


.jpg)
Joto kubwa limeibuka kufuatia ufafanuzi ambao umetolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Hifadhi ya Jamii (SSRA) juu ya marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na Sheria ya SSRA ambazo zimefanyiwa marekebisho na kupitishwa na Bunge Aprili 13 mwaka huu. Sheria hiyo tayari imekwisha kusainiwa na Rais na hivyo kuanza kutumika rasmi.
Taarifa ya SSRA iliyotolewa mwishoni mwa wiki na kuleta taharuki kubwa inasema kuwa katika marekebisho hayo yanayowahusu wafanyakazi wote nchini bila kubagua sekta yoyote, fao la kujitoa (withdrawal benefits) yamefutwa na kuanzia sasa hayatakuwepo.
Mafao hayo yalikuwa yanatolewa pale mwanachama alipokuwa anaacha kazi. Kwa mabadiliko hayo, wanachama wa mfuko wowote wa hifadhi ya jamii sasa atapata mafao yake pale tu atakopfikisha umri wa kustaafu kwa hiari wa miaka 55 au kwa lazima wa miaka 60 au pale anapopata ulemavu wa kudumu.
Taarifa hiyo pia ilifafanua kuwa kwa kuzuia fao la kujitoa mwanachama anapata fursa ya kupata mikopo ya nyumba kwa kutumia dhamana ya michango yake kama ilivyoelezwa kwenye Sheria ya SSRA kipengele cha 38.
SSRA ilikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa marekebisho ya kuzuia mafao ya kujitoa yamefanyika ili kutimiza lengo na madhumuni ya hifadhi ya jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa mwanachama anapostaafu anapata mafao bora yatakayomwezesha kumudu maisha ya uzeeni wakati huo akiwa hana tena nguvu ya kufanya kazi ili kujipatia kipato cha kumudu mahitaji yake.
Ingawa wanachama wengi wa mifuko ya hifadhi ya jamii wanajua vilivyo madhumuni ya michango yao kwenye mifuko hiyo ni kujiandalia maisha ya uzeeni, mabadiliko haya ya kisheria yamepokelewa kwa upinzani mkali kutoka kwa wadau mbalimbali ambao ni wanachama wa mifuko hii.
Miongoni mwa wadau hao ni wafanyakazi wa migodini, walimu na wadau wengine wengi. Ukifuatilia kwenye vyombo vya habari kama magazeti, mitandao ya kijamii na hata vijiweni kuna mijadala mikali inayoendelea juu ya sheria hii mpya; watu wanasema na kuhoji wazi kuwa uamuzi huo kwanza hakuwashirikisha wanachama wa mifuko hiyo ambao ni wafanyakazi, lakini pia ni maamuzi ya kikandamizi ambayo yanalenga kuwaumiza zaidi wafanyakazi kwa kuwa siyo wote watajaliwa umri mrefu wa kuishi hadi miaka 55 na zaidi.
Pia wanahoji mantiki ya kung’ang’ania fedha za mwanachama ambaye amethibitisha pasi na shaka yoyote kwamba hana ajira yoyote ya kumwezesha kuendelea kuchangia akiba katika mifuko hiyo.
Tunajua suala usalama wa fedha za wanachama katika mifuko ya jamii limekuwa tete kwa miaka mingi; wananchi wengi wamejenga dhana ambayo siyo vema kuipuuza kwamba fedha zao zimekuwa zikitumika katika mambo ambayo aghalabu hayana faida nao; kuna wengine wamediriki kusema kuwa fedha zao zinatumika kifisadi kama ambavyo imeshuhudiwa kwenye baadhi ya miradi ambayo siyo vema kuitaja hapa.
Kadhalika, wamesema kuwa kumekuwa na juhudi ama ndogo sana au isiyoridhisha kutoka kwa mifuko hii kutoa elimu kwa wanachama wake juu ya usalama wa fedha zao; ni kwa nini kuwekeza, na ni kwa taratibu zipi hasa mwanachama anastahili kusubiri hadi miaka 55 ndipo aanze kunufaika na fedha zake.
Kwa miaka mingi mifuko ya hifadhi ya jamii ilikuwa ikijiendesha bila kuwa na chombo cha kuwadhibiti, SSRA ni matokeo ya juhudi za kutaka kuweka udhibiti juu ya mwenendo na utendaji wa mifuko hii, kwa maana hiyo wanachama wa mifuko hii katika kipindi hiki ambacho SSRA imeanza kufanya kazi wangependa kuona uwazi zaidi katika matumizi ya fedha zao katika mifuko hii na kwa ujumla mwenendo wa uwazi zaidi kwa kila kitu.
Kadhalika, wanachama wangependa kujua katika kipindi hiki kuelekea miaka 55 kama mwanachama hawezi kujiondoa na kuchukua fedha zake kwenda kuanzisha shughuli nyingine ya kujikimu, ananufaika vipi, ni kwa mafao gani hasa anaweza kujisikia fahari kuacha fedha hizo hadi umri wake ufikie miaka 55 na kuendelea?
Kama tulivyosema hatuna majibu ya mambo haya, pia haya yote yanayoelezwa na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii siyo mambo ya kupuuza. Sisi tunasema maswali haya yote yanayoibuka kutokana na marekebisho ya sheria hizi yanapaswa kupata majibu sahihi. Hapana shaka SSRA watabeba jukumu hili ili kujenga hali ya kuaminiana baina ya mifuko na wanachama wake.