Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Haki za binadamu waingilia kati sakata la aliyejifungua amesimama

29th April 2012
Print
Comments

Sakata la mwanamke kujifungua akiwa amesimama limeingia sura mpya baada ya Mashirika ya kutetea haki za binadamu kuingilia kati na kuitaka Serikali kuwaadhibu watu waliohusika na uzembe huo.

Katika tukio hilo lililotokea wiki iliyopita na kuripotiwa na gazeti hili, mwanamke huyo Kuruthum Abdallah (30), mkazi wa Majohe jijini Dar es Salaam alijikuta akijifungua akiwa amesimama katika Hospitali ya Amana na kusababisha kichanga kudondoka sakafuni.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11: 30 jioni baada ya mwanamke huyo kufikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya kupata huduma ya kujifungua, lakini alipofika wodini alilazimishwa kusimama na mmoja wa wauguzi hadi alipojifunga kichanga hicho ambacho kwa kudura za Mungu kilinusurika kufa.

Hata hivyo wakati mashirika hayo yakitoa kauli nzito juu ya tukio hilo, Uongozi wa Hospitali hiyo umeshakutana na mume wa Kuruthum, Jabir Yahya na kumuomba radhi na kutaka suala hilo liishe kwa kutotoa taarifa yoyote kwenye vyombo vya habari.

Wakizungumza na NIPASHE Jumapili, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Ananilea Nkya alishutumu vikali tukio hilo na kueleza kuwa Serikali inatakiwa kuwaadhibu wauguzi waliosababisha tukio hilo.

Alisema hatua ya uongozi wa Amana kumuomba radhi mume wa mwanamke huyo haitoshi kwa sababu hakuna suala la kijinai likaisha kwa kirahisi hasa ikiwa ni tukio la kutaka kutoa uhai wa mtu.

Nkya alieleza matukio ya wauguzi na watendaji wa Hopitali za Serikali kuacha wajibu wao wa kazi yamekithiri na hali hiyo inatokana watu wanaoajiriwa kutokuwa na wito na walioajiriwa bila kufanyiwa vipimo maalum.hawakustahili kupewa kazi hizo.

"Pamoja na Uongozi wa Hospitali kuomba radhi, hilo halitoshi kinachotakiwa ni kumchukulia adhabu kali mtu aliyehusika pamoja na kutoa elimu kwa wafanyakazi wote juu ya majukumu yao ili kuwafanya wawajibike ipasavyo," alisema Nkya.

Alisema hakubaliani na suala hilo kuisha hivi hivi kama vile biashara ya nyanya na kumtaka wazazi wa mtoto huyo kwenda katika vyombo vya sheria kuwachukulia hatua watu wote waliohusika na suala hilo.

"Kweli kumfanya mama mjamzito kujifungua huku amesimama halafu unasema liishe mezani? alihoji

"Hapana, hapana, lazima sheria ifuate mkondo ili iwe fundisho na hili litafanyika endapo wazazi wataamua kufungua mashtaka," aliendelea kusema Mkurugenzi huyo wa tamwa.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na haki za binadamu (CHRC), Hellen Kijo-Bisimba alisema uzembe uliofanyika hauvumiliki ni lazima Serikali isaidie jambo hilo haraka ikiwa pamoja na kumfanyia vipimo mtoto aliyezaliwa ili kufahamu athari alizopata.

Alisema kitendo cha mtoto kuangukia sakafuni kinaweza kumletea athari kubwa mtoto huyo huko baadaye na inatakiwa ifanyike uchunguzi huru wa kuangalia mtoto huyo kiasi gani ameathirika.

"Tukio kama hilo hata mimi lilinikuta nilipozaa mmoja wa watoto wangu, lakini niliweza kijiepusha kwa kukataa na kwenda sehemu ya kuzalia, ni jambo baya sana tena linaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto," alisema Kijo-bisimba.

Alitaka suala hilo lisichukuliwe kienyeji na kuomba jamii kulikemea kwa nguvu zote ili kuonyesha ni jinsi gani wanaguswa na tabia hizo zinazoonyeshwa na baadhi ya wauguzi wa hospitali mbalimbali za serikali.

Akizungumzia kikao hicho, Mume wa mwanamke huyo Jabir Yahya alisema aliitwa na uongozi wa hospitali hiyo kwa ajili ya mahojiano na kubaini kweli tukio hilo limefanyika.

Alisema katika kikao hicho cha pande mbili, uongozi huo ulimuomba radhi kwa tukio hilo na kumtaka asitoe taarifa katika vyombo vya habari.

"Tuliitwa kwa ajili ya kuhojiwa na kubaini ukweli wa tukio zima, kwa kweli ilibainika ni kweli mke wangu alijifungua akiwa amesimama. Walituomba radhi na kututaka jambo hilo liishe na tusitoe taarifa kwa waandishi," alisema Jabir.

Akizungumzia suala hilo Afisa malalamiko wa Hospitali hiyo, Agnes Mbuya, alisema anasikitishwa na tukio hilo ambapo uchunguzi mkali unafanyika kubaini watu waliohusika ili kuwachukulia hatua.

Alisema kwa sasa ni mapema kueleza ni hatua gani watakayochukua, lakini alibainisha endapo itaonekana kuna ukweli wa jambo hilo atalifikisha kwa Mganga Mkuu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua ya nidhamu.

"Tumeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuchunguza tukio zima lilivyotokea ili tuweze kuchukua hatua za nidhamu," alisema Mbuya.

Pamoja na hayo aliwataka wananchi wanaopatiwa huduma katika hospitali hiyo kutoa taarifa mapema pale wanapoona hawahudumiwi ipasavyo kwa ajili ya kuhakikisha watu hawapotezi ushahidi.

Kuruthum alifika hispitalini hapo akiwa katika dalili zote za mwisho za kujifungua, muuguzi aliyekuwa zamu siku hiyo alimtaka kwenda kubadilisha nguo zake na kisha amfuate hadi kwenye meza yake ili atoe maelezo yake.

Alieleza alipoelezwa hayo, alimjibu asingeweza kufanya hivyo kwa sababu ana kila dalili ya kujifungua kwa wakati huo na kumuomba ampeleke kwenye chumba cha kujifungulia (leba).

Hata hivyo, muuguzi huyo alionekana kuwa mkali na kumtaka afanye kama alivyomueleza kwani wakati wa kudeka umekwisha kwa kuwa hata huo ujauzito wakati anaupata hakuwepo.

Kuruthum alisema baada ya kujibiwa hayo, aliamua kumfuata muuguzi huyo hadi katika meza yake, lakini kipindi hicho uchungu uliongezeka kiasi cha kutoweza kusimama vizuri.

Alisema wakati anahangaika kujibu maswali, ghafla alishtukia mtoto akitoka kwa kasi na kuangukia sakafuni.

"Nilishtukia mtoto akitoka na kuangukia sakafuni na kisha kuserereka hadi chini ya meza, tukio lilinishtua sana na hata watu waliokaa mlangoni walipiga kelele ya hofu," alisema mama huyo.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles