Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tanesco `yamvimbia` Magufuli

4th May 2012
Print
Comments
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limekaidi agizo lililotolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, la siku saba kuhamisha nguzo zilizo katika hifadhi ya barabara kupisha mradi wa ujenzi wa babaraba ya mabasi yaendayo kasi (DART) na kutaka wanaojenga barabara hiyo kufanya kazi hiyo.

Dk. Magufuli alitoa agizo hilo kwa juzi jijini Dar es Salaam alipotembelea Dart na kuelezwa na mkandarasi anayejenga barabara za mradi huo kuwa moja ya vikwazo vinavyochelewesha utekelezaji ni nguzo za umeme.

NIPASHE jana ilimtafuta Mkurugenzi wa Tanesco, William Mhando, ili kujua wamejipanga vipi kutekeleza agizo la Waziri Magufuli, lakini mmoja wa wasaidizi wake ambaye hakutaja jina lake, alisema yuko safarini nchini Sweden.

Hata hivyo, Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema zoezi la kuhamisha nguzo linatakiwa kufanywa na Wakala wa Barabara (Tanroads) kupitia mkandarasi wake.

Badra alisema kuwa Tanroads pia ina jukumu la kumlipa mkandarasi huyo kwa kufanya kazi hiyo kwa niaba yake na kuongeza kuwa jukumu la Tanesco ni kutoa ushauri wa kiufundi tu.

“Zoezi la kuhamisha nguzo linatakiwa kufanywa na Tanroads kupitia mkandarasi wao kwa gharama zao, sisi Tanesco kazi yetu ni kutoa ushauri wa kitaalamu wa kiufundi,” alisema Badra.

KAULI YA NGELEJA

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ambaye wizara yake ndiyo yenye dhamana na Tanesco, alipoulizwa na NIPASHE jana kama shirika hilo litatekeleza agizo la Dk. Magufuli, hakutaka kuingia kwa undani kuhusiana na suala hilo, zaidi ya kusema ni la kiutendaji na Tanesco ndio wanaohusika na utekelezaji wake.

“Hilo ni suala la kiutendaji, Tanesco ndio wanaohusika na utekezaji wake,” alisema Waziri Ngeleja.

Ujenzi wa DART unaofanywa na mkandarasi huyo kutoka kampuni ya Stra Bag ya Ujerumani unahusu barabara za  Kimara-Ubungo, Morocco-Magomeni, Jangwani-Fire na Kariakoo-Kivukoni.

Juzi alipotembelea ujenzi wa mradi huo, Magufuli alielezwa na mkandarasi huyo kuwa baadhi ya changamoto wanazozipata ni pamoja na nguzo za umeme zilizoko barabarani, mabomba ya maji na baadhi ya vifaa kukwama bandarini.

Aidha, alielezwa vikwazo vingine kuwa ni miundombinu ya maji na kukwama kwa vifaa bandarini.

Baada ya kuelezwa hivyo, aliitaka Tanesco kuondoa nguzo zake ndani ya siku saba vinginevyo Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) watazing’oa.

Dk. Magufuli alimuagiza Mtendaji Mkuu wa Tanroad, Patrick Mfugale, kuhakikisha analisimamia suala hilo na endapo Tanesco haitatoa nguzo hizo wazitoe ili mradi huo usikwame.

Waziri Magufuli alisema kama itashindikana na mradi huo kukwama, atakwenda kumweleza mkubwa wake, ambaye hata hivyo, hakumtaja kwa jina.

Juzi Waziri Wagufuli pia aliahidi kulitafutia ufumbuzi suala la mabomba ya maji yanayopita katika barabara za mradi kwa kukutana na Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya.

Kuhusu kukwama kwa vifaa vya kampuni ya ukandarasi, aliahidi kuwa atakutana na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment