Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

….Mwananyamala watishwa

29th June 2012
Print
Comments

Madaktari wa Hospitali ya Mwananyamala wameagizwa kuendelea kutoa huduma kwa mujibu wa ratiba zao na kila baada ya saa tatu uongozi utakuwa unafanya ukaguzi katika kila eneo kuhakikisha huduma inaendelea kutolewa kwa wagonjwa.

Katibu wa Hospitali hiyo, Dk. Edwin Bisakala, alisema daktari yeyote atakayekosa kutoa huduma kwenye kitengo chake akibainika hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Alisema tayari Serikali imetoa maelekezo na kuagiza kuwa yeyote ambaye hajafika kazini basi wamepewa mamlaka ya kumuondoa ili kuendeleza kudumisha nidhamu ya kazi.

Dk. Bisakala aliongeza kuwa hata kama Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamegoma, tayari Serikali imetoa mwongozo wa kuwapeleka wagonjwa wa rufaa katika Hospitali kubwa za binafsi ambazo tayari Serikali imefanya mazungumzo nazo.

TANGA: NI ITIKADI ZA KISIASA

Tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Dk. Ulimboka kumepokelewa kwa hisia tofauti na wananchi wa mkoa wa Tanga huku baadhi wamedai ni kutokana na itikadi za kisiasa.

Wakizungumza na NIPASHE jana, walisema nchi imekumbwa na malumbano ya kisiasa ndani ya chama tawala na vyama vya upinzani hivyo tukio hili limetokea ili kuipaka matope serikali ya CCM kwa wananchi ionekane imehusika.

 “Serikali ina matatizo na inalalamikiwa sana tunakubali lakini kwa suala hili ni wazi utaona kuwa kuna watu wamejipanga ili kuichafua serikali na kutaka serikali itupiwe lawama”, alisema Haji Zuberi mkazi wa Jijini Tanga.

Wananchi hao wameiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka ili kuwabaini waliohusika na kitendo hicho.

IRINGA WALAANI

Baaadhi ya wakazi wa mikoa ya Iringa na Njombe, wamelaani tukio la kushambuliwa kwa Dk. Ulimboka na kueleza kuwa tukio hilo limetokana na chuki za watu wenye mrengo wa upande mmoja wa kisiasa ambao wanapingana na hatua ya madktari kuendesha mgomo.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, waliitaka serikali kufanya tathimini ya kina kuhusu aina ya ripoti ambazo imekuwa ikizifanya kwa gharama kubwa pasipo kuwekwa hadharani majibu ya chunguzi hizo.

Juma Mwase mkazi wa Makambako katika mkoa wa Njombe, alisema pamoja na serikali kuunda tume inapaswa kulaumiwa kutokana na kujenga desturi ya kuunda tume nyingi za uchunguzi na baadaye kuficha ripoti hizo baada ya kazi kukamilika.

Mkazi wa Manispaa ya Iringa, Hendrick Kipande, alisema kutekwa kwa Dk. Ulimboka ni hujuma dhidi ya madaktari ambayo inafanywa kwa nia ya kuwatisha badala ya kusikiliza madai yao.

Imeandikwa na Leonce Zimbandu na Jimmy Mfuru, Sanula Athanas, Yoramu Mrobezi na Nebert Msokwa, Dar; Godfrey Mushi; Iringa na Lulu George, Tanga





 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment