Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

TBS, FCC wasaidie kukomesha simu feki

15th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Mwaka juzi akiwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (Excellence in Journalism Awards –EJAT), Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alisema kuwa wakati wa utawala wake walipofungua milango ya kiuchumi na kuruhusu sekta binafsi kujiingiza katika kuendesha uchumi, miongoni mwa athari zilizojitokeza ni kujipenyeza kwa ‘majongoo na wadudu wengine’ kupitia dirishani’ kuchafua fursa hiyo.

Mzee Mwinyi ambaye alikuwa amealikwa kama mgeni rasmi kwa kutambua mchango wake katika kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari, aliwakumbusha wanahabari kwamba ni wajibu wao kuandika habari za kusaidia majongoo na wadudu waliopitia dirishani kuondoka katika uchumi ili soko huria liwe na manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Jumamosi iliyopita Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) ilifanya semina ya nusu siku kwa wahariri wa vyombo vya habari ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya habari, mawasiliano na teknolojia (ICT), ambayo pamoja na mambo mengine athari zinazofanana na zile za jongoo kutumbukia katika fursa ya ufunguaji wa milango ya kiuchumi ilijitokeza.

Kilichojitokeza ni changamoto kubwa ya kuzidi kuzagaa katika soko simu za mikononi zenye ubora wa kiwango cha chini ambazo zinasukumwa katika sekta ya mawasiliano ambayo inakuwa kwa kasi kubwa, hasa ya simu za mokononi zikikadiriwa kuwa na laini milioni 25 ambazo zimeuzwa kwa wateja hadi sasa.

Kutokana na kuzagaa kwa simu hizo zenye ubora wa kiwango cha chini, kumeongeza changamoto ya taka zinazotokana na vifaa vya kielektroniki wakati hakuna sera wala kanuni zinazodhibiti aina ya taka hizo ambazo ni hatari zaidi kwa mazingira hasa kutokana na kuwa na asilia ya plastiki kwa kiwango kikubwa.

Uzagaaji wa taka hizi kwa kiwango kikubwa unachangiwa na tamaa ya wafanyabiashara wenye nia ya kujinufaisha na kukua na kupanuka kwa mawasiliano ya simu za mkononi, hivyo kuingiza nchini simu zenye ubora wa chini ili kupata wateja kwa haraka, lakini wakati huo huo zikiwa hazidumu kwa muda mrefu hivyo kuwa moja ya chimbuko la taka nchini.

Ingawa TCRA wanaamini kwamba utaratibu wa kupunguza kodi kwa vifaa vya eletroniki kama simu utasaidia upatikanaji wa simu bora na zenye viwango, kwa ujumla eneo hilo bado linakabiliwa na changamoto kubwa kwa sababu inavyoonekana sasa ni kama serikali imejitoa kabisa kusimamia aina ya vifaa vinavyoingizwa nchini.

Kwa upeo wetu, mamlaka zenye wajibu wa kusimamia eneo hili, hususan Shirika la Viwango nchini (TBS) na Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC), hazijafanya kazi ya kutosha ili, kwanza kuepusha nchi kugeuzwa dampo la bidhaa za elektroniki zenye ubora wa chini na mbovu, lakini la muhimu zaidi kusaidia kuokoa fedha kidogo za kigeni ambazo zinahitajika sana kutumika kuagiza bidhaa ambazo kimsingi hazisaidii kubadili hali ya wananchi wetu.

Kwa vyovyote itakavyoangaliwa, kupanuka kwa sekta ya mawasiliano, hususan sekta ya ICT, kunaacha mwanya mkubwa sana kwa watu laghai kuwatumbukiza watu wetu katika umasikini ambao ni vigumu kung’amua kwa kuwa vyombo vya usimamizi ama vimelala usingizi wa pono, au hata kama viko macho, basi havina weledi wa kina juu ya ni kitu gani hasa kinapaswa kufanywa ili kulinda walaji wa bidhaa za kieletroniki, hasa simu za mkononi.

Ni kumtumbukiza mtu katika umasikini kama atadhani kuwa ananunua simu kwa bei nafuu lakini haimalizi mwaka, hivyo kujikuta kila baada ya muda si mrefu akinunua nyingine. Matumizi ya namna hii yanamsababishia kutumia fedha nyingi kununua simu kwa sababu tu soko limefurika bidhaa duni.

Tunaamini kwa kuwa sasa nchi imefunguka, hatua zinastahili kuchukuliwa na mamlaka ya usimamizi wa biashara ili soko huria liziwe ni kisingizio cha kumwaga katika soko la Tanzania bidhaa dhaifu kama ambavyo tunashuhudia kwa sasa kwa simu za mkononi.

Madhara ya bidhaa hizi ni makubwa kuliko inavyoweza kelezwa kwa maneno matupu, ni kutokana na ukweli huu tunasema kwamba pamoja na Watanzania kwa ujumla wetu kuungana na TRCA kuadhimisha wiki ya mawasiliano, ni vema pia tathmini inafanywe kama kweli tupo katika mstari uliyonyooka wakati huu tukifurahia kuimarika na kupanuka kwa sekta ya mawasiliano ya simu nchini.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles