Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Polisi watangaza kumsaka Dk. Slaa

26th April 2012
Print
Comments
Katibu Mkuu wa chama Chadema, Dk. Willibrod Slaa

Sakata la wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliocharangwa mapanga mwanzoni mwa mwezi huu limechukua sura mpya, baada ya Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kudai kuwa linamchunguza Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, na kwamba ikithibitika kuwa kauli aliyoitoa hivi karibuni ni ya uchochezi basi watamtia mbaroni.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Jumapili iliyopita kwenye viwanja vya Sahara jijini hapa, Dk. Slaa, alitoa siku saba kwa jeshi hilo kuwakamata na kuwafungulia mashtaka watu wote waliotajwa kuhusika katika tukio la kuwacharanga mapanga wabunge wa chama hicho, Highness Kiwia wa Ilemela pamoja na Slvatory Machemli wa Ukerewe.

Wabunge hao walishambuliwa na kujeruhiwa kwa mapanga na silaha nyingine usiku wa kuamkia Aprili Mosi, mwaka huu katika eneo la Ibanda katika Kata ya Kirumba, wakati wakitoka kwenye mkutano wa ndani wa Chadema kwa ajili ya kuandaa mawakala wa chama hicho kwa ajili ya kusimamia kura za uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika siku hiyo katika Kata ya Kirumba.

Kiwia na Machemli baada ya kujeruhiwa na kupata majeraha makubwa, siku hiyo walihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya muhimbili jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, huku wakilituhumu Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwamba liliwalinda waliotenda uhalifu huo.

Wabunge hao pia walidai kuwa wanawafahamu waliowajeruhi, lakini wanashangaa sababu za polisi kutowakamata.

Kutokana na malalamiko ya wabunge hao, Idara ya Upelelezi ya Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam ilituma timu ya makachero waliowahoji wabunge hao wakiwa wodini Muhimbili kuhusiana na tukio hilo.

Katika mkutano wa hadhara wa Jumapili jijini hapa, Dk .Slaa alibainisha kuwa, iwapo watuhumiwa hao hawatakamatwa katika kipindi hicho cha siku saba, basi atahamasisha wananchi wa Mwanza wakusanyike na kwenda kuteka kituo cha polisi.

Hata hivyo akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Phillip Kalangi, alisema wanaichunguza kauli hiyo ya Dk. Slaa na kama ikibainika ni ya uchochezi basi watamtia mbaroni na kumfungulia mashtaka.

Alisema kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa utaratibu iliojiwekea na siyo kufuata maelekezo wala mashinikizo ya wanasiasa.

“Ni kinyume cha sheria kuipangia serikali muda na jinsi ya kutekeleza majukumu yake, sisi polisi tuna taratibu zetu za kushughulikia uhalifu na wahalifu. Kauli aliyoitoa Dk. Slaa ni sawa na uchochezi, hivyo tunamchunguza ikibainika ni kweli tutamkamata,” alisema Kalangi.

Hata hivyo, Kamanda Kalangi, hakueleza kwa undani lini uchunguzi wa kauli ya Dk. Slaa utakamilika.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa na jeshi hilo kuhusu tukio la wabunge wa Chadema kukatwa mapanga, Kalangi, alisema Jeshi la Polisi limewatia mbaroni watu wengine watatu, hivyo kufanya idadi ya waliokamatwa kwa tuhuma za kuhusika katika tukio hilo kufikia 18.

Awali Jeshi hilo lilisema kuwa watu waliokamatwa walikuwa ni 15.

Bila kutaja majina ya watuhumiwa wa tukio hilo, Kamanda Kalangi, alisema kwamba baadhi yao bado wanaendelea kushikiliwa na kuhojiwa, lakini wengine wameachiwa kwa dhamana.

Tangu wabunge hao walipocharangwa mapanga na kujeruhiwa vibaya, kumekuwepo na lawama kutoka kwa viongozi wa Chadema dhidi ya Jeshi la Polisi kushindwa kuwachukulia hatua watu waliotajwa kuhusika.

Katika madai yake aliyoyatoa jijini Mwanza kwenye mkutano wa hadhara Jumapili iliyopita, Dk. Slaa, alidai kuwa watu wake akiwemo Diwani Mteule wa Kata ya Kirumba, Dani Kahungu, wametoa ushirikiano wa kutosha kwa Polisi ikiwa ni pamoja na kuwataja watuhumiwa lakini hakuna aliyekamatwa.

Siku moja baada ya kutokea tukio hilo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto kabwe, ambaye alikuwa jijini Mwanza kwa ajili ya uchaguzi huo, alidai kuwa miongoni mwa watu waliohusika kuwashambulia na kuwajeruhi wabunge hao ni kiongozi mwandamizi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mwanza.

Aidha, baadhi ya viongozi wa Chadema mkoa wa Mwanza wamekuwa wakidai kuwa makada kadhaa wa CCM mkoani Mwanza walihusika katika kitendo hicho cha kihalifu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles