Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kibaha yapambana na makazi holela

24th May 2012
Print
Comments

Ili kufanikisha azma ya upangaji wa miji na kuepuka makazi holela, Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kwa kushirikiana na kampuni ya Kibaha Golf Course Estate Development, imepima viwanja vya makazi na biashara zaidi ya 169 ambavyo vitaanza kuuzwa wiki ijayo.

Tayari Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ametangaza zoezi la uuzaji wa viwanja hivyo vilivyopo eneo la Pangani Kibaha, kilometa 4.5 kutoka barabara ya Morogoro na kilometa 1.5 kutoka eneo jipya la biashara la mji wa Kibaha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, huduma ya umeme ipo umbali wa kilometa 1.5 kutoka kwenye viwanja hivyo na kwamba mikakati iliyopo ni kufikisha nishati hiyo kwenye mradi pamoja na huduma nyingine za kijamii yakiwemo maji.

"Wananchi, makampuni na taasisi zinazohitaji viwanja wanakaribishwa kufika ofisi ya Mkurugenzi wa Mji wa Kibaha kuanzia Mei 28, kuchagua kiwanja kwenye ramani zitakazokuwa zimebandikwa kwenye mbao za matangazo," ilieleza taarifa hiyo ya Mkurugenzi.

Hata hivyo, taarifa hiyo ilieleza kwamba mwombaji atatakiwa kulipa Sh. 10,000 kama ada ya maombi pamoja na asilimia 25 ya gharama za kiwanja atakachochagua.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja mradi wa kampuni ya Kibaha Golf Course Estate Development iliyopima viwanja hivyo, Gaston Sanga, alisema viwanja 159 ni makazi na 10 ni kwa ajili ya makazi na biashara.

Aliongeza kuwa hivi sasa utafiti unafanyika kwenye eneo hilo kubaini maji yaliyo chini ya ardhi na kuyachimba ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.

"Kila mmoja anaweza kufika kwenye kiwanja kwa barabara zilizochongwa kwa sababu vyote vipo kwenye ramani, sasa hivi tunafanya utafiti wa maji na tayari tumewasiliana na Shirika la Umeme (Tanesco) ili liweze kufikisha umeme ndani ya mradi, tunaamini kwamba kuishi kwenye makazi yaliyopimwa ni bora kwa sababu hata thamani yake inapanda kila siku," alisema. Sanga alisema viwanja hivyo ni vikubwa kuanzia mita za mraba 600 hadi 3,000.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles