Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Ya Abdoulaye Wade wa Senegal na tarajio langu Arumeru Mashariki

28th March 2012
Print
Comments

MstariI wa kalamu umepigwa juu ya jina la aliyekuwa Rais wa Senegal, Abdoulaye Wage (85) wa chama cha Senegalese Democratic (PDS), hivyo kufunga ukurasa wa utawala wake baada ya kuingia madarakani mwaka 2000.

 

Wade amebwagwa na mshindani wake anayekuwa Rais mpya wa nchi hiyo, Macky Sall (50), akitokea chama cha upinzani cha Alliance for the Republic aliyepata asilimia 60 ya kura, huku Wade akiambulia asilimia 30 ya kura za uchaguzi wa marudio.

 

Shirika la Habari la Serikali ya Senegal (APS) limetangaza kuwa Wade ameshampigia simu Sall, akielezea kuridhika kwake na matokeo yanayomfanya aondoke kwenye Ikulu ya nchi hiyo pasipo shuruti wala umwagaji damu.

 

Ushindi wa Sall na mabadiliko ya utawala wa Senegal yanayofanyika kwa njia ya kidemokrasia huku amani na utulivu wa kweli vikitarajiwa, si mara ya kwanza kujitokeza barani Afrika.

Mathalani  katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana nchini Zambia, Michael Satta kutoka chama cha upinzani cha Patriotic Front (PF) alimshinda rais aliyekuwa madarakani, Rupiah Banda wa  Movement for Multi-Party Democracy (MMD).

Lakini tukirejea katika uchaguzi wa Senegal, matokeo yake ya maana pana katika utekelezaji wa misingi ya demokrasia, ikiwemo uhuru wa watu kuwachagua viongozi wanaowataka, na uamuzi huo kutangazwa kwa kadri ya mahitaji ya umma.

Akiwa Rais aliyeonyesha ‘uchu wa madarakani’ baada ya kubadili Katiba ya Senegal ili kumruhusu agombee tena urais katika Uchaguzi Mkuu uliomwangusha, raia wa taifa hilo lililo Magharibi mwa Afrika walipaza sauti, wakamwambia ‘imetosha’.

Hivyo Wade katika hilo akajionyesha katika sura mbili, moja ikiwa ni kielelezo cha viongozi wang’ang’anizi wa madaraka ikibidi kwa kubadili Katiba ya nchi kwa maslahi binafsi, lakini pili, kwa kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo, pamoja na tishio la kuibuka machafuko ikiwa ‘angeyachachua.’

Inawezekana Wade alishinda mtihani wa awali wa kubadili Katiba kutokana na hulka ya ‘wanaokubali waseme ndioooooo…ndiooooooooooooooo’, wasioafiki waseme sioooooo….sioo. Waliokubali wameshinda.”

Lakini alipoingia katika mtihani wa pili ulioushirikisha umma, nguvu ya umma ikatumika kufikia uamuzi kwa njia ya kura, matakwa ya Wade hayakufikiwa. Akazisoma nyakati na kuamua kuyakubali matokeo.

Mchakato wa uchaguzi katika nchi kadhaa za kiafrika zikiwemo zilizowahi kukumbwa na hatari ya machafuko, unatoa nafasi ya ukweli unaothibitisha kwamba, uamuzi wa raia unapoheshimika nyakati za chaguzi, amani na utulivu wa kweli unakuwepo.

Wade alikuwa na uwezo wa kiyaamuru majeshi ya ulinzi na usalama yauvuruge uchaguzi wa Senegal, alikuwa na uwezo wa kushirikisha hata Usalama wa Taifa wa nchi hiyo uchakachue matokeo ili abaki madarakani, angewashurutisha wasimamizi wa uchaguzi wafanye anavyoona inafaa, kwa maslahi binafasi ama ya chama chake.

Wakati upepo wa mabadiliko ukitokea katika nchi kama Senegal, ni dhahiri kwamba salaam kubwa inayopaswa kutangazwa kupitia vyombo vya habari ama baragumu za vijijini, ni kwamba vyama vya upinzani si adui wa mataifa ya Afrika.

Vyama vya upinzani vinaundwa na wanasiasa walio raia halali wa mataifa husika na ambao anapoingia madarakani, wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba.

Hapo ndipo msingi wa kuwa na Katiba ya kitaifa, ile isiyotengenezwa kwa kuangalia ama kujali maslahi ya kikundi cha watu wachache, hata wakiwa milioni kadhaa ndani ya chama cha siasa kilichopo madarakani.

Nchi inapokuwa na Katiba ya kitaifa yenye kujali maslahi ya Taifa, hakuna nafasi ya Rais atakayeshinda, kufanya ‘uchuro’ wake Ikulu, pale ambapo Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipafananisha na ‘mahali patakatifu.’

Aliyekuwa Rais wa Senegal, Abdoulaye Wade, anaondoka madarakani kwa amani, anaiachia Afrika salaam moja, kwamba wananchi wakiamua, wameamua.

Wakati Wade akiondoka madarakani, Tanzania inaelekea katika uchaguzi mdogo wa ubunge, jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha.

Arumeru Mashariki inashirikisha nafasi ndogo ya uwakilishi wa wananchi ikilinganishwa na Senegal, lakini jambo moja lililo sawa katika mizani ya demokrasia, amani na utulivu, ni kuepuka ‘uchakachuaji’ unaweza kuligeuza jimbo hilo kuwa eneo lisilo rafiki wa amani.

Vyama vya siasa vimeshiriki kampeni za uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki na sasa vipo vipo katika ngwe ya salala salama. Wapo ‘magwiji’ wa kuchakachua matokeo ya uchaguzi, wapo walio hodari wa kuvishurutisha vyombo vya ulinzi na usalama.

Wapo wanaoweza kutumia rasilimali zikiwemo za umma ili kuvuruga uchaguzi na matokeo ya Arumeru Mashariki, wapo wanaoweza kushinikiza rangi iliyo nyekundu mithili ya damu ionekane nyeupe kama theluji.

Wade angeweza kuyafanya hayo, yakatokea na akatangazwa kuwa mshindi. Lakini ushindi wake usingeiweka Senegal mahali ilipo.

Senegal ilikuwa salama, yenye amani na utulivu kabla na baada ya uchaguzi uliomwangusha Rais Wade. Kwa kuheshimu matakwa ya umma, imebaki jinsi ilivyo.

Vivyo hivyo, Arumeru Mashariki ipo katika hali ya salama, amani na utulivu, wadau na mamlaka husika hawapaswi kuifanya tofauti baada ya uchaguzi mdogo na hilo litafanikiwa ikiwa ‘uchachuaji’ utaepukwa na uamuzi wa wapiga kutangazwa kama ilivyo.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540 ama barua pepe: [email protected].

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles