Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

JK amekosea kumuacha Profesa Lipumba, Dk. Slaa

6th May 2012
Print
Comments

Alhamisi wiki hii, Rais Jakaya Kikwete, alimteua Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Profesa Sospeter Muhongo na Janet Mbene, kuwa wabunge.

Kisha siku iliyofuata, Rais Kikwete akamtangaza Saada Mkuya Salum kuwa Mbunge anayetimiza idadi ya walioteuliwa ndani ya siku mbili kufikia wanne.

 Uteuzi huo wa Rais Kikwete umefanyika takriban miaka miwili tangu afanye hivyo mwaka juzi.

 Katika uteuzi wa mwaka juzi, Rais Kikwete alimteua Shamsi Vuai Nahodha, kuwa mbunge. Nahodha kwa sasa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

 Wengine walioteuliwa na Rais Kikwete mwaka huo, ni Profesa Makame Mnyaa Mbarawa ambaye ni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji.

 Uteuzi huo unatimiza idadi ya majina saba katika nafasi 10 za ubunge anazopewa Rais kuteua kikatiba.

 Kama kawaida, uteuzi wowote unaofanywa hupokewa na watu kwa hisia tofauti. Kuna watakaounga mkono, lakini wapo pia watakaopinga kwa hoja, vigezo na sababu.

 Hata hivyo, vyovyote  itakavyohisiwa, Rais Kikwete amekwishafanya uteuzi wake kwa kutumia mamlaka aliyonayo Kikatiba na kwa sababu na kwa vigezo vyake.

 Pamoja na ukweli huo, siku zote waungwana kukumbushana ni wajibu.

 Lipo suala la kuangalia mahitaji ya wananchi, wakati na rekodi za wateuliwa katika kufikia maamuzi ya kufanya uteuzi wa viongozi, watendaji au wawakilishi.

 Rekodi inahusisha mteuliwa kuwa na uwezo wa kuibua hoja, kuichambua na kuwa na mchango uliosaidia katika maendeleo ya taifa.

 Kwa kuangalia vigezo hivyo peke yake, kumuacha Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba au Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, katika uteuzi wa ubunge, nionavyo mimi ni kosa kubwa sana.

 Kwa mfano, hivi sasa nchi ina mipango na mikakati mingi ya kiuchumi.  

Ni hivi majuzi tu (Juni 7, mwaka jana), Rais Kikwete ametoka kuzindua Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) wa Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Lakini ipo pia mipango na mikakati mingine ya kitaifa ya kiuchumi. Hiyo ni pamoja na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (Mkukuta), Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar (Mkuza) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita). 

Yote hiyo ni kwa ajili ya kuliwezesha taifa kupiga hatua ya maendeleo. Hata hivyo, wananchi wengi wanaiona kama ni lugha ambayo haijapata mkalimani.

Mipango na mikakati hiyo ikijaa tele, nchi bado inakabiliwa na hali ngumu ya maisha. Mfumuko wa bei hausemeki. Kilichokuwa kikiuzwa Shilingi 500 miaka mitatu iliyopita, hivi sasa kinauzwa hadi Shilingi 2,000!

 Shilingi imeota mbawa. Kuipata ni taabu. Na hata ukiipata haikufikishi popote. Kila mtu amechacha!

 Wakati hali ikiwa hivyo, nchi imebahatika kutunukiwa na mweledi mkubwa na bingwa wa uchumi anayeheshimika kitaifa na kimataifa, Profesa Lipumba.

 Angalau Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, enzi za uongozi wake, aliwahi kumpa nafasi. Alimtumia kufufua uchumi ulioonekana kudidimia. Matokeo, neema ikashamiri nchini.

 Ule utaratibu wa kupata robo kilo ya unga wa dona wa njano kwa kupanga foleni kutwa nzima au hadi hapo mtendaji wa kijiji au mtaa atakapoamua kufungua duka la ushirika, kuanzia hapo ukabaki kuwa historia.

 Naamini uteuzi wa Profesa Lipumba kuwa mbunge, ungetoa mchango mkubwa sana bungeni. Kwa kutumia taaluma yake, angeweza kusaidia kuchambua bajeti, Bunge likapitisha bajeti nzuri yenye kuleta neema kwa Watanzania.

 Kwanini mtu huyu asitumiwe? Je, ni busara kumuacha, tuendelee kuishia kumsikia redioni na kwenye televisheni akisaidia kutibu uchumi wa nje ya nchi, kama Ulaya na Marekani?

 Pili, angalau hivi sasa Rais Kikwete na serikali yake wananufaika na matunda ya jasho la harakati zilizofanywa na Dk. Slaa katika Bunge la Tisa chini ya Spika Samuel Sitta.

 Kupitia Bunge hilo, Dk. Slaa amekuwa na mchango mkubwa. Aliweza kuibua hoja nzito na kufichua ufisadi mwingi na mkubwa wa kuifilisi nchi, ukiwamo ule uliohusisha ukwapuaji wa zaidi ya Sh. bilioni 133 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Rais amechukua hatua, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani baadhi ya watuhumiwa, wakiwamo waliokuwa mawaziri.

 Ufike wakati tuangalie katika kufanya maamuzi, kwani kuna watu taifa linawahitaji.

 Muhibu Said ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE. Simu: 0717055551 au 0755925656. Baruapepe: [email protected]

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles