Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Okwi kwenda Italia Julai 4

25th June 2012
Print
Comments
Mshambuliaji tegemeo wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Simba, Emmanuel Okwi.

Mshambuliaji tegemeo wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Simba, Emmanuel Okwi, anatarajia kuondoka nchini Julai 4 mwaka huu kuelekea Italia kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio na timu mbalimbali zinazoshiriki ligi ya Serie A ya nchini humo.

Hata hivyo, tayari Simba imeshakubaliana na klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini kwa dau la Euro 550,000 (sawa na Sh. bilioni 1.07) endapo nyota huyo atashindwa kupata timu huko Italia.

Okwi ambaye alikuwa akiitumikia timu yake ya taifa ya Uganda (Cranes) bado yuko Kampala na atarejea jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii ili kukamilisha taratibu za safari.

Akizungumza jana na gazeti hili, Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa Okwi atakuwa Italia kwa muda wa wiki mbili na atakuwa chini ya wakala ambaye aliwasiliana na Simba kwa ajili ya kumtafutia timu mshambuliaji huyo.

Kamwaga alisema kuwa Simba imefurahi kuona kuwa nyota ya mchezaji huyo imefunguka na ndio malengo yake kuona inatimiza ndoto za wachezaji wake kupata timu zinazoshiriki katika ligi zilizoendelea.

Alisema pia Simba inajipanga kuhakikisha inasajili wachezaji watakaoziba nafasi ya nyota walioondoka na waliowaacha ili waweze kufanya vizuri katika msimu ujao wa ligi na mashindano ya kimataifa ambayo watashiriki.

Simba pia imeshapokea maombi kutoka kwa Orlando Pirates ya Afrika Kusini ikitaka kumfanyia majaribio mshambuliaji huyo mwenye miaka 19.

Wakati huo huo, Kocha mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, alirejea nchini jana usiku akitokea kwao Serbia ambako alikuwa likizo baada ya kumalizika kwa msimu.
Cirkovic ataanza kukinoa kikosi chake kuanzia Jumatano baada ya kurejea kutoka Mwanza.

Simba ikiwa chini ya Kocha Msaidizi, Amatre Richard, juzi ililipa kisasi kwa kuifunga Toto African magoli 2-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza.

Magoli ya Simba yalifungwa na Uhuru Suleiman na kiungo mpya wa timu hiyo kutoka AFC Leopard ya Kenya, Salim Kinje.

Jana jioni mabingwa hao wa Bara walitarajiwa kucheza mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Express ya Uganda kwenye Uwanja wa Kambarage uliopo mkoani Shinyanga.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles