


.jpg)
Kocha wa timu ya soka ya Taifa ya Wanawake 'Twiga Stars', Charles Mkwasa, amesema hawatakuwa na sababu ya kutoifunga Ethiopia katika mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika leo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkwasa alisema kuwa kikosi chake kimefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mchezo wa leo ambapo wamepanga kucheza kwa kushambulia zaidi.
"Baada ya mchezo wa kwanza kule Adis Ababa, tuliporudi nyumbani tulifanya marekebisho ya makosa niliyoyaona na kwa sasa timu ipo tayari kwa ajili ya mchezo wa marudiano, hatutakuwa na kisingizio tukishindwa kuwafunga," alisema Mkwasa.
Aidha, alisema kuwa wanajua kuwa wanafahamu kuwa ni ushindi pekee ndio utakaowavusha kushiriki mara ya pili fainali hizo za Afrika.
"Wachezaji wapo kwenye morali na ujio wa nahodha wetu Sophia (Mwasikili) umeongeza hamasa kikosini," alisema.
"Tunawaomba watanzania wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti."
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, naodha msaidizi wa Twiga Stars, Asha Rashid 'Mwalala', alisema kuwa watafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanaibuka na ushindi leo.
"Tunaomba tu wanatanzania wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti, tunawahaidi hatutawaangusha, tutahakikisha tunaibuka na ushindi.
Kocha wa Ethiopia, Abreham Haimanot, alisema kuwa pamoja na kuifunga kwenye mchezo wa kwanza, wanafahamu Twiga Stars ni timu nzuri.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Adis Ababa, Twiga Stars ilifungwa 2-1 hivyo kuhitajika kushinda kwenye mchezo wa leo utakaoanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa.
Endapo Twiga Stars itafanikiwa kuibuka na ushindi itakuwa imefuzu kushiriki kwa mara ya pili katika fainali za Afrika za Wanawake zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Guinea ya Ikweta.