Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Msaidizi wa Mahalu akana kuisababishia serikali hasara

9th May 2012
Print
Comments
Profesa Costa Mahalu

Mshatakiwa wa pili na aliyekuwa Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, Grace Martin (50), amekanusha kuisababishia serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 katika mkataba wa ununuzi wa jengo la ubalozi.

Hata hivyo, Grace aliiambia Mahakama jana kuwa alishiriki katika mchakato wa kupatikana mpaka kutia saini kwa mikataba miwili ya ununuzi wa jengo la ubalozi huo.

Kadhalika, aludai kuwa hatua hiyo ilifikiwa baada ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutoa kibali cha kufanyika mchakato wa kupata jengo la kudumu la ubalozi nchini humo.

Grace ambaye ni shahidi wa tatu wa upande wa utetezi alitoa madai hayo jana wakati akitoa utetezi wake huku akiongozwa na wakili wa utetezi, Cathbert Tenga, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, Illivin Mgeta, anayesikiliza kesi hiyo.

Alidai kuwa aliyekuwa balozi wakati huo, Profesa Costa Mahalu  (63), alistahili shukrani kwa kazi nzuri aliyoifanyia serikali na sio mashtaka yanayomkabili.

Alidai kuwa aliyekuwa Mhasibu wa ubalozi huo, Prosper Migwano, ambaye alihusika na utaratibu wote wa kutafuta mpaka kupokea nakala ya risiti za malipo ya jengo hilo, alifunguliwa mashitaka pamoja na wao, lakini anashangaa upande wa Jamhuri ulimfutia mashitaka na kumtumia kama shahidi kwa upande wa mashtaka dhidi yao.

”Nashangaa upande wa mashitaka kwamba aliyekuwa mtumishi na mhusika katika mchakato huu tulishtakiwa naye mahakamani hapa, lakini sijui ni kwa sababu zipi walimfutia mashtaka ambapo alikana kufahamu suala la masharti ya mmiliki wa jengo hilo kwa kuandikiana naye mikataba miwili...

Kitu cha kushangaza zaidi Jamhuri walimtumia kama shahidi na alikana kufahamu mikataba hiyo,” alidai Martin. Aidha, alidai kuwa mashtaka sita yanayomkabili sio ya kweli na kwamba hakuna ushahidi uliothibitisha tuhuma dhidi yake.

Jana upande wa utetezi ulifunga ushahidi wake baada ya mashahidi watatu, Grace, Profesa Mahalu na aliyekuwa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kutoa ushahidi dhidi ya tuhuma hizo. Hakimu Mgeta alisema pande zote mbili zitakabidhiwa mwenendo wa kesi Mei 16, mwaka huu ili ziweze kuandaa hoja za kama washitakiwa watiwe hatiani au la.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles