


Mjadala wa kufurahisha ulizuka katika moja ya mihadhara midogo ndani ya warsha ya mwaka ya kitafiti ya REPOA, asasi ya utafiti uchumi kuhusiana na kupunguza umaskini uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Ulihusu 'wajibu kijamii wa makampuni makubwa.' Suala hilo liliibuliwa katika mada ya mhadhiri wa masuala ya biashara na mwandishi wa safu kadhaa kufundisha masuala hayo, Dk. Honest Prosper Ngowi wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Akasema katika mada yake kuwa makampuni makubwa yanafanya suala la wajibu wao kwa jamii zinazozunguka maeneo wanakofanya kazi (hasa migodi ya dhahabu) kuwa la hiari tu, la kujisikia, kwa hiyo wanatoa 'vijisenti' na hawawajibiki kwa njia inayofaa.
Chanzo kimojawapo muhimu cha kuzuka kwa suala hilo ni mwelekeo wa mjadala mpana zaidi wa nafasi ya uwekezaji katika kuleta mabadiliko ya jamii, na moja ya majawabu ni wazo la Dk. Ngowi, kuwa makampuni makubwa yakiwajibika, mabadiliko yanakuwa na uhakika zaidi.
Ni wazo ambalo baadhi ya washiriki wa mhadhara mdogo (kandokando ya hadhara kubwa za pamoja kwa siku mbili za warsha) walilifurahia, kuwa makampuni makubwa yawajibike ipasavyo kwa jamii zinazowazunguka, na siyo wakijisikia watoe 'vijisenti.'
Tatizo likaja kwenye mapana yake ya kisheria kwa upande mmoja, yaani aina ya mkataba unaofikiwa na wawekezaji katika migodi halafu pia suala la utamaduni, kuomba.
Tatizo la kwanza la kisheria ni kuwa kampuni ya uwekezaji ina mkataba na serikali ambao msingi wake ni kodi itakazolipa, na hiyo si kampuni ya shughuli ndogondogo ambayo itakuwa chini ya Halmashauri ya Wilaya kama vile ni duka au meza sokoni.
Ikishalipa kodi hizo kimsingi imetimiza wajibu wake, na ndiyo maana kunatokea suala la 'wajibu wa kijamii' wa makampuni, kuwa yasingependa kupuuzia kuwa wako wakazi wa maeneo ambayo wanaendesha kwa mfano mgodi wa dhababu, kwani kupuuzia uwepo wa watu katika eneo hilo una madhara yake.
Hata hivyo haina maana kuwa kampuni ya uwekezaji ikiwa inajali na kutoa michango halmashauri basi tatizo hilo litaisha, kwani inategemea pia matazamio yao.
Ndiyo hapo linakuja tatizo la kujua kama shughuli hizi za kijamii ambazo makampuni haya yanagusa zisimamiwe na kuratibiwa kama eneo rasmi la uwajibikaji au la wajibu, au libaki kama lilivyo kuwa ni suala la hiari? Hapo mwendesha mhadhara mdogo na katibu mkuu wa siku nyingi, pia mtawala wa zamani wa shirika la ufilisi na dhamana la LART, Dk. Jonas Kipokola akatofautiana na Dk. Ngowi katika majumuisho yake ya mjadala.
Akasema kwa taratibu za kiafrika ni aibu kwa mwenyeji kuomba fadhila kwa mgeni, kufunua aibu ya nyumbani kwa mgeni kwa kutaka nyumba hiyo 'ihemee kwake,' ipone kutokana na ujio wake, akasisitiza umuhimu wa kuliacha suala hilo liwe tu la hiari, au ushirika.
Aliainisha kuwa ingekuwa rahisi zaidi kama kungetokea michango ambako kampuni inaweza kutoa nusu na halmashauri nusu, kuliko mazingira ambako halmashauri haina mchango wowote katika mradi fulani, inaorodhesha mahitaji inampelekea mwekezaji.
Isitoshe, kama mada ya Dk. Ngowi ilivyoainisha anataka pia asimamie mgeni atatoa kiasi gani na kwa kawaida asingependa kuulizwa kwa karibu jinsi anavyotumia.
Suala hilo halikujadiliwa kwa undani lakini limejitokeza katika wilaya tofauti za migodi, kwa mfano wilayani Tarime ambako mabadiliko ya ubunge yalihusiana na mizozo kuhusu matumizi.
Mchumi mwandamizi katika ofisi ya Benki ya Dunia nchini, Dk. Josephat Kweka alitoa mapana zaidi ya suala hilo (ambayo pia yalilenga kujibu mantiki ya ndani ya hoja ya Dk. Ngowi) akisema kuwa suala la kuangalia 'nafasi ya uwekezaji katika mabadiliko ya jamii' lina utata.
Akaainisha kuwa uwekezaji ni moja ya vichangiaji katika mchakato mzima wa mabadiliko, na siyo msingi wake, hivyo kuzua hisia kuwa kama makampuni yakiwajibika katika maeneo wanayofanyia kazi, basi maeneo hayo yatafaulu 'kupiga vita umaskini.'
Akaainisha kuwa mabadiliko yanatokana na kile wananchi wanachofanya, tija halisi ya shughuli zao, na siyo uhusiano wao na mwekezaji (kwa maana hiyo ni shughuli tu nyingine).
Mchangiaji mwingine aliainisha kuwa suala la uwajibikaji linaendana na dhana ya jumla ya kudhania kuwa watu kutoka nje wanatupenda sana,yaani wasiweke kipaumbele katika kuendesha shughuli zao kwa nia ya kupata faida, na badala yake shughuli hiyo iwe kama 'kambi' ya shughuli pana zaidi ya kupambana na umaskini.
Ilikuwa ni suala la mantiki la kutenganisha shughuli hizo mbili, ambalo baadhi ya washiriki (hata bila kuchangia moja kwa moja) walihisi kuna aina ya udanganyifu au tuhuma zisizo na msingi kuwa 'kuna mgodi, mbona bado kuna umaskini,' kuwa haviingiliani. Kwa vile hayo makampuni ya migodi yako maeneo ya vijijini ambako hakuna kampuni nyingine kubwa, uoanishaji huo unatokea.
Mijini hali ni tofauti; huwezi kusema Shoprite iko hapo, kwanini Mlalakuwa ni maskini! Hilo 'duka' (supermarket) la Shoprite likishalipa kodi kupitia ankara zinazoonekana, halina wajibu tena.