Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

CCM imepoteza nguvu ya udhibiti

25th April 2012
Print
Comments

NI sahihi kuamini kwamba kasi ya viongozi na wanawachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhamia upinzani hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inaongezeka.

Kitendo cha wana-CCM kukikimbia chama hicho kilichoanzishwa Februari 5, 1977 hakijaanza kwenye uongozi Rais Jakaya Kikwete. Ni muendelezo uliokuwepo husasun baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Itakumbukwa kwamba wakati wa ukoloni, Tanganyika na Zanzibar zilizoungana Aprili 26, 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilikuwa katika mfumo wa vyama vingi.

Hata Tanganyika na Zanzibar zilipoungana kuiunda Tanzania iliyopo, vyama vingi vikiwa na sera, dira, malengo na mwelekeo tofauti, vilikuwepo katika pande mbili hizo.

Mwaka mmoja baada ya Muungano, yaani 1965, mfumo wa vyama vingi ‘uliuawa’ kwa mujibu wa sheria, ikiaminishwa kwamba vilishindwa kutekeleza wajibu wake kwa umma.

Hapo Tanzania ikaendelea kuwa yenye mfumo wa chama kimoja cha siasa, hadi ilipofika 1992, hali ikabadilika na kuruhusiwa (kwa mujibu wa sheria) kuanzishwa vyama vingi vya siasa.

Kuanzishwa kwa mfumo huo kuliwafanya viongozi na wanachama wengi wa CCM hasa waliokuwa wanasigana ndani yake kuhusu namna tofauti za uendeshaji na utekelezaji wa majukumu yake, walijiengua na kujiunga ama kuanzisha vyama vya siasa.

Hapo utaona kwamba sehemu kubwa ya walio katika upinzani walitoka CCM. Wakifuata sheria, taratibu na kanuni zilizohalalisha uwepo na utendaji kazi wa vyama hivyo.

Kwa hali hiyo, wimbi la viongozi na wanachama wa CCM wanaokikimbia chama hicho na kujiunga Chadema si la kwanza, lakini kwa namna ya pekee, linafanyika katika taswira inayoonyesha mwelekeo hasi wa chama tawala.

Ikumbukwe pia kwamba hata mwaka 1992 baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, viongozi na wanachama mahiri wa CCM, wakiongozwa na aliyewahi kuwa Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana ya Vijana, Augustine Mrema.

Mrema alijiengua CCM na kujiunga NCCR-Mageuzi, hali iliyoonekana kama ‘tsunami’ kwa chama tawala. Mrema hakukaa sana NCCR-Mageuzi kutokana na mgogoro mkubwa wa kisiasa uliobuka ndani ya chama hicho.

NCCR-Mageuzi ikameguka makundi mawili, moja likimuunga mkono Mrema na jingine likiwa upande wa aliyekuwa Katibu Mkuu, Mabere Nyaucho Marando.

Hatimaye Mrema ‘alibwaga manyanga’ akakimbilia TLP, huko pia alifuata na watu ingawa kwa uchache ikilinganishwa na alipotoka CCM na kujiunga NCCR-Mageuzi.

Wimbi la wana-CCM kukihama chama hicho lilikuwa upande wa Zanzibar, wengi wao wakijiunga Chama cha Wananchi (CUF), wakakipa nguvu zaidi na sasa kimebaki kuwa kinara wa upinzani visiwani humo.

Wimbi la kuelekea Chadema

Je, hatua ya wana-CCM kuhamia Chadema hivi sasa, ina maana gani kwa uhai wa chama tawala?

Tangu kundoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoa wa Arusha, James Ole Millya kujiunga Chadema, moto huo umesambaa maeneo mengine nchini.

Millya ameondoka na sasa madiwani na wanachama wengine katika maeneo tofauti ya nchi, wanajiengua.

Jambo lililo miongoni mwa yenye msingi wa tofauti kati ya kuhama kulikotokea awali na sasa, ni kwamba CCM ya sasa imegawanyika. Ni chama kimoja chenye makundi mengi yakiwa na malengo na matamanio yanayotofautiana.

Hivyo wanapotokea wanachama wanahama, CCM inakosa uhalali wa kubuni mkakati wa pamoja wa kuwarejesha ama kukomesha hali hiyo. Kwa maana inategemea zaidi mtu ama ofisi inayopaswa kuidhibiti hali hiyo.

Mwenye mamlaka hayo anaweza kuwaona walioondoka na wanaoendelea kuondoka ‘si watu wetu’ bali watu wa kundi lile. Kuondoka kwao kunakuwa faida kwa kundi lake kwa maana ‘kundi adui’ ndani ya chama ndilo limepata pigo.

Upepo wa mageuzi


Mabadiliko ya upepo wa kisiasa yanayoifanya CCM izidi kupoteza udhibiti wa wanachama na viongozi wake, ni miongoni mwa sababu ya kukua kwa wimbi la kukihama chama hicho na kukimbilia Chadema.

Ikumbukwe kwamba awali, kulikuwa na dhana potofu kwamba mafanikio yoyote ya kisiasa hayawezi kupatikana isipokuwa kupitia CCM.
Dhana hiyo ilisakafiwa na matumizi ya nguvu za dola, vitisho na hujumu dhidi ya haki za kidekrasia, kuwafanya watu wabaki ndani ya CCM hata kama hawakipendi chama hicho, hawaguswi na sera ama uongozi wake.

Hapo ndipo yanapokumbukwa matukio kama ya waraka wa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Laurence Gama, alipoandika akitaka majina ya watu waliosaidia upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa 1995 ili washughulikiwe.

Kama vile haikutosha, aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Tluway Sumaye, akimkampenia aliyekuwa mgombea ubunge wa Moshi Vijijini (CCM), Elizabeth Minde, akatangaza kuwa mtu yeyote anayetaka mambo yake yamnyookee, atundike bendera ya CCM.

Wafanyabiashara tofauti zikiwemo za nyumba za wageni, baa, migahawa ya chakula hata kama ziliendeshwa kinyume cha sheria, kanuni na taratibu, walitundika bendera za CCM!

Wasafirishaji kwa njia za barabara na majini, hata kama walibeba bidhaa haramu na zinazohujumu uchumi ama kuhatarisha amani na usalama nchini, walipeperusha bendera za CCM, hawakukuguswa.

Kwa sababu Waziri Mkuu alishantangaza, kwamba anayetaka mambo yake yamnyokee, apeperushe bendera ya CCM.

Lakini hiyo haikuwa katika kuiimarisha CCM, ilikiangamiza chama hicho kwa maana kila jambo ovu na lenye nia ovu, lilifanyika kupitia mgongo wa CCM.

Pengine hata kuimarisha kwa kundi la mafisadi waliojipenyeza hadi ndani ya Baraza la Mawaziri, ni matokeo ya mfululizo wa vitendo hasi vya viongozi wa CCM na serikali.

Hapo ndipo kinapotokea chama mbadala kama Chadema, kikazungumza lugha ya Watanzania, kikawaunganisha Watanzania, kikakemea wanaowahujumu Watanzania na kuahidi kuipigania Tanzania huru itakayowanufaisha Watanzania wote, kinaaminika kwa urahisi.

Ndio maana unapoisoma historia ya mageuzi nchini, Chadema ni chama pekee cha upinzani upande wa Tanzania Bara ambapo mafanikio yake yamekuwa yakiongezeka mwaka baada ya mwaka.

Wameongezeka kwa idadi ya viongozi wa serikali katika ngazi za vitongoji, vijiji na mitaa, wameongezeka kwa viti vya madiwani na ubunge, wameongezeka kwa kuaminiwa na wananchi, wameongezeka kwa ushawishi unaougusa umma mpana.

Hali hiyo umebomoa uwezo wa CCM kuhodhi na kuudhibiti umma, kwamba umma sasa haupo katika kuamini kwamba ili mambo yako yakunyookee, upeperushe bendera ya CCM!

Kwamba ili ushinde katika ngazi ya kitongoji, kijiji, mtaa, kata ama jimbo, lazima uwe umetokana na CCM, si hivyo tena! Kasi ya madaliko imekuwa kubwa, inaonekana kuzidi uwezo wa CCM iliyobaki katika makundi kinzani.

Inapofikia hatua hiyo, busara pekee kwa waliopewa dhamana ya umma kama wabunge na madiwani, ni kuyaelekeza macho na masikio yao kwa umma, kuutambua umma unataka nini na si chama kinataka nini.

Kama chama kinakuwa sehemu ya vikwazo katika kuyafikia matarajio ya umma, haina maana ya kuendelea kuwemo ndani yake, ndio maana wimbi la kuondoka linaongezeka, na watazidi kuondoka.


Wataondoka kama wanaotangaza kuondoka sasa, wakiwa katika nafasi mbalimbali ambazo si rahisi kuushawishi umma uamini kwamba kuhama huko ni kwa sababu ya ‘njaa zao.’

Migogoro isiyofikia ukomo

Tangu wakati na baada ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ambapo Rais Jakaya Kikwete aliingia madarakani kwa mara ya kwanza, CCM ilipata mpasuko mkubwa.

Waliokuwa wagombea, wafadhili na washauri wao, walitumia mbinu chafu ya kueneza uongozi wenye kukigawa chama hicho, ili watimize matakwa yao.

Walizusha mambo hata yasiyostahili kuzushwa, kwa maana hayakuwa na ukweli hivyo kukosa uhalali wa kimaadili, isipokuwa kukigawa na kukiangamiza chama hicho.

Mgawanyiko huo ukakua hadi kufikia hatua ya kuundwa Kamati ya Wazee, ikiwa na Mwenyekiti wake, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Abdurrahman Kinana na Pius Msekwa.

Taarifa ya kamati hiyo iliyolenga kubaini chanzo cha mgawanyiko na kupendekeza suluhu yake, haijulikani kama ilitolewa ama  imehifadhiwa kwenye makabati ya nyumbani kwa wajumbe ama ofisi za CCM.

Aidha dhana ya kujivua gamba iliyoasisiwa na Rais Jakaya Kikwete, inaendelea kuwa mwiba dhidi ya umoja na mshikamano ndani ya CCM.

Lakini yote kwa ujumla wake, CCM imepoteza nguvu ya udhibiti wa wanachama wake, imepoteza nguvu ya mvuto na kuaminika kwa wananchi, inakimbiwa na huenda ikaendelea kukimbia hasa ifikapo 2015.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles