Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Nguvu kubwa itumike kutangaza utalii

15th July 2012
Print
Comments

Moja ya rasilimali zetu muhimu hapa nchini ni utalii, yapo maeneo mengi ya asili yenye historia kubwa na muhimu kwa vizazi vilivyopo na ustawi wa kizazi kijacho.

Si sahihi kwa wageni wanaokuja nchini kutukumbusha umuhimu wa kutangaza rasilimali zetu zilizohifadhiwa kwa faida yetu kiuchumi. Nchi yetu ina bahati kubwa duniani kuwa na vivutio vingi vya utalii ambavyo kwa bahati mbaya sana hata baadhi ya wananchi wetu bado hawajapata elimu ya umuhimu wa kutembelea vivutio hivyo.

Katika kipindi cha mwaka uliopita, Zanzibar ilitangaza kuwa imepokea watalii wengi zaidi kuliko miaka mingine iliyopita, na mapato ya serikali yaliyotokana na biashara ya utalii yaliongezeka zaidi kuliko miaka mingine.

Juhudi zinazofanywa na Zanzibar za kutangaza vivutio vya utalii visiwani humo zinatokana na mahusiano ya ofisi za mabalozi na nchi marafiki, matangazo kwa njia ya vipeperushi pamoja na kuonyesha kwenye fukwe zao zilivyo tulivu na za kuvutia.

Kwa upande wa Tanzania Bara, kuna maeneo mengi ya kuwavuta watalii wa ndani na nje kwenda kutembelea, ukiacha maeneo ya mbuga nyingi zilizopo za wanyama, mlima Kilimanjari ni moja ya vivutio vikubwa kutokana na kuwa ndio mlima mrefu kuliko yote barani Afrika ambao pia unahifadhi wanyama waliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.

Hifadhi nyingi zinajidhihirisha kuwa ni maajabu ya dunia, kama ile iliyoko katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambako maelfu ya wanyama wanaishi ndani ya pango kubwa la asili sambamba na wananchi wa jamii ya wafugaji na kulifanya eneo hilo kuwa kivutio kikubwa kwa wote wanaotembelea huko. Jamii hiyo ya wafugaji nayo huwa sehemu ya kivutio kwa watalii.

Kutokana na hali ya uchumi duniani kuyumba kuanzia miaka mitatu iliyopita, hali ya kibiashara ya kimataifa bado haijatulia, kumekuwepo na hali ya kupanda bei kwa kila bidhaa na kusababisha maisha ya wananchi wengi kuwa magumu.

Athari mojawapo iliyojitokeza kutokana na mtandao wa biashara za kimataifa ni kushuka kwa thamani ya shilingi. Hali hiyo imetuacha tukiendelea kufadhaika na kuanza kuinung'unikia serikali, tumesahau kuwa wakati nchi zilizoendelea zinatafuta masoko ya bidhaa zao kwa gharama kubwa, sisi pia tungetumia fursa ya kutumia urithi wa rasilimali zetu kwa kuzitangaza kwa nguvu zote ili watalii wengi zaidi waje nchini kutalii pamoja na kuwekeza.

Nina imani kuwa mikakati ya makusudi ya kutangaza utalii katika nchi mbalimbali duniani ipo, na inawezekana pia ofisi za mabalozi wetu huko duniani zinafanya mipango ya kuitangaza Tanzania katika nyanja za utalii na fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Ninafahamu pia gharama za kujitangaza ni kubwa, lakini faida zake ni kubwa zaidi kwani watalii wengi wakija nchini, wao pia wanakuwa mabalozi wa kuitangaza Tanzania warejeapo nchini mwao, na zoezi hili likifanyika kwa muda mrefu, Tanzania inaweza ikawa moja kati ya nchi zitakazojizolea fedha za kigeni kwa wingi na hatimaye kupunguza umaskini uliokithiri sasa.

Miezi michache iliyopita, Balozi wa Ufaransa nchini Marcel Escure alisema Tanzania inatakiwa kufanya kampeni maalumu nchini Ufaransa ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania kutoka Ufaransa iongezeke. Alisema wananchi wa Ufaransa wanapenda sana kutembelea nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kujionea maajabu ya dunia.

Kutokana na wito wa Balozi Escure, ambaye ameshika wadhifa wa kuwa Balozi nchini hapa kuanzia mwaka jana, ni dhahiri kuwa wananchi wengi wa Ufaransa hawajui kama Tanzania ni kitovu cha vivutio vya utalii duniani. Inawezekana tatizo kama hilo lipo katika nchi nyingi, lazima sasa Wizara inayohusika itoe kipaumbele kwa kuitangaza utalii wa Tanzania duniani kote.

Kwa kuona umuhimu wa biashara ya utalii hapa nchini, Balozi Marcel Escure wa serikali ya Ufaransa na Tanzania wanashirikiana kwa karibu sana na ndio maana nchi hizo zipo katika mpango wa kuanzisha Chuo cha Utalii kitakachokuwa na hadhi ya kimataifa.

Balozi huyo aliongeza kuwa hali ya uchumi ni ngumu katika kila kona ya dunia ikiwa ni pamoja na nchi za Ulaya na akakiri kuwa kwa kiasi fulani Tanzania inajitahidi kupiga hatua, akaongeza kuwa Watanzania wanapaswa kujivunia kwa kuwa na nchi nzuri yenye vivutio vingi pamoja na utulivu, amani na watu wake wakarimu na wacheshi.

Mkazo mkubwa uliwekwa katika sekta nyingine za uzalishaji, imegundulika kuwa maliasili nyingine kama madini si miradi endelevu, kuna wakati madini yatachimbwa hadi kumalizika ardhini, tofauti na sekta hii ya utalii ambayo inategemea zaidi umakini katika uhifadhi na kuyatunza mazingira yaendelee kuwa ya asili.

Uhifadhi makini wa vivutio hivyo ndio gharama kubwa ya kuendeleza maliasili hizo katika Hifadhi za Taifa. Kupambana na ujangiri, uchafuzi wa mazingira pamoja na kuheshimu sheria zinazomiliki ustawi wa maliasili hiyo ni jambo la msingi katika kuendeleza urithi huu adimu tuliojaliwa na Mwenyezi Mingu.

Ni wajibu pia wa vyombo vya habari kuitangaza Tanzania katika sura ya kuwavutia watalii, hata kama yapo mapungufu ya ndani yazibwe na vyombo vya habari badala ya kuelezea kila kitu kwa uwazi, mfano wa vibaka walioko katika fukwe, habari kama hizo zikisomwa na wageni huwa ni kikwazo.

Maoni; 0715-047304 na 0762-233116

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment