Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Simba yadharau kundi Kagame

1st July 2012
Print
Comments

Siku moja baada ya Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kutaja makundi na ratiba ya mashindano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Simba imesema haitishwi na timu walizopangwa nazo Kundi A.

Katika makundi yaliyotangazwa juzi, Simba ipo kwenye Kundi A linaloonekana kuwa la kifo ikiwa na timu za URA ya Uganda, Vita Club ya JK Kongo na Ports ya Djibout.

Lakini akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema Simba haina hofu na kundi hilo na ina uhakika wa kuibuka kinara.

"Timu inafanya maandalizi kwa lengo la kuchukua ubingwa wa mashindano haya, tumeona makundi yalivyopangwa, hatuna hofu na timu yoyote," alisema na kueleza zaidi, "nawahakikishia hakuna timu itakayotuzuia."

Aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye michezo ya Simba ili kuwaona wachezaji wapya na uwezo wao.

Simba ndiyo inaongoza kwa kutwaa mara nyingi zaidi ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati tangu michuano huyo ianzishwe mwaka 1974 mara sita.

Ilitwaa ubingwa wa michuano ya kwanza mwaka 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002 wakati michuano hiyo ilipofanyika ama Bara au Zanzibar.

Simba itafungua mashindano hayo kwa kucheza na URA Jumatatu Julai 16 kwenye Uwanja wa Taifa.

Mashindano hayo yataanza Julai 14 kwa mchezo wa ufunguzi kati ya mabingwa watetezi Yanga na Atletico ya Burundi.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment