


.jpg)
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana iliahirisha kesi ya mashitaka manane yakiwemo ya matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) Ltd, hasara ya Sh. bilioni 2.4 bilioni inayomkabili Mwenyekiti wa Bodi wa shirika hilo, Iddi Simba na wenzake wawili hadi Julai 19, mwaka huu.
Mbali na Simba ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, washtakiwa wengine ni Meneja Mkuu wa Uda, Victor Milanzi na Mkurugenzi wake, Salim Mwaking’inda.
Mwendesha Mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mariagoreth Richard, alidai kuwa kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ambapo washtakiwa wangesomewa maelezo ya awali.
Kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi Faisal Kahamba, kutokana na mshtakiwa Mwaking’inda kufiwa na mwanawe.
Awali, ilidaiwa kuwa kati ya Septemba 9 na Februari 11, mwaka 2011, washtakiwa hao wakitekeleza majukumu yao, walitumia vibaya madaraka yao kwa kugawanya hisa 7,880,330 zisizotumika za UDA.
Ilidaiwa kuwa, Septemba 2, mwaka 2009 jijini Dar es Salaam, Simba na Milanzi, walikula njama ya kuchepusha fedha kinyume na Kifungu cha 29 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 11 ya 2007.
Pia ilidaiwa kuwa Simba na Milanzi walighushi barua wakionyesha kuwapo kwa kiwango zaidi cha fedha kwenye akaunti zote za benki za Uda.
Aliongeza kuwa siku hiyo hiyo, Simba na Milanzi kwa pamoja, walichepusha Sh. milioni 320 wakijifanya ni malipo ya awali ya mauzo ya hisa katika shirika hilo fedha ambazo walijipatia kutokana na nyadhifa zao.
Aidha, kati ya Septemba 3, mwaka 2009 na Machi 31, mwaka 2010, Simba na Milanzi, wanadaiwa kujipatia Sh. milioni 320 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Robert Kisena, wakijifanya ni sehemu ya malipo ya hisa za Uda.
Lincoln alidai kuwa washtakiwa Simba na Mwaking’inda, kati ya Septemba 2009 na Februari 2011, wakati wakitekeleza majukumu yao, kwa makusudi walitumia vibaya nafasi zao waliharibu hisa 7,880,330 zisizotumika za Uda ambalo ni shirika linalomilikiwa kati ya Serikali Kuu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Hisa hizo zinakadiriwa kuwa na thamani ya Sh.1,142,643,935.
Washtakiwa wote wako nje kwa dhamana.