Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kampuni za simu zisibweteke

25th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Juzi Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia alitoa wiki mbili kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzungumza na kampuni za simu nchini ili zitoe majibu kuhusiana na kuwepo kwa matatizo ya huduma za simu na lini yatatatuliwa.

Agizo hilo alilitoa alipotembelea ofisi za TCRA kujionea utendaji kazi wake na alisema kuwa pamoja na kukua kwa sekta ya mawasiliano nchini, lakini kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wateja wanaotumia huduma za simu kwamba zinasumbua.

Ingawa Naibu Waziri huyo alisema anazungumza kama mwananchi wa kawaida ambaye pia anatumia huduma hizo, alisema mbali ya kusikia malalamiko kutoka kwa wananchi, pia ameshuhudia kuwepo kwa matatizo ya mitandao ya simu kwani kuna kero nyingi kama vile kupiga simu ukaambiwa haipatikani hata kama iko hewani, au ukakatwa fedha nyingi tofauti na matumizi, lakini tatizo lingine ni lile la kutumiwa ujumbe mwingi wa promosheni.

Wakati Naibu Waziri akitoa maagizo hayo, alikumbusha kuwa haiwezekani kampuni za simu zikawa zinatumia fedha nyingi katika promosheni pasipo kujali kuweka miundombinu yao vizuri, hali aliyosisitiza ni lazima ifanyiwe kazi haraka.

Hakuna mtumiaji yeyote wa simu za mkononi atapingana na ukweli aliosema Naibu Waziri. Ni kweli kwamba kampuni za simu zimeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya mawasiliano; yamerahisisha ufanyaji kazi katika nyanja nyingi; yamepunguza gharama za kusafiri kutoka kituo kimoja kweli kingine kufuatilia kitu ambacho kingeweza kutatuliwa kwa kuzungumza kwa simu tu. Kwa kifupi mapinduzi ambayo yamefikiwa katika huduma za mawasiliano ya simu ni makubwa ajabu.

Kuna maeneo ambayo hakika kwa miaka mingine 50 ya Uhuru wa Tanzania yasingefikiwa kwa mawasiliano ya simu kama tungeendelea kutegemea mawasilino ya simu za kuunganisha kwa mkonga; tunapongeza kwa dhati kabisa kwamba hatua zilizopigwa zimefungua nchi, zimewezesha maeneo ya vijijini ambayo yalikuwa yametengwa katika mawasiliano ya kisasa kufikika kirahisi zaidi.

Leo hii mwenye ndugu yake aliyeko kijijini anawasiliana naye kirahisi, ana uwezo wa kumpelekea fedha akiwa huko huko kijijini, lakini pia ana uwezo wa kuwasilisha nyaraka za kiofisi akiwa huko huko kijijini bila kutaabika kusafiri umbali mrefu ilmradi tu awe na huduma ya intanet kupitia huduma za simu za mkononi. Haya yote ni mapinduzi makubwa ambayo yamefikiwa katika kipindi cha chini ya miaka 20.

Hata hivyo, pamoja na maendeleo haya tunayofurahia leo, tayari kampuni za simu zikiwa zimeuza takribani laini milioni 25, kuna shinda kubwa zimeanza kujitokeza kama alivyodokeza Naibu Waziri. Kero zilizoanishwa hapo juu zinaanza kumomonyoa furaha na neema ambayo imeletwa na hatua zilizopigwa na kampuni za simu.

Tunaangalia kero hizi sawa na kile Waswahili wanachosema ‘mgema akisifiwa sana tembo hulitia maji.’ Inavyoelekea kwa sasa kampuni za simu zimejikita zaidi katika kusaka wateja wapya; kama vile kupitia promosheni za aina mbalimbali, lakini nguvu ndogo ikielekezwa kuimarisha miundombinu yake kiasi cha kujikuta ikizidiwa na idadi ya wateja hivyo kushindwa kuwahudumia vema.

Kwa mfano, tabia ya simu kupigwa na kujibiwa haiko hewani wakati mtu ameishikilia mkononi ni kielelezo cha kuzidiwa nguvu kwa mfumo wa mawasiliano wa kampuni hizi; kutiririsha ujumbe wa promosheni usiku na mchana kwa wateja ni aina nyingine ya kubweteka katika mafanikio kiasi cha kuanza kukosa heshima kwa wateja; licha ya ukweli kuwa ujumbe huu ni usumbufu pia ni kuingilia haki binafsi ya wateja ya kuamua apelekewe ujumbe upi na asipelekewe upi.

Tunakumbuka wakati TCRA wakiadhimisha wiki ya mawasilino mapema mwezi huu, suala la wateja kutiririshiwa ujumbe wa kulazimishwa kushiriki promosheni za kampuni za simu liliibuliwa na kwa kweli TCRA waliahidi kufuatilia suala hilo. Ujumbe huu umekuwa ni kero kwa sababu hata pale mteja anapotaka kuwaambia wasimtumie tena hana jinsi ya kufanya kwa hiyo ni kama ameambiwa apende asipende atapelekewa ujumbe huo tu.

Tumesema na tunarudia kuwa kampuni za simu zimeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya mawasiliano, zimefungua maeneo ya pembezoni mwa nchi yaliyokuwa hayafikiki kuingia katika mtandao wa mawasiliano, hii ni kazi nzuri; hata hivyo, tunasema kuwa wasije kuingia katika mtego wa mgema aliyesifiwa akalitia tembo maji, kwa maana hiyo kampuni hizi zijidadisi na kujihoji zenyewe kama zinawatendea haki wataja wake hasa katika maeneo hayo yanayolalamikiwa na hivyo kuchukua hatua za kurekebisha hali ya mambo. Siyo lazima kusubiri TCRA ndipo kuchukua hatua.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles