Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Shule zinazoendeshwa bila vigezo, wakaguzi wako wapi?

10th June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Ni jambo la kufadhaisha na kusikitisha kuona kwamba sekta ya elimu inazidi kudorora na kiini chake kikiwa kinafumbiwa macho japokuwa kinaonekana dhahiri.

Zipo kelele nyingi zinapigwa na wananchi kuashiria kwamba sekta ya elimu imegubikwa na matatizo makubwa lakini badala ya kuchunguza kiini, serikali inahimiza wingi wa mashule bila kusimamia vigezo vinavyowekwa kama vinazingatiwa au la.

Mtu au taasisi inapotaka kuanzisha shule, yapo masharti ya msingi ambayo anapaswa kukubaliana nayo ikiwa ni pamoja na kusajili shule katika mamlaka husika, ambako hupewa kibali.

Na hata baada ya kukubaliwa, upo utaratibu wa kuzifanyia ukaguzi shule zetu kuona kama kweli yale yaliyokubaliwa wakati wa kuanzishwa kwake yanazingatiwa. Wakaguzi hawa wapo wizarani na wanatakiwa kila mwaka kutoa ripoti ya ukaguzi.

Huo ndio utaratibu wa serikali. Lakini kama hivyo ndivyo, kwanini shule katika miaka hii ambayo wigo wa maendeleo umepanuka zibainike kukosa vigezo na matokeo yake baadhi zifungwe na kuwanyima haki watoto kusoma kwa utulivu badala ya kuhamishwa hamishwa?

Kazi hii ambayo tunadhani imewekwa kando na wakaguzi, imeanza kufanya na uongozi wa juu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambapo kuanzia mwezi Januari mwaka huu zimefungwa kwa kinachoelezwa kukosa vigezo.

Miongoni ni shule ya sekondari ya Mabogo inayomilikiwa na Jumuia ya Wazazi ya CCM iliyoko Turiani Morogoro iliyofungwa juzi na Naibu waziri wa wizara hiyo, Philipo Mulugo.

Shule hiyo iliyoanza rasmi mwaka 2002, imepewa muda wa mwaka mmoja kuhakikisha inatimiza vigezo vyote vinavyopaswa kuwa sekondari huku akimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Antony Mtaka kusimamia amri hiyo na endapo viongozi wa Jumuiya hiyo watakiuka wakamatwe mara moja na kushitakiwa.

Baadhi ya vigezo ni pamoja na kukosa walimu wenye taaluma ya ualimu, madarasa kuwa manne ambayo yamejengwa chini ya kiwango, kutokuwepo jingo la utawala, ofisi ya mkuu wa shule, kutokuwa na samani eneo maalumu la kutunzia mitihani ya kitaifa pamoja na kutokuwepo kwa madawati ya kutosha.

Upungufu mwingine ni kutokuwepo maktaba, hakuna maabara, vifaa vya kufundishia kama vitabu, kutokuwa na mkuu wa shule mwenye taaluma ya ualimu, matundu ya choo hayatoshi, kutokuwa na mtaji wa kujiendesha badala yake kutegemea karo za wanafunzi jambo ambalo ni kinyume na uendeshaji wa shule za sekondari za binafsi.

Mulugo aligundua pia udanganyifu wa mtu aliyedai kuwa ndiye kaimu Mkuu wa shule jambo ambalo siyo kweli kwani alipotakiwa na waziri kuonyesha vyeti vyake vya ualimu alishindwa kuvitoa na alipobanwa alikiri kutokuwa na taaluma ya ualimu na alihitimu kidato cha sita Tosamaganga na kupata daraja la nne.

Madudu hayo ndiyo aliyogundua waziri Mulugo katika ziara yake. Sasa tunajiuliza, hivi idadi kubwa ya wanafunzi wanaofeli mitihani yao ni halali au kwa kiasi kikubwa kimechangiwa na vigezo vingi kukiukwa?

Na je, shule kama hiyo ya Mabogo, imewahi kukaguliwa na wakaguzi wizarani tangu ilipopewa namba ya usajili? Tuambizane ukweli. Serikali imekaa mezani na kuandaa taratibu nyingi zikilenga kuinua ubora wa elimu lakini wasimamizi ndio tatizo kubwa.

Haishangazi mwanafunzi wa darasa la saba anamaliza hajui kuandika hata barua ya kuombea kazi. Wengine tumesikia wanafaulu kwenda sekondari lakini wakifika huko hawajui kuhesabu wala kuandika. Tatizo hapa ni wakaguzi wetu wamelala usingizi.

Na ukiona shule kama hizo zilizofungwa zimekiuka masharti na kuendelea kutoa huduma ya elimu, ujue mlungula unatembea hapo. Rushwa imekuwa ni tatizo kubwa linaloitafuna nchi hii katika nyanja zote za maendeleo.

Nenda hata kwenye shule za awali. Zipo nyingi zimeanzishwa lakini ni chache sana zinazozingatia vigezo vya kuwepo kwake. Hizi hazina walimu makini bali wababaishaji na zingine walimu wanawafanyia watoto mitihani na kuwadanganya wazazi kuwa ni akili ya watoto kumbe ni udanganyifu mkubwa.

Ni wakati sasa wizara ya elimu ikafunguka na kuwavalia njuga wakaguzi wake wazifuatilie shule zote nchini kuona kama vigezo vinazingatiwa ili matatizo yagundulike mapema kabla taifa halijaangamia kwa kujaa watu mbumbumbu. Turejee misingi bora ya elimu yetu ili kujenga taifa makini la sasa na la baadaye. Mungu ibariki Tanzania yetu.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment