


.jpg)
Pendekezo la serikali kutaka kupunguza umri wa magari unaoingia nchini uwe wa miaka minane kutoka miaka 10, limekwama.
Pendekezo hilo liliibua mvutano mkubwa bungeni jana, baada ya wabunge kulipinga na kusababisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuingilia kati.
Mvutano uliibuka wakati serikali ilipowasilisha muswada wa sheria ya fedha utakaowezesha ukusanyaji wa mapato kwa mwaka 2012/13 kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa bajeti yake.
Akiwasilisha muswada huo, Waziri wa Fedha William Mgimwa, pamoja na mambo mengine, alisema serikali inakusudia kupunguza muda wa magari yaliyotumika kuingia nchini ili kudhibiti magari chakavu, kutunza mazingira na kuwapunguzia wananchi mzigo wa kununua mafuta kwa kuwa yanatumia nishati hiyo kwa wingi.
Alisema serikali inatekeleza hoja hiyo kwa kuwa hata Kenya na Uganda wameanza kufanya hivyo na kwamba ni mpango wa nchi nyingi.
Baada ya kuwasilisha muswada huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, iliwasilisha maoni yake na kupinga pendekezo hilo la serikali kwa kueleza kwamba uwezo wa wananchi wengi kununua magari mapya ni mdogo hivyo pendekezo hilo litawaumiza.
Akiwasilisha maoni ya kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Andrew Chenge, alisema serikali pia haina nia ya kuyaondoa barabarani magari yenye umri zaidi ya miaka 10 hivyo pendekezo hilo halina manufaa kwa taifa.
“Kamati ina amini kwamba sababu zilizofanya serikali kuleta mapendekezo bungeni mwaka 2006 ya kutoza ushuru wa bidhaa za magari yenye umri zaidi ya miaka 10 bado zina nguvu hadi leo…kamati inashauri umri wa magari yanayostahili msamaha uwe miaka 10 na sio minane inayopendekezwa,” alisema.
Msimamo huo wa Kamati uliungwa mkono na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambayo ilisema hoja ya serikali katika eneo hilo ni dhaifu kwa kuwa wananchi wengi hata wabunge hawana uwezo wa kununua magari mapya na wala umri wa gari sio kigezo pekee cha ubora.
Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Christina Mughwai, alisema inashangaza serikali inaleta mapendekezo hayo miezi michache baada ya kuleta muswada wa kuiruhusu kununua vyombo ‘chakavu’ vya usafiri ambayo imepitishwa na Bunge.
Baada ya msimamo huo, Bunge lilikaa kama kamati kwa ajili ya kupitia kifungu kwa kifungu ili kupitisha muswada huo, lakini wabunge hususani wa CCM akiwamo Peter Serukamba (Kigoma Mjini na Christopher Ole Sendeka, waliungana na kamati pamoja na kambi ya upinzani.
Akijibu, Waziri Mgimwa alisisitiza kwamba azma hiyo inalenga kulinda mazingira na kuwasaidia wananchi wanaotumia magari kwa kuwapunguzia mzigo wa kununua mafuta kwa kuwa magari chakavu yanatumia mafuta mengi.
Kadhalika, Mgimwa alisema magari chakavu yanachangia kuongeza ajali.
Majibu hayo yaliibua hasira za wabunge ambao walimpinga walieleza kuwa magari chakavu sio pekee yanayochafua mazingira kwa kuwa ukataji miti kwa ajili ya mkaa ni eneo linalochangia zaidi uharibu wa mazingira nchini.
Mvutano huo ulimlazimu Waziri Mkuu Pinda kuingilia kati na kueleza kwamba serikali imekubaliana na maoni ya wabunge na kukubali umri wa magari yanayoingia nchini uwe miaka 10.
Hata hivyo, Pinda aliwataka wabunge wafanye utafiti zaidi juu ya athari za magari chakavu ili ikiwezekana baadae wazo hilo la serikali liridhiwe na Bunge.
Kadhalika, wabunge walipinga pendekezo la serikali kutaka kuongeza ushuru wa maji ya chupa kutoka Sh. 69 hadi Sh. 83 kwa lita moja na pia ile ya kupandisha ushuru wa muda wa maongezi.
Baada ya mvutano, serikali ilikubaliana na wabunge na kukubali kushusha ushuru wa maji ya kunywa ya chupa hivyo ushuru huo umebakia Sh. 69 kwa lita moja huku ikipandisha ushuru wa muda wa maongezi kwa asilimia mbili kutoka asilimia 10 hadi 12.
KAMATI YA MGWILIZI YALAZA KAZI
Kamati ndogo iliyoundwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuchunguza tuhuma za baadhi ya wabunge kuhongwa na kampuni za mafuta, imeshindwa kukamilisha kazi yake katika muda wa wiki mbili iliyopewa.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Naibu Spika, Job Ndugai, alisema Kamati ya Kudumu ya Uongozi iliyoketi jana mchana iliona kuwa kamati hiyo ingetoa maelezo, lakini kutokana na suala la muda imeshindwa kupatiwa muda.
“Tumejaribu kuangalia muda ili angalau waje waeleze kidogo, lakini tukaona haiwezekani kabisa labda mkutano ujao wa Bunge,” alisema Ndugai.
Alisema baadhi ya wabunge wale waliosafi wanataka Bunge kuweka wazi kuwa hawakuhusika ili wabunge hao watakapoenda majimboni kuepuka kukashifiwa.
Hata hivyo, alisema kutokana na kukosa muda wameshindwa kusema chochote kabla ya Mkutano wa Nane kuahirishwa jana jioni.
Habari ambazo NIPASHE ilizipata kutoka katika kikao cha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi usiku, zinaeleza kuwa Mbunge wa Viti Maalum, Munde Tambwe na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika Makinda, Selemani Zedi, waliibuka na kutaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye ni mwenyekiti wa wabunge hao kumwambia Spika awasafishe bungeni.
Walisema hatua hiyo itawawezesha kwenda majimboni wakiwa wasafi na kuepuka kwenda kusakamwa mara watakaporejea majimboni mwao.
Kamati hiyo ndogo iliyoundwa kutoka Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali Mstaafu, Hassan Ngwilizi, ilipewa wiki mbili kumaliza kazi ya kuchunguza tuhuma hizo, ambazo zinadai kuwa wabunge kadhaa walihongwa na kampuni za mafuta ili kushinikiza kuondolewa kwa Waziri wa Nishati na madini, Profesa Sospeter mhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.
Maswi alituhumiwa kuipa zabuni Kampuni ya Puma kuiuzia serikali mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura.
Naye Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, juzi alisema kuwa kama kamati hiyo bado haijakamilisha kazi yake inaweza kuomba kwa Spika kuongezwa muda ili imalizie kazi yake iliyopewa.
“Wao wanaweza kuomba kuongezwa muda kwa Spika kama hawajakamilisha kazi yao ili waweze kukamilisha,” alisema Dk. Kashililah.