Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Upo wapi udhamini wa Taifa Stars?

2nd June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Timu ya taifa, Taifa Stars, ilitangaziwa hivi karibuni, kuwa ilipata udhamini mara tatu ya ule wa awali uliokuwa chini ya Kampuni ya Bia ya Serengeti, SBL.

Katika udhamini huo wa Kampuni ya Bia, TBL, ambao kama ulivyokuwa wa SBL vipengele vyake havijawekwa wazi kwa wadau wa soka japo unaihusu timu ya taifa, ilielezwa kuwa pamoja na mambo mengine:

Umejikita katika kuboresha yaliyokuwa yakitolewa kwa timu hiyo ambayo leo inatupa karata yake ya kwanza katika michuano ya awali ya Kombe la Dunia kanda ya Afrika kwa kucheza na Ivory Coast, katika mechi ya Kundi C.

Tunasubiri kwa hamu kuona basi kubwa la kisasa ambalo Nipashe hatuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuwa halitapatikana kweli, pengine, baadaye mwaka huu.

Kulitolewa ahadi nyingine nyingi pia ambazo si kusudio la letu leo kuzirudia hasa ikizingatiwa kuwa mkataba kati ya TBL na shirikisho la soka, TFF, ndiyo kwanza umeanza.

Lakini pamoja na uchanga wa ushirikiano baina ya TFF na TBL, tungependa kuchukua fursa hii kueleza wasiwasi wetu kuwa upande mmoja umeanza kutumika kikamilifu huku upande wa pili ukiwa unafanya majukumu yake kwa kiwango cha zamani.

Tayari wachezaji wa Taifa Stars waliondoka nchini wakiitangazia TBL vifuani, mtindo kama ule uliokuwa ukitumiwa na SBL na mshirika wake NMB wakati wakiwa wadhamini wakubwa wa timu ya taifa.

Tulitaraji kwamba hiki kilikuwa kipindi cha wachezaji wa Taifa Stars kusafiri wakiwa katika nguo ambazo wakuu wa misafara ya timu hiyo na maofisa wake wangependa kuvaa..suti za vitambaa.

Hivyo woga ulitushika baada ya kuona wachezaji wetu wakiondoka uwanja wa Julius Nyerere wakiwa wamevaa fulana zenye tangazo la biashara kifuani.

Na woga ulizidi baada ya kuona ni fulana za 'chata' ile ile ambayo ilitumika tangu enzi za kusaka tiketi ya kucheza Ghana 2008 badala ya Adidas iliyoahidiwa wakati wa uzinduzi wa mkataba huo.

'Chata' ya zamani imeendelea kutumika pia katika jezi za mazoezi ya timu ikiwa nyumbani, kwenye msiba wa marehemu Patrick Mafisango wa Simba na hata ugenini kama ambavyo picha za mazoezi ya Stars ya juzi, tulizo nazo, zinavyoonyesha.

Aidha, tulitaraji, kwamba kutokana na udhamini mpya kudaiwa kuwa wa sh. bilioni 3 kwa mwaka, wachezaji wetu wangeondoka nchini wakiwa wamebeba masanduku japo madogo-madogo ya kisasa.

Kila mtu anaweza kuwa na staili yake ya kupakia mizingo ya kusafiri nayo, hatukatai, lakini tuna hakika kuwa mabegi ya kubeba begani kama ya safari za mikoani za mabasi hayana hadhi ya kubebwa na 'jeshi' lenye udhamini wa sh. bilioni 3 kwa mwaka linalokwenda kutetea bendera na hadhi ya nchi yetu kimataifa.

Tuna hakika kuwa mabegi ya kubeba begani kama ya safari za mikoani za mabasi hayana hadhi kwa sababu tuna hakika wadhamini wenyewe, kwa mfano, wasingeyabeba kama wangekuwa wanasafiri wao kikazi kwenda nje ya nchi. 

Aidha, palikuwa na madai kuwa timu ingeweka kambi katika hoteli ya nyota tatu.

Lakini hatuna uhakika, kama hoteli iliyo kandokando kabisa ya moja ya barabara kuu za jijini Dar es Salaam, hoteli isiyo na eneo la maegesho mbele ya jengo lenyewe na hoteli iliyo katika eneo lililokuwa likionekana Uswahilini wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika, kama ni hoteli ya hadhi ya nyota tatu.

Inaweza kuwa ni hoteli ya nyota tatu kweli kwa mujibu wa takwimu zilizopo nchini, hilo tusingependa kulisisitiza sana.

Lakini ilikuwa ni matarajio yetu, Nipashe, kwamba Stars sasa ingehamisha kambi katika hoteli kama hizo na kuwekwa katika mahoteli yenye 'mizizi' ya kimataifa ambayo yamejaa jijini siyo tu ikae katika hoteli ya nyota tatu bali wadau waone kweli imepiga kambi katika hoteli za nyota tatu.

Pengine TFF haikuwa imeliona hili.Ni mapendekezo yetu basi, kwamba, kwa sababu wachezaji wa timu yetu wameshaanza kutangaza kikamilifu bidhaa ya mdhamini, wakati umepita kwa mdhamini naye kubanwa mabavu ili atekeleze japo yale ambayo yaliwekwa wazi katika siku ya uzinduzi wa mkataba wenyewe.

Tutabaki tukijiuliza upo wapi udhamini wa Taifa Stars?

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment