Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Malinzi kugharimia uchaguzi mkuu riadha

27th April 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi

Kufuatia kusuasua kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT) kutokana na ukosefu wa fedha, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi, amesema atatoa fedha mfukoni mwake kugharimia kila kinachohitajika ili kufanikisha uchaguzi huo.

Awali, uchaguzi huo ambao ulipangwa kufanyika April 29 mkoani Ruvuma, ulihitaji Sh. milioni 27 kwa kushirikisha baadhi ya mikoa, lakini ukosefu wa fedha ukawalazimu viongozi wa sasa wa RT kuusogeza mbele hadi Mei 20 na kuamua kuwa sasa ufanyike mkoani Morogoro.

Mbali na kuamua kugharimia uchaguzi huo, Malinzi pia amewaondolea gharama za uchukuaji fomu za wanaowania uongozi. Awali zilikuwa zikitolewa kwa kulipiwa Sh. 20,000 na kila mgombea.

Katika hatua nyingine, mikoa yote ambayo ni wanachama hai na ile isiyokuwa mwanachama imeruhusiwa kushiriki katika uchaguzi huo na kutakiwa kuwasilisha wajumbe watatu walioteuliwa na kamati ya michezo ya mkoa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa RT, Henry Tandau, alisema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa juzi baada ya kikao cha serikali na shirikisho hilo, kilichoongozwa na viongozi wa juu wa BMT, pamoja na Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo nchini, Leonard Thadeo.

Tandau alisema wamefikia maamuzi hayo baada ya kukubaliana kuwa RT ni chama cha taifa na kwamba viongozi wake wanatakiwa kuchaguliwa na wajumbe kutoka mikoa yote nchini.

Alisema baada ya kikao hicho, ilionekana kwamba RT walikuwa wakiahirisha uchaguzi huo mara kwa mara kutokana na ukata mkubwa wa fedha unaowakabili, pamoja na baadhi ya mikoa kutokuwa na katiba inayoendana na ile ya RT.

"Hizo ndizo sababu kubwa zilizopelekea uchaguzi huo uahirishwe kila mara," alisema Tandau.

Alisema baada ya kubaini hali hiyo, Mwenyekiti wa BMT, pamoja na kamati ya kikao hicho, walitoa maamuzi ya kugharimia uchaguzi na baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, iteuliwe kamati ya kuunda katiba mpya ya RT ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Alisema kwamba mbali na uamuzi huo, ilikubaliwa vilevile kwamba hakutakuwa na pingamizi wala mgombea kukata rufaa baada ya kukamilika kwa usaili wa wagombea uliopangwa kufanyika Mei 18 mkoani Morogoro.

Tandau aliongeza kuwa baada ya maamuzi hayo, siku ya mwisho ya uchukuaji fomu za wagombea imesogezwa hadi Mei 15, usaili utafanyika Mei 18 na majina yatakayopitishwa yatajulikana Mei 19 kabla ya uchaguzi kufanyika katika siku inayofuata.

Viongozi waliopo sasa RT wamedumu madarakani kwa miaka zaidi ya sita sasa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles