Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Waziri wa Fedha apewa ilani

24th May 2012
Print
Comments
Waziri mpya wa Fedha, Dk. William Mgimwa

Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi imesema kuwa bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2012/2013 itapaswa kuelekezwa zaidi katika kuboresha uzalishaji na usambazaji wa vyakula kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi wengi.

Katika bajeti yake ya mwaka huu (2011/2012), serikali ilitenga zaidi ya Sh. trilioni 13.5 ikiwa ni kiasi kikubwa zaidi ya ile ya mwaka 2010/2011 ambapo ilitumia Sh. trilioni 11.1.

Aidha, kamati hiyo imeitaka serikali ije na mkakati wa kibajeti kushughulikia tatizo la mfumuko wa bei, hasa katika sukari na mchele.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Victor Mwambalaswa, katika mahojiano na NIPASHE.

Mwambalaswa alisema hali ya maisha kwa wanachi kwa sasa ni ngumu kutokana na mfumuko wa bei ya vyakula inayosababishwa na kuporomoka kwa thamani ya Shilingi, hivyo bajeti ya mwaka 2012/13 inapaswa kuwa kubwa kuliko ya mwaka 2011/12.

Alisema serikali katika bajeti yake ya 2012/2013 itaelekezwa zaidi katika kuhakikisha mfumuko wa bei ya vyakula unadhibitiwa.

“Nimetembelea masoko bei ya sukari na mchele iko juu sana, hivyo kuna haja katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao itazame katika masuala ya mfumuko wa bei ya vyakula,” alisema Mwambalaswa na kuongeza:
“Serikali inapaswa kupunguza misamaha ya kodi ili ijiongezee mapato yatakayowezesha kuendesha wizara zake kwa kuwalipa mishahara wafanyakazi.”

Alisema serikali inapaswa kukusanya kodi kwa nguvu zaidi kuliko kusamehe ili iweze kujiendesha pasipo kutegemea misaada ya wafadhili.

Mwambalaswa alisema kamati yake itaitaka serikali kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha inasimamia na kutekeleza majukumu yake ya kukusanya kodi.

Alisema katika kuhakikisha makusanyo ya kodi yanaongezeka, serikali inapaswa kuhalalisha biashara ambazo siyo rasmi ili TRA ikusanye mapato zaidi.

“Biashara kama vile mama lishe, mashamba ambayo hayajapimwa na za wamachinga zipewe uhalali wa kibiashara ili Serikali iweze kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara hao na nchi itasonga mbele,” alisema Mwambalaswa, ambaye ni Mbunge wa Lupa.

MFUMUKO WA BEI

Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Takwimu Taifa (NBS) iliyotolewa Mei 15, mwaka huu, mfumuko wa bei kwa Aprili ulishuka hadi asilimia 18.7 kutoka asilimia 19.0 za Machi, mwaka huu.

Hata hivyo, pamoja na nafuu hiyo ya mfumuko wa be, NBS ilisema kuwa tangu Septemba mwaka 2010 Shilingi ya Tanzania imepoteza thamani yake kwa wastani wa asilimia 23 hadi ilipofika Mei mwaka huu.

Taarifa hiyo ya NBS pia ilionyesha kuwa vyakula vilichangia ongezeko la bei hizo kwa mchanganuo kwamba; mchele asilimia 3, mahindi asilimia 1.6, unga wa mahindi asilimia 0.5, vitafunwa asilimia 7.3, unga wa mihogo asilimia 6.7, mayai asilimia 2.1, siagi asilimia 2.9, machungwa asilimia 6.8, ndizi mbivu asilimia 4.8, maembe asilimia 12.8, papai asilimia 8.9 na nanasi asilimia 8.7.

Vyakula vingine na asilimia za kupanda kwa bei kwenye mabano ni mbogamboga (2.2), mihogo (7.7), vinywaji baridi (9.7); wakati bidhaa zisizo za chakula ni mavazi (0.9), gesi (3.9), mafuta ya taa (2.3), mkaa (5.3), petroli (3.9), na begi za mikononi (5.6).

MISAMAHA YA KODI

Akichambua ripoti za ukaguzi za mwaka 2010/2011 mjini Dodoma Aprili 14, mwaka huu baada ya kuziwasilisha bungeni, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alisema TRA imetoa misamaha ya kodi ya Sh. trilioni 1.2 sawa na asilimia 18 ya mapato yote.

Alisema hali hiyo ni hatari ukilinganisha na misamaha inayotolewa na nchi jirani za Kenya na Uganda.

Mei 18, mwaka huu, Waziri mpya wa Fedha, Dk. William Mgimwa, aliliambia gazeti hili kuwa kazi yake ya kwanza katika wadhifa huo ni kushughulika na mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa sarafu ya Tanzania inalindwa dhidi ya matumzi ya ovyo ya Dola ya Marekani.

Alisema mfumuko wa bei ni tatizo na ni lazima kujipanga upya katika kuimarisha mifumo ya kiuchumi nchini.

Dk. Mgimwa alisema juhudi hizo ni lazima ziende sambamba na mikakati ya kulinda thamani ya sarafu  ya Tanzania ambayo imekuwa ikiporomoka thamani yake kwa mfululizo.

Alisema hali hiyo ndiyo imechochea mfumuko wa bei kutokana na kuadimika kwa baadhi ya vyakula sokoni kwani usambazaji wake umekuwa mdogo tofauti na mahitaji ya nchi.

Wakati kiwango cha mfumuko wa bei kikionyesha picha hiyo, NBS pia ilisema kuwa kuanzia Septemba 2010 hadi Aprili 2012 Shilingi imepoteza thamani yake kwa wastani wa asilimia 22.75, kwa maneno mengine Sh. 100 ya Septemba 2010 sasa thamani yake ni Sh. 77.25.

Pia  alisema taifa linaweza kukabiliana na tatizo la mfumuko wa bei, kwa kuwa na utaratibu bora zaidi wa kuuza bidhaa nyingi zaidi nje ya nchini kuliko kuingiza na kuna haja ya wizara yake kujipanga na kuhakikisha kwamba inakuwa na sera nzuri ambazo zitachangia katika kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.

Waziri Mgimwa alisema: “Taifa limetumbukia katika mfumuko wa bei kwa sababu serikali huko nyuma ilichelewesha kupeleka fedha kwenda kwenye maeneo yenye maghala ya taifa yanayonunua chakula.”Alisema kuwa hali hiyo haitaachwa itokee tena.

Alisema mkakati mpya wa kuokoa thamani ya Shilingi ni kuhakikisha kwamba matumizi yote ya fedha na mahitaji ya nchi yanafanyika kwa fedha za Tanzania badala ya Dola ili kuliepusha taifa kuendelea kuathiriwa na hali hiyo.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles