Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Matusi ya Lusinde na hatima ya CCM

8th April 2012
Print
Comments
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde

Takribani dakika 16 za kuwepo kwake jukwaani, akimnadi aliyekuwa mgombea ubunge wa Arumeru Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sioi Sumari, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, aliporomosha matusi.

Hakuna lugha rahisi inayoweza kubeba maana ya hotuba ya Lusinde ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM zaidi ya ‘matusi ya Lusinde.’

Akiongea kwa kujigamba na ‘kujitanua’ mithili ya Mfalme aliyetoka vitani akiwa mshindi, Lusinde akajigamba kwamba ‘amezaliwa na ukichaa’ na kama ni suala la matusi, yeye ndio mwenyewe katika hilo!

Akakishambulia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akawatukana Katibu Mkuu wake, Dk Wilbrod Slaa, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kisha akatoa kejeli kwa wanawake kupitia kigezo cha kubeba mamba.

Si rahisi kuyaandika matusi ya Lusinde yanayopatikana pia kwa njia ya mtandao wa you tube kwa anwani yahttp://www.youtube.com/watch?v=1lSaLItmj-c kwa maana ni kichefuchefu, ni fedheha, ni soni, ni kila aina ya hali isiyomstahili binadamu mwenye akili timamu.

Lusinde aliyafanya hayo huku (bila shaka) akijua kwamba CCM iliyokuwa mmiliki wa majimbo yote ya uchaguzi kwa upande wa ubunge nchi nzima, miongoni mwa hayo yamechukuliwa na vyama vya upinzani.

Hilo peke yake, hata kama limefanyika katika kipindi cha mfumo wa siasa za vyama vingi, linatoa ishara ya kuwepo raia halali wa Tanzania wasioridhishwa na chama hicho kilichotokana na Tanganyika African Nation Union (TANU) na Afro Shiras Party (ASP) cha Zanzibar.

Kwamba tangu kuzaliwa kwa CCM Februari 5, 1977 hadi sasa, yapo mabadiliko na changamoto zinazokikabili chama tawala, ikiwemo kupoteza mvuto wake kwa wananchi, hivyo kufifisha nia ya kujihakikishia uwezo wa kushika dola kwa miaka kadhaa ijayo.

Katikati ya hali hiyo, anaibuka Lusinde, mmoja wa ‘vijana’ walioaminika wangeiweka CCM jimboni Arumeru Mashariki katika siasa za kisasa, kujenga hoja zenye mashiko kwa umma na kuzihubiri itikadi na ilani za chama hicho ili kipate ushindi, badala yake akakiangamiza.

Kama hotuba ya Lusinde ingetumwa na CCM kwenye runinga ili itolewe tangazo, ni dhahiri kwamba ingekuwa ni upotevu wa fedha za umma, lakini pia ingechochea kasi ya mmomonyoko wa maadili na kushuka kwa heshima ya mzazi na kiongozi wa umma.

Lakini nafsi ya Lusinde ambaye ni Mwakilishi wa wananchi wa Mtera katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, haikumsuta hata kwa sekunde moja ndani ya takribani dakika 16 alizoporomosha matusi jukwaani, kwamba alitembea njia isiyo njema!

Huyo ni Mbunge kupitia CCM, mjumbe wa Nec ya chama tawala anayepaswa kuitumia kila fursa anayoipata, ikiwemo ya jukwaa alilopanda na kuhutubia kule Arumeru Mashariki, kuzitangaza sera, ilani na itikadi ya chama hicho badala ya ‘kumwaga matusi.’

Kwa upande mwingine, unaposoma mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya jamii kupitia `intaneti’, wapo wanaohoji, hivi Lusinde alikuwa na ufahamu timilifu kuhusu kile alichokuwa anakiongea, kwamba kilimstahili?

Kuna nadharia inayoeleza kwamba, inawezekana mzazi akawa na mtoto mtukutu, anayejihusisha na uvutaji bangi, kila anapotenda kwa kadri anavyotumwa na bangi anayoivuta, mzazi anakereka.

Kwa mtoto mhusika katika uvutaji bangi, inakuwa ni jambo la kawaida. Anaweza kutukana lakini asijue kwamba ni kosa, bali jambo lililo jema tena jema sana. Hata anapozongwa na kuhojiwa, anaweza kusisitiza kwamba ‘nilichokifanya ni chema, mniache nilivyo’

Sitaki nikifananishe kisa cha Lusinde na mtoto mtukutu anayetajwa kupitia nadharia hiyo, lakini bado kuna haja ya kujiuliza, CCM ikiwa mfano wa mzazi wa Lusinde, ilifurahishwa ama kukerwa na matusi yake?

Umma wa Watanzania wanaoweza kutajwa kama majirani wa CCM, walimshuhudia Lusinde akitema matusi yaliyotoka kupitia kinywa safi kilichoumbwa kwa ajili ya yaliyo mema, ukakereka. Nafsi ya Lusinde inatuma wapi katika hilo?

Tayari Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, ‘ameshamkingia kifua’ Lusinde, kwamba alichokifanya kilikuwa kujibu mapigo dhidi ya upinzani.

Kwa vile Mukama ni Mtendaji Mkuu katika CCM, ni sawa na kusema kwa chama hicho, ni heri ya mtu anayekoga bafuni, kisha akapita kichaa aliye uchi akakwapua taulo lililotundikwa juu mlangoni, yule anayekoga akatoka (akiwa uchi) na kumfukuza kichaa ili ampe taulo lake!

CCM inapiga wapi mstari kutofautisha matusi ya Chadema na wajibu wake kwa umma, kikitambua kuwa kupitia ilani ya uchaguzi, sera, mikakati na mipango inayotekelezwa na serikali yake, umma unategemea maisha bora kwa kila Mtanzania?

Inapotokea Mbunge wa CCM kuporomosha matusi, yakaungwa mkono na Katibu Mkuu wake, hatma ya chama hicho katika nafasi ya utawala inakuwaje?

CCM ina safari ndefu ya kujichunguza, kama alichokinena Lusinde kikaungwa mkono na Mukama, basi sioni soni kuamini kwamba chama hicho kinazidi kupotea njia, kinatoka nje ya mstari wa utawala hivyo kuzidi kufifisha imani ya wananchi kwao.

CCM na serikali yake wana mambo yake ya kuuelezea umma, wana hoja nyingi za kuhalalisha utawala wake, wana majawabu mengi ya kuelezea mafanikio ya kuwepo kwao madarakani.

CCM na serikali yake wana mambo mengi ya kuhutubia kuhusu dira ya kuharakisha maendeleo ya nchi kitaifa, kupitia uanachama wa kikanda na ushirikiano wa kimataifa. Wakishindwa kuzitumia fursa wanazozipata, badala yake wakajikita kwenye matusi kama alivyofanya Lusinde, watakuwa wanajimaliza.

Shauri yao!

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE.Anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe:mgeta2000@yahoo.com.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment