Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Sheria kuwatambua wanasheria wasiosomea kuanzishwa

19th May 2012
Print
Comments
Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kairuki

Serikali iko mbioni kutunga sheria ya kuwatambua na kuwasimamia wanasheria wasiosomea  (paralegals) ili waweze kuwapa msaada wa kisheria watanzania wengi hasa wa maeneo ya vijijini.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kairuki, wakati akizindua rasmi mfuko  maalum wa kusaidia huduma za kisheria (LSF).

Alisema kwa kuwatambua watu hao, watanzania wengi hasa waishio maeneo ya vijijini watakuwa wakipata haki pindi wanapokwenda mahakamani kwani wengi wa wanasheria wasiosomea wanapatikana vijijini.

Alisema watanzania wengi hasa maskini hawawezi kumudu gharama za kusimamisha mawakili kwenye mashauri yao kutokana na bei kubwa hivyo wanasheria wasiosomea ni msaada mkubwa sana kwao.

“Serikali kwa kutaka kuhakikisha watanzania wengi hasa maskini wanapata haki Tume ya Kurekebisha sheria ilifanya utafiti wa kutosha kuhusu namna hawa wanasheria wasiosomea wanavyoweza kutumika kutoa msaada wa kisheria ikiwemo kuwawakilisha watu mahakamani, Tume imeshakabidhi ripoti yake kwa serikali na inafanyiwa kazi,” alisema.

Alisema serikali inayashukuru na kuyatambua mashirika yasiyo ya kiserikali kwani yamekuwa yakitoa msaada mkubwa kwa upatikanaji wa haki hasa kwa wananchi wasio na uwezo wa kuweka mawakili kwenye kesi zao.

“Tunatambua mchango wa asasi binafsi katika kutoa msaada wa kisheria, mnafanya kazi kubwa sana katika jamii yetu na nawaomba mwendelee na moyo huo huo, watu wengi wasio na uwezo kama yatima, walemavu, wajane wamekuwa wakiwategemea nyingi, natambua si kazi rahisi kutokana na uwezo mdogo wa kifedha mlionao lakini msikate tama,” alisema Kairuki.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo, Joaquine De Mello, alisema mfuko huo ni maalum kwa ajili ya kutoa fedha kwa asasi zinazotoa msaada wa kisheria Tanzania Bara na Visiwani.

Alisema asasi hizo ni zile zinazosaidia wananchi kupata haki zao na kulinda haki za wananchi pale zinapotaka kukiukwa na watu wenye maslahi binafsi.

Mwenyekiti huyo alitaja malengo ya mfuko huo kuwa ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki walizonazo kwa mujibu wa sheria, kuongeza wigo wa utoaji wa sheria, kubadili fikra na mtazamo wa watoa msaada wa sheria na kuimarisha mijadala ya ushawishi kuhusu masuala ya utoaji wa msaada wa sheria.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles