


Maeneo mengi ya kulaza magari kwa malipo yanayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), yameelezwa kuwa si salama kutokana na ulinzi wake kuwa ni wa kawaida huku magari yanayolazwa yakiwa ni ya thamani kubwa.
Maeneo ambayo si salama yameelezwa kuwa ni yale yanayomilikiwa na CCM ngazi za kata ambayo yameanzishwa kienyeji kwani hata taratibu za kisheria kama kuwa na bima hazikuzingatiwa.
Aidha maeneo hayo ambayo mengi yapo kwenye makazi ya watu, yamekuwa kero nyakati za jioni na usiku kutokana na wamiliki wa magari hayo kuyalaza bila utaratibu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa maeneo ambayo ni salama ni machache hasa yale ambayo yako kwenye ofisi za wilaya tofauti na yale yaliyopo kwenye ofisi za kata na vitongoji.
Hata hivyo upo wasiwasi mkubwa kama fedha zinazoingia kutokana na biashara hiyo endapo zinalipa kodi.
Utaratibu huo wa maegesho unaonekana haufahamiki rasmi makao makuu ya CCM na hivyo kuonekana ukiendeshwa kienyeji zaidi.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema suala hilo hawezi kulizungumzia kwani halijui na badala yake wenye wajibu wa kulijua ni CCM Mkoa na Wilaya.
“Unajua si kila kitu kinaendeshwa na makao makuu, kuna masuala mengine ni miradi iliyoanzishwa na mikoa, wilaya, kata na hata vitongoji. Nenda kawaulize huko,” alisema Nnauye.
Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam, Katibu wa CCM wa Mkoa Abilahi Mihewa, alionekana kutoifahamu kinagaubaga biashara hiyo jinsi inavyoendeshwa.
Alisema kuwa kuhusu suala la kodi, CCM kama taasisi inalazimika kulipa kodi hasa katika miradi yake.
Hata hivyo hakuzungumza kwa undani zaidi endapo maegesho hayo yanalipa kodi na badala yake alizungumzia ulipaji wa jumla kama taasisi.
Kuhusu usalama wa magari yanayoegeshwa katika maeneo ya ofisi hizo, alisema inawezekana mengine si salama ingawa alikiri mengine ni salama.
“Unajua kama kuna vijieneo vingine vimeibuka na kulaza magari, na hawakujiandaa kwa biashara hiyo kwa maana ya usalama wa magari, ni suala la uelewa wa watu tu, watu wengine uelewa wao ni mdogo…,” alisema.
Hata hivyo alikiri kuwa haifahamu vizuri Dar es Salaam hasa ofisi za CCM na maeneo yake kutokana na kuwa na miezi sita tu tangu ahamishiwe jijini hapa.
Kutokana na mazingira hayo, alisema anakusudia kuandaa ziara ya kutembelea maeneo mengi ili kujionea mambo yanavyoendeshwa huko.