Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Waziri aeleza siku 14 za machingu

15th May 2012
Print
Comments
  Alitukanwa na kupewa pole
  Ashangaa kubebeshwa zigo lisilo lake
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, amesema siku 14 baada na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na taarifa za kamati za kudumu za Bunge kujadiliwa na wabunge zilikuwa ni ngumu kwake.

Mkuchika aliyasema hayo jana mjini Dodoma wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi ofisi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.

“Lakini niwashukuruni na wale ambao mlikuwa mnaniombea, hapa katikati palikuwa pagumu, tulikuwa tunajadili taarifa ya Mkaguzi inayoishia 2010 bungeni wakati mwaka 2010 mimi nilikuwa Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni kabla ya kupachikwa pale (Tamisemi),” alisema na kuongeza: 

“Sikutajwa kwenye taarifa ya Controller and Auditor General (CAG) kwamba mimi ni mwizi, sikutajwa na mbunge yeyote kwamba mimi ni mwizi, lakini jina limeingia.”

Alisema magazeti mengine yameandika tahariri na moja kati ya hayo lilimtaka kuachia ngazi kwa sababu CAG alimtaja kama mbadhirifu wa fedha za umma.

"Najiuliza nikusanye vitabu vya CAG na kupeleka katika magazeti yaliyonitaja kuwa mimi ni mwizi na niwatake wanionyeshe ukurasa upi umenitaja kuwa mimi ni mwizi,” alisema na kuongeza:

“Sasa nadhani hiyo ndio iliyonisababisha nipone, kwa sababu sikuwepo (wakati ubadhirifu unatokea)...Mlikuwa mnanipigia simu aha waziri pole, bungeni huko kukoje, lakini ndio siasa, na sisi tulioingia katika siasa kuna ups and down (kuna kushuka na kupanda),” alisema.

“Nilikuwa na siku 14 za hali ngumu tangu Ijumaa ile mpaka Ijumaa Rais alipotangaza baraza la mawaziri. Si mnajua nilitoa namba pale bungeni mimi Waziri wa Tamisemi mkisikia watu wanaiba nipigieni,” aliongeza.
Mkuchuka alisema alipata simu nyingi za pole, lakini pia simu za kumtukana. “Lakini pia simu za kunitukana kuwa mshenzi, kwamba siridhiki,” alisema.

AMSHUKURU JK
“Haya mambo yamepita mimi namshukuru sana Mheshimiwa Rais (Jakaya Kikwete), kwanza kuwaeleza Watanzania kwa kuniteua kushughulika na Utawala Bora. Huwezi kupeleka jambazi kwenda kushughulikia watu,” aliongeza.

“Amewajibu kwamba this man is mr clean (huyu mtu ni msafi), mimi sina biashara, sina majumba makubwa ninaishi maisha ya kawaida, pesa yangu yote niliyoipata nimeinvest (nimeiwekeza) katika kuwasomesha watoto wangu watano,” alisema Mkuchika.

Alisema anamshukuru Rais kwa kuangalia ukweli wa jambo lenyewe na kwamba ameonyesha kuwa anazidi kumuamini.

Alisema wizara aliyopewa (Utawala Bora) ni ngumu na kwamba mambo yaliyoko ndani yake atakwenda kuambiwa huko huko wizarani.

Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri wasiibe na kwamba kama wakiiba wajue wazi kuwa wizara yake ambayo ina taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), itapambana nao.

“Mnaoshikashika hela msiibe, mkiiba mnamualika Waziri Mkuchika na watu wake waje kuwachunguza," alisema na kuongeza kuwa wizara hiyo (Tamisemi) ni kubwa na kwamba wakati wote aliokaa hakuwahi kumaliza kuyapitia mafaili yote.

Alisema huwezi kuwa Waziri wa Tamisemi na ukalala saa 12.00 jioni wakati Watanzania wanataka maendeleo.

Aliwataka wafanyakazi wa wizara hiyo kushirikiana na waziri mpya ili kuwahudumia vizuri Watanzania.
Aidha, Mkuchika aliitaja changamoto kubwa katika wizara hiyo ni usimamizi wa fedha zinazopelekwa katika halmashauri.

Alisema iwapo madiwani watafanya kazi zao ipasavyo wataweza  kusimamia fedha hizo ipasavyo kwa manufaa ya taifa.

Wakati wa mjadala huo, wabunge walidai kuwa Mkuchika alishindwa kusimamia fedha katika halmashauri mbalimbali nchini ambako ufisadi wa kiwango kikubwa uligundulika.

GHASIA AWAPASHA TAMISEMI
Kwa upande wake, Waziri Ghasia alisema walikuwa pamoja na Waziri Mkuchika katika kipindi cha wiki mbili tangu Bunge lilipojadili ripoti za CAG na Kamati za Bunge, ili kujaribu kumshusha presha.

“Kwa kweli presha ilikuwa kubwa, unakaangwa kwa kitu ambacho kwa kweli hukuhusika moja kwa moja kwa vile tu ni watoto wako au kwa vile uko katika wadhifa wa kuwasimamia walioko kule chini,” alisema.

Ghasia aliwataka watumishi wa wizara hiyo kuhakikisha wanajipanga ili katika kipindi cha muda mfupi kuhakikisha kuwa lawama ambazo wamekuwa wakitupiwa na wananchi zinaondoka.

Aliwataka pia kuchukulia ripoti za CAG na kamati za Bunge kuwa ni changamoto ambazo wanatakiwa kuzitatua na kuondoka nazo.

“Tuendelee kufanya kazi vizuri na tuwabane walioko chini, tukiwabana watafanya kazi vizuri, tusipowabana watatuangusha katika viti vyetu. “Niwahakikishie kuwa tutafanya kazi pamoja kwa wale walioko tayari kufanya kazi na sisi, lakini wale ambao hawako tayari kufanya kazi na sisi kwa kweli hatutakuwa tayari tusukumwe sukumwe au tuwekwe katika vikaango ambavyo havituhusu," alisema na kuongeza:

“Nataka niwahakikishie kuwa sitamuonea mtu, kwa yule ambaye atajituma na atatekeleza majukumu yake, lakini pia sitambeba mtu ambaye hataki kutekeleza majukumu yake, kila mtu ajiweke katika nafasi ya kutekeleza majukumu yake kama unaona huwezi kufanya kazi katika kipindi hiki uondoke.”

Katika mkutano wa saba wa Bunge ulimalizika Aprili mwaka huu, mawaziri wanane waliwekwa kiti moto kutokana na ripoti ya CAG kwa mwaka wa 2009/10 kuonyesha udhaifu mkubwa wa usimamizi wa fedha.
Ripoti hiyo ilipigiwa msumari na ripoti za Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC). Pia ya Ardhi na Mazingira.

Kutokana na moto huo, Bunge lilitaka uwajibikaji kwa mawaziri hao na Kamati ya Wabunge wa CCM, ilikaa na kuwataka mawaziri hao kuachia ngazi hasa kutokana na moto kugeuzwa na kuelezwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye hoja ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye ilikuwa inaandaliwa.

Waliopoteza nafasi zao katika mabadiliko aliyofanya Rais Kikwete ni pamoja na Mustafa Mkulo (Fedha), Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Haji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Omari Nundu (Uchukuzi), William Ngeleja (Nishati na Madini), pamoja na naibu wawili, Athumani Mfutakamba (Uchukuzi) na Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii).

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment