Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Polisi, watawala Pwani tupeni macho Ikwiriri

22nd May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Kwa kitambo sasa ndani ya nchi hii kumekuwa na matukio ya mapambano baina ya wakulima na wafugaji, ugomvi wao siyo wa kitu kingine ila wa ardhi.

Tunasema ni wa ardhi kwa  sababu wakati wakulima wanahitaji maeneo ya kuendesha shughuli za kilimo, wafugaji nao wanahitaji ya kulisha mifugo yao.

Katika utekelezaji wa majukumu ya kila kundi kati ya haya, hutokea mifugo ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya kulishwa kwenye mashamba ya wakulima, hali ambayo huamsha mapambano baina ya makundi hayo; aghalab vifo vimekuwa ni matokeo ya ugomvi wa aina hii.

Mwishoni mwa wiki wilayani Rufiji yalitokea mapambano ya watu wanaodaiwa kuwa ni wakulima wakipinga kuuawa kwa mwenzao katika ugomvi na wafugaji. Mtu mmoja aliuawa baada ya kutokea mapigano kati yake na wafugaji waliokuwa wanalisha mifugo katika shamba lake.

Habari zinasema kuwa kijana mmoja mwenye umri wa miaka 12 amefikishwa mahakamani mjini Ikwiriri akikabiliwa na shikata la kusababisha kifo cha mkulima huyo.

Ingawa ugomvi huu umevalishwa sura ya mapambano baina ya wakulima na wafugaji, ulichukua sura tofauti kabisa; maduka kuporwa, majumba kuchomwa moto zikiwamo nyumba za askari polisi; kufungwa kwa  barabara kuu inayokwenda Lindi na Mtwara, kuchinjwa kwa mifugo, uvamizi huo ukionyesha kuwa umelenga kundi fulani katika jamii, kwa kisingizio cha kulipiza kisasi.

Vyombo vya uslama na uongozi wa mkoa wa Pwani umejitahidi kufafanua kuwa vurugu zilizojitokeza mjini Ikwiriri juzi siyo mapigano baina ya wakulima na wafugaji, ila ni watu wanaotumia hali iliyotokea ya kuuawa kwa mkulima huyo, kuendesha uhalifu ambao hauna mguso wa moja kwa moja na hali hiyo; kwa kifupi, walioendesha vurugu hizo juzi walitumia kisingizio cha migogoro baina ya wakulima na wafugaji kutimiza malengo yao.

Tunajua kwamba wapo watu kwa makumi wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kutokana na kadhia hii; wapo walioshitakiwa kwa ujambazi, uporaji na kufunga barabara vitendo vinavyoelezwa kutokuwa na uhusiano wowote na ugomvi wa kugombea ardhi.

Tunaamini huko mahakamani haki itatendeka, ni matarajio yetu kuwa katika uendeshaji wa kesi hizi, kwanza ya mauaji na hizi za ujambazi na ufungaji wa barabara zitasaidia kujua kwa kina kuna nini hasa Ikwiriri hadi wananchi wafikie hatua za kuchukua hatua kama hizo, je,  ni tukio la juzi za kuuawa kwa mkulima tu, au ni mlolongo wa matukio ya huko nyuma ambayo hayajapatiwa ufumbuzi kiasi kwamba sasa yamepata mwanya wa kutoka katika sura iliyoshuhudiwa juzi?

Sisi daima tunaamini katika njia za amani za kutatua matatizo katika jamii, siyo utamaduni wala sera yetu kuchochea vurugu, chuki na wanananchi kujichukulia sheria mkononi hata kama watakuwa wamekwazwa kwa kiwango gani.

Vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwetu sisi tunaviona ni sawa kabisa na uhalifu wa aina nyingine katika jamii, havivumiliki.

Pamoja na kutambua ukweli huu na kwa kweli tukilaani kwa nguvu zetu zote mchezo huu wa hatari wa kujichukulia sheria mkononi, iwe ni kwa kikundi cha watu, au hata mtu mmoja mmoja, tunasema kuwa Ikwiriri kuna shida.

Hapana shaka shida hii ni ya kiutawala na kiuongozi zaidi. Tunapata hisia kuwa kwa muda mrefu wananchi wa Ikwiriri ama wamepoteza matumaini kutokana na vyombo vyenye mamlaka ama kushindwa kuchukua hatua stahiki kwa wakati kuondoa kero ambazo zimewakabili kwa kitambo sasa, au wenyewe wameonekana kuwa sehemu ya matatizo hayo.

Tunapata shida kusadiki kwamba wananchi wanaweza tu kulipuka kwa kiwango kilichoshuhudiwa Ikwiriri, yaani kuchomwa kwa nyumba ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), kuchomwa kwa nyumba ya Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Tarafa (OCS), kuchoma maduka na kupora vitu vingi tu, lakini pia kufunga barabara kama kuna kichocheo ambacho kimekuwa ndani yao kwa kitambo sasa.

Kumekuwa na malalamiko mengi sana kutoka Ikwiriri juu ya uhasama baina ya wakulima na wafugaji, na kibaya kinachoelezwa katika hali hii ni vyombo vya usalama, hususani polisi ama kushindwa kuwajibika vilivyo kwa wakati au kuonekana wakiegemea upande mmoja kati ya pande zenye uhasama.

Hali hii imefanya jamii isadiki kuwa polisi wanatumiwa au wanajiruhusu kutumika kinyume kabisa cha maadili yao.

Ni kwa kutafakari hali hii tunasema kuwa pamoja na maelezo yoyote yanayoweza kutolewa na polisi na watawala wa mkoa wa Pwani juu ya vurugu za Ikwiriri, ukweli mmoja unabakia peupe, kwa nini hali hii sasa?

Kwa hivyo uchunguzi wa kina wa kiutawala unatakiwa kufanywa katika eneo hili ili kuepusha jamii na madhara kama haya ya juzi ambayo yameacha watu bila makazi. Hali hii ikomeshwe.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles