Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kishindo cha James Millya chazidi kuitikisa UVCCM

25th April 2012
Print
Comments
Aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya ambaye alihamia Chadema

Siku chache baada ya Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mrisho Gambo, kumtaka aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya, kurudisha fedha za Chama cha Kuweka na Kukopa (SACCOS) cha jumuiya hiyo, jumuiya hiyo mkoa imekanusha madai hayo na kusema UVCCM haijawahi kuwa na mradi huo.

Tamko la kumsafisha Millya dhidi ya tuhuma hizo za wizi wa Sh. milioni mbili lilitolewa jana na Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Abdallah Mpokwa.

Mpokwa alisema hayo katika kikao cha Kamati ya Utekelezaji Baraza Kuu la UVCCM, Mkoa wa Arusha, kilichojumuisha wenyeviti na makatibu wa wilaya zote za mkoa huo.

Aidha, Mpokwa alikanusha madai kwamba Millya alitakiwa kukabidhi ofisi baada ya kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) takribani wiki mbili zilizopita na kufafanua kuwa kwa mujibu wa taratibu, Millya hakuwa na ofisi kutokana na kutokuwa mtendaji wa jumuiya.

Alisema kuwa Millya kama mwenyekiti, jukumu lake lilikuwa ni kufungua mikutano na kwamba kanuni za umoja wao zinaeleza kuwa mtendaji na mwenye ofisi ni katibu, hivyo tuhuma hizo dhidi ya Millya hazina ukweli.

“Mimi ninachosema haya matamko yanatolewa na watu wasioutambua umoja wetu, huyu Gambo alifukuzwa katika kikao chetu tulichofanya Longido na hatumtabui,” alisema na kuhoji: “Sasa anatoa matamko kama nani?”

Kuhusu madai ya Millya kuchukua fedha za SACCOS, alisema halijawahi kuwepo katika kumbukumbu za ofisi zao kuhusu kuwepo kwa mradi wa SACCOS.

Mpokwa alisema kuwa kujitoa kwa Millya ni haki yake kama kanuni ya Ibara ya 19 (a), kipengele cha (1) hadi cha (4) kwamba mwanachama kujitoa ni haki yake ya msingi.

Hata hivyo, alisema pamoja na wimbi la kuondoka kwa baadhi ya viongozi na wanachama wa UVCCM, umoja huo haujatetereka wala hautatetereka na kwamba kwa sasa wanajiandaa na uchaguzi katika ngazi zote.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Longido, Ngiono Nangelesa, alikanusha uvumi kuwa amejitoa CCM na kujiunga na Chadema na kuongeza kuwa hana mpango huo.

Gambo, akiwa na wenzake Kennedy Mpumilwa ambaye ni Mjumbe UVCCM Wilaya ya Arumeru walimtaka Millya kukabidhi ofisi ya UVCCM na kurudisha fedha za SACCOS zilizotolewa na makada wa CCM, Elisa Mollel na Felix Mrema.

Walidai kuwa fedha hizo zilitolewa katika kikao cha kwanza cha baraza la vijana, kilichofanyika Karatu mwaka 2008.
Aidha, walidai kuwa Millya amekula Sh. milioni 600 za makusanyo ya kodi za nyumba katika jengo la UVCCM.

Millya alijitoa CCM na kujiunga na Chadema akisema kuwa amechukua uamuzi huo baada ya kubaini kuwa Chadema ndicho chama pekee kinachoweza kuwakomboa Watanzania.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles