



Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Margareth Sitta, amesema bajeti iliyotengwa kwa ajili ya sekta ya afya haikidhi mahitaji.
Amesema ufinyu wa bajeti hiyo unasababsha upatikanaji wa dawa hasa katika maeneo ya vijijini kuwa mdogo.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati akizindua rasmi mtandao wa wadau wa kuboresha manunuzi ya dawa na ufunguzi wa warsha ya waangalizi wa taratibu za ununuzi wa dawa.
Alisema awali waliomba Serikali itenge Sh. bilioni 198 kwa ajili ya ununuzi wa dawa lakini kiasi kilichotolewa ni Sh. bilioni 62 tu.
“Na tulipolalamika wameongeza Sh. bilioni 5 lakini hata hivyo tunaona kuwa hazitoshelezi.” Alisema.
Aidha, alisema fedha zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa bado ni ndogo kutokana na Bohari ya Madawa (MSD), kudai zaidi ya Sh. bilioni 41 fedha ambazo zinatakiwa kulipwa mapema ili kuwezesha bohari hiyo kufanya kazi zake vizuri.