Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Fedheha ya kughushi vyeti ni ishara gani?

27th May 2012
Print
Comments

Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia baadhi ya wasomi waliobobea wakituhumiwa kwa kashfa za kughushi vyeti vya taaluma mbalimbali, walikuwepo baadhi ya viongozi wa serikali na wabunge ambao kwa pamoja walituhumiwa kuwa na vyeti vya shahada kutoka vyuo vikuu visivyojulikana au visivyosajiliwa rasmi. Suala hilo liliwahi kumfikia aliyekuwa Spika wa Bunge Samwel Sitta, naye akalirejesha serikalini kwa hatua zilizostahili.

Hata kabla hilo halijasahaulika akilini mwa wengi wanaofuatilia, juzi likaibuka jingine ambalo hilo sasa limevuka mipaka, limehusu waajiriwa wa vyobo vya Ulinza na Usalama hasa majeshi ya Polisi pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) hivi karibuni iligundulika na kudai kuwa Jeshi la Wananchi lilikuwa limeajiri vijana 248 na Jeshi la Polisi likiwa limeajiri vijana 700 ambao kwa pamoja iligundua kuwa majina yao katika vyeti vyao vya shule yalifanana na watumishi wengine serikalini.

Hali ya tuhuma hiyo kwa majeshi hayo ilianza kutoa sura ya utata hasa baada ya Mkurugenzi wa NIDA, Dikson Maimu alipoamua tena kutoa kauli ya kusahihisha tuhuma hiyo kupitia vyombo vya habari. Hata hivyo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema mwishoni mwa wiki kuwa jeshi hilo limeanza kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma ya kuwa wanajeshi wake walijiunga na jeshi kwa kutumia vyeti vya watu wengine kwa makusudi ya kujipatia ajira.

Nia yangu si kurejea mambo ambayo majeshi hayo yatawafanyia waajiriwa hao, nataka kutoa angalizo la namna jamii sasa inavyohangaika kutafuta ajira kwa gharama yoyote hata ikiwa ni kwa kughushi taaluma kupitia vyeti batili!

Hilo ni tatizo kubwa na la hatari, na kama hatua madhubuti hazitachukuliwa dhidi ya waajiriwa hawa wanaopata nafasi kwa kutumia vyeti na nyaraka nyingine zisizowahusu, taifa litaingia katika janga ambalo litaathiri amani, maendeleo na ustawi wa taifa.

Wakati taifa linafanya warsha pamoja na makongamano ya kimataifa kwa gharama kubwa kwa ajili ya kujikwamua katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, juhudi za aina hiyo zinaingia dosari kubwa inapodhihirika kuwa wakati huo huo wengine wanatumia sayansi pamoja na teknolojia kughushi vyeti kwa ajili ya kujipatia ajira, hali hii inaweza kuzaa matatizo makubwa mawili au zaidi.

Moja ni kutoa ajira kwa asiyestahili kielimu, na matokeo yake ufanisi wake unakuwa chini ya kiwango kilichotegemewa, na pili ni kudhoofisha azma ya kufikia lengo la kujitegemea kitaaluma, na matokeo yake ni kurudisha nyuma maendeleo ya taifa kisayansi na kiteknolojia.

Mfano, mwanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania akipata ajira kwa cheti cha kumaliza kidato cha sita cha kughushi, na hatimaye Jeshi likampa nafasi ya kusomea utaalamu unaofanana na masomo yaliyojionyesha katika cheti hicho, akasomee utaalamu wa mizinga, huyu askari lazima atakumbana na mahesabu pamoja na masomo ya Jiografia yanayolingana na kiwango cha elimu iliyojidhihirisha katika cheti batili.

Matokeo yake ni askari huyo kutomudu masomo hayo au kama akibahatika kufuzu, anaweza kuangamiza askari wake na madhara mengine wakati wa operesheni zao za kijeshi, atakuja kukosea mahesabu na mabomu ya mizinga yakavurumishwa maeneo tofauti.

Ajira kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania inapotangazwa, huwavutia vijana wengi sana, miaka ya nyuma ajira hiyo haikuhitaji sifa za elimu kubwa, ingawa sasa elimu ya darasa la saba siyo sifa tena ya kujiunga na Jeshi hilo. Hata hivyo huwepo mtafaruku wa kuwania nafasi hizo, mojawapo ni katika kutafuta vyeti vya bandia ili kukidhi mahitajio ya kupata ajira.

Kwa namna vijana wanavyokimbilia ajira ya Jeshi hilo, baadhi yao huthubutu kukatisha masomo ili wawahi ajira kwa kutumia vyeti halisi vya elimu ya nyuma.

Tafsiri ya kuwepo kwa maisha magumu nchini ni pamoja na kuwepo uhaba wa ajira serikalini. Nafasi nyingi za ajira hutokea ndani ya majeshi yetu, Jeshi la wananchi wa Tanzania, Polisi, Magereza, Mali Asili, Usalama wa Taifa, Uhamiaji nk.

Vijana pia wanaangalia wapi maslahi yanalipa zaidi, na pia wanaangalia na sifa za vyeti vinavyohitajika katika kila sekta hizo. Ushawishi wa kuingia katika vyeti vya kughushi unatokana na uchaguzi wa wahusika wa aina ya ajira wazitakazo.

Nimeshuhudia ajira kwa vyeti halali kwa vijana wasomi katika sekta binafsi, katika kampuni, taasisi za fedha kama mabenki nk. Akiwa katika ajira, utamkuta akihangaika kila siku kupeleka maombi ya kazi katika sehemu anayoona ina maslahi zaidi, na mara nyingi siyo kwa maslahi halali, bali ni eneo analoona lina mipenyo ya kujineemesha kwa haraka.

Vijana wasomi wanapotafuta ajira wanakuwa na malengo ya kuwa na maisha bora kwa muda mfupi, gari, nyumba nk. Hayo ndiyo ya ushindani wa maendeleo kwa vijana. Ni kwa mbinu gani vijana wa aina hiyo watafanikisha dhamira hizo kama si kwa mbinu za ubadhirifu na ufisadi wa nafasi walizoajiriwa nazo?

Hilo nalo ni tatizo, ufisadi sasa umeenea nchini kama kansa, kuanzia kwa wakubwa hadi hawa sasa! Tiba yake ni ngumu, lazima hatua za kuwaelimisha vijana zichukuliwe mapema kabla kansa hii haijatumaliza.

Maoni: 0715-047304 na 0762-233116

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment