


Wakati wananchi wengi wakiibeza bajeti ya serikali iliyotangazwa Alhamisi iliyopita, Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), wameipongeza serikali kwa kuongeza kima cha kukatwa kodi ya mshahara mfanyakazi tutoka Shilingi 135,000 hadi 170,000.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa CTI, Felix Mosha, alisema kiwango hicho cha kukatwa kodi kitasaidia kuwalinda watumishi wanaolipwa Shilingi 135,000.
“Kuna baadhi ya mambo bajeti hiyo imetenda haki, lakini kuna sehemu nyingine imewabana wananchi na wenye viwanda vile vile,” alisema Mosha.
Aidha, Mosha alisema CTI wanaipongeza bajeti hiyo kwa kuweza kutenga kiasi kwa ajili ya kuimarisha usafiri wa reli ya Kati na ile ya Tazara, ambazo zitawanufaisha wenye viwanda kusafirisha bidhaa wanazozalisha kwa umakini.
Alisema baejti hiyo pamoja na kuonekana ‘mzigo’ kwa wananchi, lakini katika sekta viwanda ‘inafurahisha’ na ‘kukeresha’.
Hata hivyo, Mosha alisema CTI inashauri bajeti hiyo lazima iimarishe usafiri wa reli, barabara na bandari ili kuweza kurahisisha huduma za usafirishaji wa bidhaa za viwandani kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi.