Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wazazi pia wana wajibu udhibiti wa shule nchini

4th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Wakati Watanzania wakiendelea kutafakari matokeo ya mtihani wa kidato cha sita ya mwaka huu yaliyotangawa mwanzoni mwa wiki hii na Baraza la Mtihani la Taifa, huku hali ya ufaulu ikiongezeka kuliko ilivyokuwa mwaka jana, wamepokea habari za kusikitisha kuhusu Shule ya Sekondari ya Central iliyoko Dodoma Mjini, ambayo ina kidato cha kwanza hadi cha sita.

Habari hizo mbaya ni za amri ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, ya kuifunga kutokana na alichosema kuwa haina sifa zinazotakiwa kisheria.

Naibu Waziri huo, ambaye ameonyesha uhai katika kushughulikia tatizo la shule za kibabaishaji nchini kwa muda sasa, na hii ikiwa ni shule ya tatu kutangaza kuifunga kwa sababu za kisheria na kisera, alichukuwa uamuzi huo juzi akisema kuwa serikali imekwisha kuuandikia uongozi wa shule hiyo barua 17, ili irekebishe mapungufu yaliyopo shuleni hapo, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hadi anatoa amri hiyo.
 
Mapungufu ambayo Naibu Waziri huyo alisema yapo shuleni hapo ni pamoja na kutokuwa na walimu wenye sifa za kufundisha sekondari, kutokuwa na meneja wa shule aliyethibitishwa na Waziri wa Elimu na hati miliki ya shule hiyo kumalizika muda wake tangu mwaka 1978.

Alitaja mengine kuwa ni usajili wa shule hiyo kuwa wa shule wa msingi badala ya sekondari, mfumo mzima wa utoaji wa elimu na kutokuwa na fomu za uhamisho wala kujiunga na shule, kuwa na taarifa za kutatanisha juu ya idadi hasa ya wanafunzi wanaopata elimu shuleni hapo, wakati menejimenti inasema ina wanafunzi 430 na mara nyingine 605, orodha ya wanafunzi waliopo inaonyesha kuwa wapo 775.

Mbali ya meneja na mmiliki wa shule hiyo anakanusha kuwako kwa mapungufu hayo shuleni hapo, pia amekwenda mbali zaidi kuhusisha hatua hizo za kufungwa kwa shule yake kuwa ni mambo ya kisiasa.

Alisema kuwa shule yake ina usajili namba S 104 wa tangu mwaka 1996 kwa mitihani ya taifa ya kidato cha nne na S 307 kwa mitihani ya kidato cha sita.

Ni vigumu kujua katika hili kipi ni kweli na kipi kina walakini, lakini lililo wazi katika kadhia hii kuwa kiasi cha wanafunzi 700 wanakosa masomo kwa hatua za kufunga shule hii; kwa hiyo wanaathirika mno. Wanapata hasara wao na wazazi wao.

Katika kutafakari hali hii tunashawishika kwanza kukubaliana na hatua za serikali kuingilia kati katika masuala yote ya uendeshaji wa shule nchini, ili kuhakikisha kuwa kinachoendelea katika shule hizi ambazo kimsingi siku hizi zimekuwa ni biashara zaidi kuliko kutoa huduma ya elimu, ndicho kinakubalika kulingana na sera na sheria za utoaji huduma ya elimu nchini.

Kwa hiyo, iwe ni hisia au ni kweli, kama kuna maneno maneno yanazungumzwa kuhusu shule hii, ni wajibu wa serikali kuchukua hatua kutafuta ukweli husika, na hizi ni pamoja na kufanyika kwa ukaguzi wa kina juu ya uendeshaji na mwenendo wa shule husika. Tunaunga mkono hatua hizo kwa dhati kabisa.

Hata hivyo, tungependa hatua hizo za kuifunga shule ziendane pia na ufuatiliaji wa karibu kwa maana ya kutoa fursa kwa mmiliki wa shule kurekebisha kasoro zote zilizoorodheshwa na Naibu Waziri, na zikikamilika basi Wizara iruhusu iendelee kutoa huduma ya elimu kwa wananchi.
 
Tunasema haya kwa sababu, kadri huduma za elimu zinavyozidi kubinafsishwa kwa maana ya kuruhusu watu binafsi zaidi kujikita katika sekta hii, ndivyo tunazidi kushuhudia mambo ya ajabu yakijitokeza katika utoaji wa huduma hii.

Zipo shule zilizogundulika kujiendesha bila kuzingatia sera ya elimu nchini, zipo zilizogeuzwa kuwa vijiwe kwa vijana kwenda kujipumzisha tu na kuwa vitovu vya kulea maadili yasiyokubalika katika jamii, lakini wakati huo huo wazazi wakilipa mamilioni ya fedha kama ada wakiamini watoto wao wanasoma.

Tunaamini tangazo la Naibu Waziri litaamsha umma, hasa hasa wazazi wenye watoto katika shule mbalimbali nchini ili kufuatilia kujua kuna nini kinaendelea humo, hatua hizo ni muhimu ili kusaidia kurekebisha mambo kabla hayajawa mabaya zaidi.

Tukumbuke anayeathirika na shule za kibabaishaji ni mzazi na mtoto wake. Tuwajibike sote sasa kutokomeza janga hili katika utoaji elimu kwa watu wetu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles