Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Simba yaifanyia mauaji Yanga

7th May 2012
Print
Comments
Mshambuliaji wa Simba,Felix Sunzu (kulia) akiwania mpira dhidi ya kipa wa Yanga, Yaw Berko wakati wa mechi yao ya kufunga msimu wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ilikuwa ni mechi ya kudhalilishwa. Hilo linaweza kuwa ni neno sahihi zaidi kulisema wakati unapozungumzia kilichowakuta Yanga dhidi ya Simba katika mechi yao ya watani wa jadi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana wakati Wekundu wa Msimbazi walipotoa kipigo cha "mbwa-mwizi" cha 5-0 dhidi ya mahasimu wao.

Penalti tatu, ikiwemo iliyofungwa na kipa Juma Kaseja, na magoli mengine mawili ya shambulizi yaliyopachikwa na mshambuliaji Emmanuel Okwi, ambaye amekuwa akituhumiwa kuwa haifungi Yanga, yaliipa Simba ushindi mnono zaidi dhidi ya mahasimu wao hao tangu walipoweka rekodi ya kipigo kikubwa zaidi katika mechi inayowakutanisha mahasimu hao cha 6-0 mwaka 1977. Yanga pia iliwahi kuifunga Simba 5-0 Juni Mosi mwaka 1968. 

Ushindi wa jana ulikuwa ni wa kurembesha tu keki ya sherehe za ubingwa ambao Simba waliupata Ijumaa baada ya washindi wa pili Azam kufungwa na Mtibwa 2-1 na hivyo kuwaacha Wekundu wakibeba kombe siku hiyo bila ya jasho.

Huku uwanja ukiwa umejaa mashabiki wa Simba waliokuwa wakishangilia ubingwa wao na mashabiki wachache wakionekana katika majukwaa ya Yanga, mabingwa wapya walianza mchezo wa jana kwa kishindo na kupata goli la kwanza katika dakika ya 1 kupitia kwa Mganda Okwi akimalizia pasi ya Mwinyi Kazimoto, na kuanza kurejesha imani yake kwa mashabiki wenye mtazamo hasi dhidi yake ambao hubeba mabango yasemayo "Mchango wako tunauona na tunauheshimu, lakini mbona huifungi Yanga?". 

Okwi ambaye amethibitisha kuwa mchezaji bora katika kikosi cha Simba msimu huu, aliendelea kuisumbua ngome ya Yanga na baada ya timu hizo kurejea kutokea mapumziko huku matokeo yakiwa 1-0, beki Shadrack Nsajigwa alimuangusha Mganda huyo katika eneo la penalti na kuzaa "tuta" la kwanza lililofungwa na kiungo Mzambia Felix Sunzu katika dakika ya 54.

Okwi tena akaifungia Simba goli la tatu katika dakika ya 61 baada ya kuwatoka mabeki wawili wa Yanga, Nsajigwa na Athumani Idd 'Chuji' kufuatia pasi ya Jonas Gerald.  

Dakika sita baada ya goli la tatu, Simba ilipata goli la nne kwa njia ya penalti tena iliyotolewa na refa Hashima Abdallah baada ya kipa Said Mohammed aliyeingia mwanzoni mwa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Yaw Berko, kumdaka Okwi aliyekuwa akielekea kufunga. Kaseja akapiga penalti hiyo na kuifunga goli la nne timu aliyowahi kuichezea kwa msimu mmoja na kuisaidia kuipa ubingwa.

Kipa Said, ambaye amekuwa hana namba kikosini Yanga, kutokana na kuwa chaguo la tatu nyuma ya Berko na Shaaban Kado, alimchezea rafu nyingine Okwi na Simba ikapata penalti ya tatu jana na Mafisango akafunga bao la tano na kuamsha shamra shamra za aina yake kwa Wana Msimbazi.  

MATATIZO YA YANGA
Lakini msiba ulikuwa kwa mahasimu wao Jangwani ambao migogoro ya kiuongozi iliiandama klabu yao ya Yanga iliyouanza msimu vibaya kwa kukaa mkiani kwa takribani raundi tano za kwanza kabla ya kufufuka baadaye na kuamsha matumaini ya kutetea taji lao.

Matatizo ya Yanga yalianza baada ya timu hiyo kufungwa na Azam katika mechi iliyotawaliwa na vurugu za kupiga refa na kusababisha wachezaji wa timu hiyo ya Jangwani kufungiwa mechi kadhaa.

Adhabu ya kukatwa pointi 3 walizopata katika ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Coastal Union ugenini Tanga kutokana na makosa yao ya kumchezesha beki Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyekuwa amefungiwa, ilionekana kuvuruga kabisa mwelekeo wa klabu hiyo ambayo ilifuatiwa na kufungwa mechi mbili mfululizo dhidi ya Toto African na Kagera Sugar.  

Huku Wazee wa Yanga wakionekana kuwa na kinyongo na uongozi wa mwenyekiti Lloyd Nchunga, ambaye amezungukwa na shinikizo la kumtaka ajiuzulu, Yanga iliingia uwanjani jana bila ya kocha wake mkuu Mserbia Kostadin Papic, aliyekaa jukwaani, ambaye alikaririwa akisema kwamba anadai malimbikizo ya mshahara wake na kwamba mkataba wake umemalizika, jambo ambalo uongozi wa klabu hiyo ulikanusha ukidai kwamba mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu.

Baada ya kipigo hicho, hali ilitarajiwa kuwa mbaya zaidi katika klabu hiyo ambayo jana iliongozwa na kocha msaidizi Fred Minziro.

MILOVAN CIRKOVIC
Baada ya kukabidhiwa kombe lao, Mserbia Milovan Cirkovic, kocha wa Simba ambayo ndiyo timu pekee iliyobaki katika michuano ya kimataifa, alisema Simba ilistahili ubingwa kwa sababu ndio timu bora msimu huu.

Aliisifu Yanga kuwa ilicheza vizuri hasa kipindi cha pili licha ya kwamba ndicho kipindi ilichofungwa magoli manne na akasema ni timu nzuri ukilinganisha na timu nyingine walizokutana nazo katika Ligi Kuu.

Matokeo mengine katika mechi za siku ya mwisho wa msimu jana yalikuwa: African Lyon 2-0 JKT Ruvu, JKT Oljoro 1-0 Polisi Dodoma, Coastal Union 1-0 Toto African, Mtibwa 1-0 Moro United, Azam 2-1 Kagera Sugar.

Kwa matokeo hayo, Simba itaiwakilisha nchi katika michuano ya Klabu Bingwa msimu ujao, Azam itacheza Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza, wakati ......................................... iliungana na timu za Moro United na Polisi Dodoma kushuka daraja.

Vikosi vilikuwa; Simba: Juma Kaseja, Nassor Masoud 'Chollo', Amir Maftah, Shomary Kapombe,  Kevin Yondan, Patrick Mafisango/ Obadia Mungusa (dk. 74), Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto/ Jonas Mkude (dk.47), Felix Sunzu/ Edward Christopher (dk.79), Haruna Moshi 'Boban' na Emmanuel Okwi.

Yanga: Yaw Berko/ Said Mohammed (dk.46), Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Athumani Iddi 'Chuji', Juma Seif 'Kijiko', Shamte Ally, Haruna Niyonzima, Davis Mwape/ Davies Mwape (dk. 46), Keneth Asamoah na Khamis Kiiza.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles