Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Buriani Steven Kanumba `The Great Pioneer`

8th April 2012
Print
Comments

Lau jana ingelikuwa ni Aprili Mosi, huenda ningeiamini taarifa ya jumbe mfupi wa simu niliotumiwa na mmoja wa rafiki zangu, juu ya kifo cha muigizaji nyota nchini, Steven Charles Kanumba 'The Great Pioneer' kwa kuamini ilikuwa utani wa 'Siku ya Wajinga'.

Hata hivyo kwa kuwa jana ilikuwa Aprili 7, sikuipuuzia taarifa hiyo na badala yake kuhaha kusaka ukweli wake kwa watu wa karibu wa msanii huyo wakiwemo waigizaji wenzake.

Nilimpigia Jacob Stephen 'JB', Jackline Wolper na Soud Ally, bahati mbaya simu zao hazikupatikana.

NI kajaribu kwa Patcho Mwamba aliipokea mara moja na kitu cha kwanza kabla ya salamu ni kutaka uthibitisho kama Kanumba alikuwa kafa.

"Ndio ndugu yangu, Steven Kanumba hatunae tena duniani, amefariki usiku wa kuamkia leo akiwa nyumbani kwake," alisema Mwamba na kuufanya moyo wangu ukaribie kusimama kwa mshtuko!

Sio kwamba ni mara ya kwanza kusikia vifo vya wasanii au sijawahi kupatwa na msiba hivyo kushtuka namna hiyo, la! Kifo cha Kanumba kimekuwa cha ghafla sana na hakuna aliyetarajia, japo Mungu ameshatubainishia kwenye maneno yao kuwa kifo huja ghafla.

Niliamua kujitutumua kumuuliza Patcho aliyekuwa bado hewani, chanzo cha kifo na kunieleza kama nilivyodokezwa na rafiki yangu kwamba, Kanumba alianguka nyumbani kwake baada ya kusukumwa na mpenzi wake ambaye ni muigizaji wenzie, Lulu Michael.

Kwa hakika, kifo kinauma na kinaumiza, lakini nadhani kwa mashabiki wa filamu nchini watakuwa wameumizwa na kifo cha Kanumba kutokana na ukweli ni majuzi tu alikuwa akiwabainishia kuwa kuna kazi yake mpya inatarajiwa kuingia mtaani, 'Ndoa Yangu'.

Filamu hiyo aliyoigiza na wakali kama Patcho Mwamba na Jackline Wolper ipo jikoni na mie nimekuwa nikiandikia sana kwenye gazeti hili, ikiwa ni kazi mpya baada ya kuachia 'Kijiji Chatambua Haki' iliyotoka mwezi uliopita.

Binafsi sina cha kuelezea kuhusu Kanumba, zaidi ya kusema alikuwa rafiki wa kila mtu, mchapakazi na aliyekuwa na ndoto nyingi za maendeleo katika sanaa ya filamu nchini.

Ni majuzi tu alikuwa amerejea toka Ghana kushiriki tamasha la filamu ambapo kazi yake ya 'Devil's Kingdom' aliyoigiza na Ramsey Nouah Jr', nyota wa Nollywood ilionyeshwa katika tamasha hilo na filamu nyingine kali za nyota mbalimbali.

Nakumbuka mara ya mwisho nilipowasiliana nae, alikuwa akisema kama kuna anachoota ni kuja kuwa miongoni mwa waigizaji wa Hollywood, mahali ambapo aliwahi kuitembelea mwaka juzi na kueleza kujifunza mambo mengi katika sanaa yake. Kwa vile kila nafsi ni lazima itaonja mauti, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa utendaji wake kwani ni yeye aliyempenda zaidi Kanumba na kuamua kumchukua wakati wengi wetu tukimhitaji zaidi ulimwenguni.

Steven Charles Kanumba, alizaliwa Januari 8, 1984, huko Ngokolo, Shinyanga akiwa ni mtoto pekee wa kiume kati ya watatu wa bwana na bibi Charles Kusekwa Meshack Kanumba.

Sanaa yake aliianza kuinyesha tangu akiwa kinda wakati akisoma Shule ya Msingi Bugoyi na pia kuimba kwaya kanisani kabla ya kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Mwadui ambapo aliendelea kutamba katika fani ya sanaa.

Alipohamia jijini Dar kuendelea na masomo ya Sekondari katika Shule ya Dar es Salaam Christian Seminary aliendelea kutamba na fani hiyo na alipojiunga na Jitegemee tayari alishaanza kupata jina kutokana na kutua kundi la Kaole Sanaa mwaka 2002.

Michezo mbalimbali aliyoigiza akiwa na kundi hilo kupitia vituo vya ITV na TBC1 (zamani TVT) kama Jahazi, Dira, Zizimo, Tifani, Sayari, Taswira, Baragumu na Gharika ilimjengea jina kubwa kabla ya kujiengua kundini 2006 na kuanza kucheza filamu.

Baadhi ya kazi zake ni pamoja na 'She is My Sister', 'Dar to Lagos', 'Cross My Sin', 'The Director', 'Hero of the Church' na nyinginezo akishirikiana na wakali wengine wa Nolllywood kama Mercy Johnson, Nkiru Silvanus, Femi Ogedegbe na wengineo.

Kanumba aliyekuwa akimiliki kampuni binafsi ya kutayarisha filamu ya Kanumba The Great Films, mbali na uigizaji, pia alikuwa mtunzi, mtayarishaji na muongozaji wa filamu kazi yake ya mwisho ambayo inatarajiwa kuingizwa sokoni ni 'Ndoa Yangu'.

Baadhi ya kazi zake ni Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Dar to Lagos, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears, Unfortunutes Love, My Valentine, The Shock, Deception na nyinginezo zinazomfanya avune tuzo mbalimbali.

Miongoni mwa tuzo alizowahi kupata msanii huyu ni pamoja na ile ya IJUMAA Sexiest male bachelor of the year-2006, Best Actor of the Year (Baab Kubwa Magazine)-2006 The Best Actor in Tanzania (Hollywood John Wayne International Awards)-2007,

Honorary Award (Tanzania Film Vinara Awards)-2008, Best Actor-2007-2008 ya (SHIVIWATA) na Uigizaji Bora na Mtayarishaji Bora-Filamu Central-2010.

Wasanii mbalimbali waliowahi kufanya kazi na Kanumba kama Patcho Mwamba, Skyner Ally, Kipemba na wengine wamedai kusikitishwa na kifo cha mwenzao na kumtakia Nsafari njema huko aendako pamoja na kuwatakia moyo wa subira ndugu, jamaa na mashabiki wa msanii huyo.

"Inauma, ni ghafla mno bro!' alisema Mwamba, wakati Skyner alisema mpaka sasa haamini kama Kanumba kaondoka, huku Kipemba alisema ameshtushwa, lakini hana budi kumhimidi Mungu kwani ndiye mpangaji wa yote.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles