Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Askofu Malasusa: Katoeni maoni ya Katiba

30th April 2012
Print
Comments
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa

Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi kutoa mchango wao wa maoni kwenye Tume ya  ya Katiba, inayotarajiwa kuanza rasmi kazi ya kukusanya maoni kesho katika  mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya.

Rai hiyo ilitolewa jana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, jijini Dar es Salaam, kwenye ibada ya kuliweka wakfu jengo la kitega uchumi la Usharika wa Kijitonyama.

“Tumemaliza mkutano wa Halmashauri Kuu, na kati ya mambo tuliyoyazungumzia ni pamoja na kuwataka wananchi washiriki kikamilifu kwenye kutoa maoni yao kwenye mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya,” alisema Askofu Malasusa ambaye pia ni Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Alisema kuna mambo mengi yanayowafanya Watanzania wasipige hatua, hivyo inawapasa wote kujadiliana, na kuyaangalia kwa umakini mambo ambayo hayatawagawa, kwa kuwa Katiba ni ya Watanzania wote na wala siyo ya madhehebu ya dini.

“Inatupasa tuangalie madaraka mbalimbali yaliyowekwa katika Katiba hii ambayo yaliwekwa wakati huo, inawezekana Katiba ilikuwa nzuri wakati huo wa wazee wetu, lakini kwa sasa changamoto ni nyingi, na Katiba itatuletea amani ambayo tumekuwa tukiiombea kila wakati,” alisema.

Tume ya kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya inaongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Malasusa aliwataka Watanzania kutokuwa watu wa kulaumu tu baada ya mambo kutokea, bali wajitokeze na kushiriki  katika mambo ya msingi yanayoihusu nchi yao, na alionyesha kushangazwa kwake na idadi ndogo ya watu wanaojitokeza katika kupiga kura.

“Katika mambo yanayonishangaza ni idadi ya watu wanaojitokeza kupiga kura,” alisema na kuhoji:  “Kwa nini watu hawajitokezi?”.

Askofu Malasusa aliongeza kuwa, kuna mambo mengi yanayojitokeza na kusababisha watu wengi wasipige kura, lakini kitendo cha vijana wengi kutojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura  ni tatizo.

Aidha, Askofu Malasusa, alisema ni vizuri kwa Watanzania kuzitumia vizuri siku zilizotolewa ili kujiandaa na kushiriki vyema katika zoezi hilo, ili watu wote wapate haki yao ya msingi ya kupiga kura, na kusiwepo na kitu chochote kinachoashiria au kusababisha mtu yoyote anyimwe uhuru huo.

“Nchi yetu  imekuwa ni ya maneno mengi bila kuchukua hatua, tunawaomba wachungaji wetu muwaambie waumini wenu,  umuhimu wa kushiriki katika mchakato wa katiba mpya pamoja na kupiga kura,” alisema.

Kiongozi huyo wa kanisa pia alisisitiza kwamba Watanzania wasiruhusu kupitishwa kwa mambo mengine kama vile ushoga na uchafuzi wa mazingira kwa mgongo wa haki za binadamu.

Kadhalika, Dk. Malasusa, alishangazwa na tofauti ya kipato iliyopo kati ya maskini na matajiri ambayo alisema inatisha sana, kwani matajiri wanazidi kutajirika na maskini wanazidi kuwa mafukara.

Awali akimkaribisha Askofu Malasusa kwenye uzindizi wa jengo hilo, Mwenyekiti wa kamati ya kitega uchumi wa cha kanisa hilo, Sanyiel Kishimbo, alisema kuwa jengo hilo lenye ghorofa tisa limegharimu Sh. bilioni 3.5, na litatumika kwa matumizi ya ofisi, chuo pamoja na shule ya watoto.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment