Sugu na kuongeza:

“Kuwaweka mawaziri hao pembeni hakutoshi, tutakomaa nao hadi kieleweke kwa kuwa tatizo halijakwisha na kama wanadhani tulichokifanya kilikuwa ni upepo kama wanavyodai, basi wajue inakuja dhoruba, tunataka kuwaona wanasimama kizimbani.”

 Mawaziri wanaotuhumiwa na wabunge hao ni pamoja na waliokuwa: Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, Waziri wa Uchukuzi Omari Nundu; Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Athumani Mfutakamba; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya. 

ASKOFU NZIGILWA AWASHAURI

Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusedius Nzigilwa, amesema anaamini kuwa mawaziri walioapishwa hawatabweteka kwa kuwa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yametokana na changamoto za kiutendaji serikalini.

Askofu Nzigilwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kuwa anaamini kuwa mawaziri wapya na serikali kwa ujumla itafanyakazi kwa ufanisi zaidi hasa kushughulikia changamoto iliyopelekea kubadilisha baraza.

“Mabadiliko haya yamekuja na changamoto kidogo na hata walioingia wanajua nini kilichosababisha wengine kuondoka, ninaamini kuwa watafanyia kazi makandokando yaliyosababisha mabadiliko. Naamini watafanyakazi vizuri,” alisema.

Imeandikwa na Muhibu Said, Restuta James, Dar na Godfrey Mushi, Iringa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment