Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Hongeza Waziri kwa kujiuzulu

25th July 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Juzi aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Masoud Hamad, alijiuzulu wadhifa huo ukiwa ni uwajibikaji wa kisiasa kutokana na ajali ya boti ya mv Skagit iliyozama bahari ya Hindi ikiwa safarini kutoka Dar es Salam kwenda Zanzibar na kuua takribani 150, kati ya 290 waliokuwamo.

Boti hiyo ilizama Jumatano iliyopita (Julai 18) umbali wa takribani kilometa 19 kutoka bandari ya Malindi eneo la kisiwa cha Chumbe saa 7:30 mchana ikiwa imeanza safari yake katika bandari ya Dar es Salam saa 6:00 mchana siku hiyo.

Hadi sasa ni maiti 73 tu zimepatikana huku idadi watu waliyookolewa ikielezwa ni 150, ingawa taarifa zinasema kuwa huenda watu ambao hawajulikani waliko ni 67; kumekuwa na taarifa za kukanganya juu ya idadi hasa ya watu waliokuwa kwenye boti hiyo.

Ajali hiyo ni ya pili kubwa kutokea visiwani huko Waziri huyo akiwa na dhamana ya miundombinu na mawasiliano. Septemba mwaka jana meli ya mv Spice Islander ikiwa safarini kwenda Pemba ilizama kwenye mkono mkali wa bahari ya Hindi eneo la Nungwi na kuua mamia ya watu.

Katika janga la mwaka jana, Waziri Masoud aliomba kupewa muda wa kujipanga kwani ndiyo kwanza alikuwa hata hajafikisha mwaka katika wizara hiyo, kwa maana hiyo baada ya kutokea janga hili tena ametangaza kujiweka pembeni mwenyewe bila kusubiri kishinikizwa na yeyote kwa kutambua yaliyotokea chini yake ili kupisha uchunguzi ufanyike.

Serikali ya Zanzibar nayo imetangaza kuundwa kwa tume ya kuchunguza janga hili, ili pamoja na mambo mengine kubaini chanzo chake, kutazama kwa kina sheria ya usafiri wa baharini visiwani huko na ikibidi kurekebisha sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA) ili kuepuka na majanga kama hayo katika siku zijazo kutokana na kuruhusiwa kwa meli chakavu kusajiliwa.

Tunampongeza Masoud kwa kuungwana wake wa kutambua kuwa kisiasa anao wajibu wa kujiuzulu wadhifa huo kutokana na majanga haya ambayo yamekuwa yakiiandama sekta ya usafiri wa baharini Zanzibar.

Hakika Masoud ameonyesha utamaduni mpya katika usimamizi wa majukumu katika ofisi ya umma. Ameonyesha bila kinyongo kwamba yanapotokea ya kutokea katika eneo lako la kazi uwajibikaji ni jambo la umuhimu bila kusubiri kusukwa sukwa na kushinikizwa, ameonyesha mfano kuwa ofisi ya umma ni dhamana.

Itakumbukwa kwamba mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya mawaziri wanane na naibu mawaziri wawili kushinikizwa na wabunge wajiuzulu kutokana na utendaji usioridhisha, wizi wa mali ya umma na ubadhirifu katika maeneo waliyokuwa wanayasimamia.

Ingawa mawaziri hao walikuwa wizara zao zikuwa zimetajwa kwa majina kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2009/10 ikionyesha madudu katika wizara zao, hawakuwa radhi kujiuzulu wenyewe, waling’olewa katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika.

Tumekumbusha kisa cha mawaziri hao ili kufananisha na alichokitenda Masoud kuonyesha tofauti ya uelewa, uadilifu na kutambua kuwa cheo ni dhamana inayoweza kuondoka kama mambo yatakwenda mrama kwenye usimamizi wa majukumu na uwajibikaji kwa ujumla. Huyu ameonyesha mfano na unatakiwa kuigwa na kuenziwa na wote wanaokalia ofisi za umma.

Masoud amesema kuwa hakusubiri kushinikizwa, amemrahisishia kazi Rais wa Zanzibar, kwanza kuondoka ili nafasi yake ujazwe na mtu mwingine, lakini pili kuiwezesha tume itakayoundwa kuchunguza janga hilo kuwa na uhuru wa kufanya kazi bila yeye (Masoud) kuweka humo mikono yake. Huu ni uadilifu na ukomavu wa kisiasa ambayo kwa hakika unatakiwa kujengwa nchini.

Pamoja na pongezi hizi, tungependa wajumbe 10 wa tume hiyo walioteuliwa jana na SMZ kufanya kazi kwa bidii na uadilifu katika kuchunguza janga hili na mwishowe hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Tunakumbuka kuwa wakati wa janga la meli ya mv Spice Islander hatua za kisheria zilichukuliwa dhidi ya watumishi wa umma na wamiliki wa meli hiyo, safari hii tungependa kuona hatua kali zaidi ili kwa kweli kuleta uwajibikaji kwa pande mbili zinazohusika na usafiri wa majini, yaani serikali na wafanyabiashara wanaomiliki vyombo vya usafiri. Hatua hizi zitasaidia kuiponja nchi na majonzi ya kila mara.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment